Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mwanzo ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba niuunge mkono hoja juu ya bajeti aliyowasilisha Waziri wa Elimu kwamba, amewasilisha kiufundi kabisa, nampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kumpa pole Naibu Waziri wa Elimu kwa msiba ambao umempata. Basi, namwombea kwa Mwenyezi Mungu amtie nguvu na Marehemu Roho yake iweze kuwekwa mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri na Naibu Waziri, Wakuu wa Wizara kwa kazi ambayo wamekuwa wakiifanya pamoja na changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kusema kwamba, elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Bila elimu hakuna viwanda, bila elimu hakuna kilimo chenye tija, bila elimu hakuna afya bora na kadhalika. Hivyo, ningeomba sana, Wizara ya Elimu ifanye kazi ya kuboresha suala zima la elimu. Suala zima la elimu likiboreshwa, tunaweza tukawapata wasomi wazuri, watakaoweza kuendesha nchi hii na kuweza kuingia kwenye soko la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Wizara ya Elimu, kwa kuanza kutazama upya ufaulu wa darasa la saba. Ufaulu wa darasa la saba uanze sasa kwak kuzingatia vigezo vya kuingia kwenye elimu ya sekondari. Utaratibu wa mitihani wa kuchagua alama za a, b, c, d, tunawapata wanafunzi ambao wanakwenda sekondari wasiojua kusoma na kuandika. Hawa wanafunzi ambao wengine wana vipaji vile vya kubahatisha, wanabahatisha halafu wanaingia kwenye elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakiingia kwenye elimu ya sekondari wanawapa tabu Walimu wa sekondari namna ya kuwafundisha, kwa sababu inabidi sasa waanze kuwafundisha kwa uelewa zaidi, masomo yale ambayo yalikuwa ni ya darasa la saba wanaanza kuwafundisha huku sekondari. Kwa hiyo, naomba sana utaratibu ule wa awali, uliokuwepo mara ya kwanza uweze kurejewa ili kuondoa usumbufu kwa Walimu wa shule za sekondari kuanza kuwafundisha wale wanafunzi ambao hawakufaulu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara irejeshe utaratibu wa zamani wa kufanya masomo kwa kufikiri badala ya kufanya masomo kwa kuchagua. Wakifanya hivyo tutawapata watoto wanaojitambua, itawarahisishia Walimu kuwa na watoto wenye uelewa na ufaulu wenye tija kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa uboreshaji wa elimu uende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya Walimu na stahiki zao. Baadhi ya stahiki za Walimu wala hazihitaji kuwa na shida kiasi kwamba Walimu wanapata matatizo, wanapata shida za kuhangaika kufuata stahili zao. Walimu inajulikana siku zao za likizo, mwezi wa Sita ni mapumziko na mwezi wa 12 ni mapumziko, hivyo niiombe Wizara, kinapofika kipindi hicho, wanapojua kwamba Walimu wanataka kwenda likizo mwezi wa Sita, wale Walimu wanaotakiwa kwenda wawe wameandaliwa tayari nauli zao miezi miwili kabla, fedha zao zipelekwe kwenye Halmashauri ili Walimu hawa wanapokuwa wanakwenda likizo, wapewe nauli zao badala ya kuwakopa kwamba waende halafu watakuja kurudi ndipo wapate nauli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la teaching allowance. Walimu hawa, ndugu zangu, wanafanya kazi kubwa, wanafanya kazi kiasi kwamba hawana nafasi ya kupumzika, hawana nafasi ya kufanya shughuli nyingine za kuwaongezea kipato. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie utaratibu wa kurejesha teaching allowance ili Walimu hawa wapate moyo wa kufanya kazi, kwa sababu hawana njia nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wengine wanapata muda wa kwenda kufanya kazi kujiongezea kipato, lakini Walimu hawana nafasi ya kufanya hivyo kwa sababu wanakuwa na shughuli nyingi ambazo zinawafanya waendelee kufanya maandalizi kwa ajili ya wanafunzi kwa kesho yake. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Serikali, ombi hili ni la muda mrefu, ni vizuri basi wakaliangalia ili Walimu hawa walipwe hiyo teaching allowance ili iweze kuwasaidia katika kujikimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la madarasa haya ya awali. Madarasa ya awali, Serikali kwa kweli imefanya kazi kubwa kuona kwamba watoto wote waende shule. Hata hivyo, niombe basi kwa kuwa Walimu hakuna wa madarasa la awali, sana sana wanawachukua wale Walimu ambao ni watu wazima ndiyo wamewapangia kufundisha madarasa ya awali. Niombe sasa waandaliwe Walimu maalum watakaokuwa wanafundisha madarasa haya ya awali, badala ya kuwatumia wale Walimu ambao wanaona ni watu wazima waliopo kwenye madarasa mengine na kuwaleta kwenye madarasa haya ya awali. Vile vile iende sambamba na suala zima la kuwapa vile vitendeakazi vya kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, kwa sababu ruzuku inapelekwa kwa wanafunzi wale wa shule za msingi, basi ruzuku vile vile ya watoto wa shule ya awali, iunganishwe kwa kupelekwa kwenye shule za msingi ili angalau na wenyewe waingie kwenye hesabu, kwa sababu safari hii walipokuwa wamepeleka zile ruzuku, hawakuingiza kwenye orodha ya watoto ambao wako shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nizungumzie suala la upandishwaji wa madaraja. Naomba upandishwaji wa madaraja uende sambamba na mabadiliko ya mishahara ya Walimu…
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.