Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza kabisa naunga mkono hoja Wizara ya Maji hii, kwa kuwa Mheshimiwa Prof. Mbarawa, Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu, Naibu Katibu wanafanya kazi ambayo sikutegemea. Mheshimiwa Prof. Mbarawa anafanya kazi kama vile Mhandisi anapita mpaka anachimba mifereji yeye mwenyewe kwa mkono wake, sijaona Waziri anafanya kazi kama Prosefa kwa vitendo. Lakini tatizo wanaomuangusha ni wafanyakazi wake, watendaji wake, namwambia ukweli awe mkali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua mfano Namanyere, nimezungumza sana kuhusu Namanyere mpaka sasa Namanyere wamepata maji asilimia 15, hata huo mradi uliokuja Mheshimiwa Profesa Mbarawa huo mradi wa sasa Namanyere wapata asilimia 46 katika Mji wa Namanyere ambayo siyo kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kawaida mijini lazima wapate maji asilimia 86 mpaka 85, lakini pamoja na huo mradi mpya Namanyere wamepewa Mkandarasi watapa maji asilimia 46. Kwenye kitabu chako hiki ukurasa 146, umeandika imetengwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kupeleka umeme kwa ajili ya mradi wa Bwawa la Mfili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa umeme umeshafika na transfoma ipo angalia wasikupige changa la macho pae tulipohitaji ni mtambo wa umeme mashine, pump ya umeme kwenye Bwawa la Mfili. Nakuomba vilevile Mheshimiwa Waziri Mkandarasi aliyepewa bwawa la Mfili na mtaalam anayeshiriki kumpa lile Bwawa la Mfili kawatapishe pesa mara moja. Haiwezekani ile bwawa thamani yake ifike milioni 900, wakati ukipiga hesabu za haraka haraka lile bwawa haifiki hata milioni 300, haiwezekani lazima ufanye jitihada kwa uwezo wako ninavyokuamini lazima mkandarasi apanue lile bwawa au atapike zile hela moja, hamna kuonea huruma! Wamezidi kuchakachua kwenye mabwawa haya mabwawa ya maji wamezidi nchi nzima nilikuambia unda tume ufuatilie mabwawa ya nchi nzima kuna uchafuaji wa hali ya juu, miradi ya maji wageuza kama ndiyo vichaka vya kuibia pesa katika nchi hii haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza Bunge la Awamu ya Nne hapa wanaandika kabisa Ofisini wamekaa Ofisini anaandika neno kodisha gari kutoka Namanyere kwenda Dar es Salam kwa shilingi milioni 14 wakati gari milioni tatu, nimepakia mabomba ya shilingi milioni 98, Mheshimiwa nilidai, hakuna mabomba waliyopakia wala hakuna gari iliyokuja Namanyere. Anakaa Ofisini anakula hela kijanja kijanja, wafuatilie wote, Wakandarasi wameshirikiana na Maofisa wako kuiba hela za miradi ya maji, unda tume, kagua mradi kwa mradi ninavyokuamini upitie nchi nzima watapike pesa mara moja. Hakuna huruma kuwachekea chekea, wengine wamejenga maghorofa, wengine wamenunua majumba kwa ajili ya miradi ya maji katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ninao, maana yake walitaka kunihonga na mimi nikawakatalia, shahidi na Mbunge wa Chemba Ndugu Nkamia walikuja mpaka Bungeni hapa, nikawaambia mimi sihongeki wananchi wangu wamejipanga foleni kunichagua niwatetee, leo Namanyere hawana maji, mnipe pesa wananchi waangamie, kupata maji kwa ajili ya utamaa tamaa, wako kwa majina, hakuna kufichika, Mradi wa Maji Kirando kabla hujakuwa Waziri walikula shilingi milioni 201 Kirando hakuna kitu kilichotengenezwa.Walijenga vizimba 18 na wakanunua pump moja kwa shilingi milioni 200 waliandika certificate za uongo hela wanachukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimwambia Waziri aliyeondoka mbele ya bwawa na RAS ambaye leo ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI, anafahamu alikuwa RAS Sumbawanga; tukamwambia usiwalipe hawa pesa iliyobaki shilingi milioni 300 kwa sababu hili Bwawa la Mfili lazima likaguliwe, lakini walilipwa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huyo Mkandarasi kama yupo hajafa atapike zile hela, akapanue Bwawa la Mfili…(Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipe taarifa..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakajoka taarifa.

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsikia nataka kumpa taarifa Mhehsimiwa Mjomba wangu Keissy pale, anasema kwamba fedha zote hizo anazozitaja zimeliwa na wakandarasi, zimeliwa na watu ambao ni watendaji wa Serikali kwenye Jimbo lake la Nkasi. Lakini namshangaa sana kwa sababu mimi najua kabisa Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kumaliza mafisadi nchini, sasa hizo hela wanakulaje wakati mafisadi tumeshawamaliza kabisa katika nchi hii?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona mjomba wangu amekwenda vibaya, hivi mafisadi wamekwisha, juzi walitaka kuiba hata za ndege hapa juzi, wewe huna habari, kupaka rangi ya ndege tukasema shilingi milioni 300 wamekwisha mafisadi! Hata humu Bungeni wako mafisadi watakwisha wapi mafisadi. Mafisadi watakwisha labda mwisho wa dunia ndiyo wataisha mafisadi, nani kakuambia, mjomba uwe macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji kadhaa katika Jimbo la Nkasi Kaskazini ukianzia Masoro, Kata nzima ya Mkwamba kule Riele, Itindi, Tambaruka, Swaila hawana hata visima vya maji, Kakoma, Lunyala hakuna hata visima wananchi wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuomba ndugu yangu hata angalau kisima kimoja kimoja katika vijiji vyangu hawana kabisa maji; maji ni uhai nakuelewa kwa sababu unatenda kazi, unafanya kazi, unakemea uovu, nimekuona kwa macho yangu sasa jitahidi kuwabana kabisa fukua makaburi, wameiba miaka ya nyuma mjomba wangu, labda kwako Tunduma kama hawajaiba, wameiba sana hawa watu wa maji bila kuwaonea huruma wameiba sana; walikuwa wanapeana kijomba kijomba tender kama ufahamu wewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapewa tender ana- raise certificate kazi haifanyaki hamna kazi, Namanyere kwa ushahidi kabisa wewe uliona wapi mjomba kazi itoke gari Dar es Salam mpaka Namanyere unapajua Namanyere, gari fuso shilingi milioni 12 uliona wapi wewe! Ni kwenda Lubumbashi na kurudi! Nilidai risiti ya hiyo gari haikuonekana kwa nini tusifukue makaburi mnaogopa kitu gani? Ushahidi upo, mabomba sikuona nimekwenda kwenye Full Council nadai mimi risiti kwa yule mtu wa maji haoneshi. Gari liko wapi, nioshe gari, nipe namba ya gari haoneshi, nikaenda TAKUKURU hamna kitu jamani, tufanyaje nchi hii, tumsaidie Rais.

Mheshimiwa Profesa Mbarawa ninakuamini unda tume pitia mabwawa yote nchi nzima, miradi ya maji nchi nzima utakuta ufisadi wa hali ya juu. Tunashida ya maji kweli Serikali inaleta pesa, lakini wapi hakuna chochote, hakuna chochote, mfano najua Namanyere, uende Namanyere wewe mwenyewe unafahamu Mheshimiwa Waziri, juzi uliunda tume, wakaja Namanyere mpaka Kirando ulikuwa mradi wa shilingi bilioni 7.4 baada ya kuleta wakandarasi wapya na watu wa tume, mradi umegundulika bilioni 4.6 wewe mwenyewe shahidi. Kabla hujakuwa Waziri ule mradi ulikuwa umeshaibiwa hela, ulikuwa umeshaibiwa shilingi bilioni 7.4, ulipokuja Waziri ukataa nikakushawishi wewe ukakataa ukasema huu mradi haiwezekani tutume watu wa kwenda kule. Tumegundua ule mradi ni shilingi bilioni 4.6 tumeokoa shilingi bilioni tatu, Mheshimiwa sasa tutasema namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawambia Waziri yuko Waziri mmoja nikimtaja itakuwa aibu, akanambia utajuaje haya mambo Mheshimiwa Keissy, nikamwambia nitakushtaki kwa Mheshimiwa Rais wewe nyamaza kimya, akanyamaza kimya, naweza kumtaja. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Mtajeee!.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Anajijua, alinitisha humu Bungeni, Waziri mmoja alinitisha Bungeni wewe usiingilie mambo ya utaalamu, unajuaje utaalamu nikamwambia mzee hata kipofu atajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Prof. Mbarawa nakuamini, unda tume pita kila kijiji, pita kila mkoa siyo kama Waziri wengine unamletea taarifa anakwambia unajuaje, kwani mimi ni sanamu nisikose kujua, nikose kujua mimi? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumtishia nitakupeleka kwa Mheshimiwa Rais akatetemeka, unakuwa Waziri tukikwambia wewe unasema Mbunge utajuaje unashirikiana na mafisadi haifai kuwa hata Waziri wewe, bora utumbuliwe tu. (Kicheko)

WABUNGE FULANI: Mtajeee!

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, huku nyuma. (Kicheko)

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Keissy angetutajua tu na sisi tumjui bwana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy naomba uendelee.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tutamtaja hata Mheshimiwa Rais akiniita faragha nitamtaja, si anasikia Mheshimiwa Rais nitamtaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu hii miradi ya maji tumsifu Mheshimiwa Prof. Mbarawa maana yake anafanya kazi kwa vitendo, Mheshimiwa Aweso anafanya kazi kwa vitendo na wasaidizi wake wanafanya kazi kwa vitendo, naomba muendelee na msikubali makadirio wanawaletea ya uongo uongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashauri angalia certificate wanazoleta lazima mzipitie, siyo wanaandika certificate mnazipitia haraka haraka mnalipa hela, wakati mwingine ni hewa, ni unafiki ulikwenda Mheshimiwa Waziri ulikuja kule Mradi wa Kata ya Isale tangu umeondoka mpaka leo kama siyo ....DC, DC ndiyo amekuwa kama mkandarasi wa Nkasi anahamasisha wananchi wachimbe mtaro ili walipe yule mkandarasi, yeye hafanyi kazi yoyote, angalieni certificate hizi na nimeshukuru kwa sasa nasikia sheria imebadilika mkimpa mtu mkandarasi kwanza afanye asilimia 30 ya kazi ndio alipwe pesa, hiyo ndiyo sheria nzuri, sio mnaanza kumlipa hela mkandarasi ajaanza chochote hayuko kwenye site anakula pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nikuombe Mheshimiwa Waziri nakuambia ukweli Mradi wa Maji Kirando alikula makandarasi shilingi milioni 201 lazima azitapike, amejenga tu vizimba 18 na kila kizimba kimetumia mifuko mitano ya cement na aliyekula hela za mradi wa Bwawa la Mfili lazima atapike huyo mkandarasi lazima maana yake yeye ndio aliyemshawishi yule mtu akaandika pesa kama waligawana sisi hatujui nataka kujua kazi yetu ya Namanyere, wana Namanyere wana shida ya maji hawapati maji chini ya asilimia 16 mzee, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)