Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Solwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa naunga mkono hoja ni hoja ni nzuri. Mheshimiwa Waziri umeeleza vizuri sana wewe na Mheshimiwa Naibu Waziri na timu yako nzima ya Wizara hii ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na mimi niendelee tu kusema kwamba naunga mkono hii shilingi 50 ambayo ni hoja au ushauri wa Kamati na imeelezwa hapa. Sasa itatoka wapi, inaweza ikatoka kwenye mawasiliano au kwenye mafuta. Hivi mtu anayejaza mafuta kwenye gari lake au mtu anayetumia simu akaona kabisa shilingi 50 hii nailipia kwenye maji, inamuuma kweli? Ni suala la Serikali kuamua tu, ninyi amueni mambo yaishe, wanaojaza mafuta kwenye magari yao au watumiaji wa simu watalipa tena wanalipa wakiwa na furaha kwelikweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hii ni utekelezaji wetu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Maana yake tunakwenda kukamilisha ahadi tuliyoiweka kwenye ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, hili ni jambo jema sana Mheshimiwa Waziri wa Maji lichukue ukalifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa Ziwa Victoria ambao unatoka Solwa ambao Mheshimiwa Waziri ameutaja hapo unaokwenda Tabora. Mradi huu umetoka kwenye Jimbo langu unakwenda mpaka Nzega baadaye unakwenda Igunga na maeneo mengine. Ni mradi mkubwa sana, gharama yake nafikiri kwenye dola milioni 270. Ni mradi uliosanifiwa vizuri sana unakwenda kutibu tatizo la maji kwenye zaidi ya vijiji 50 katika Jimbo la Solwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu una uzuri wake sana na niishukuru sana Serikali tena kwa asilimia zote na nimshukuru Mheshimiwa Rais na wewe pia Mheshimiwa Waziri. Hata hivyo, kuna kata ambazo mmeziruka kwa maana ya kwamba ama mmeruka katika upembuzi yakinifu ama mmeziruka kwa maana ya kwamba vijiji vipo nje ya kilometa 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri anisikie, athari yake ni kwamba Kata hizo tano ni Bukene, Usule, Nsalala na Usanda maana yake ni kwamba mradi ukipita wanaona wenzao wanatumia maji na wao wamerukwa matokeo yake ni kwamba watakwenda kuhujumu mradi. Sasa hapo tutakwenda Waheshimiwa Wabunge kwenda kuongea nao acheni tunafanyia kazi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, una Katibu Mkuu Profesa mzuri sana, tuma timu hata kama vile vijiji viko nje ya kilometa 12 kwenye Kata hizi hasa Usule, Bukene, Nsalala na Usanda zikafanyiwa upembuzi ziingizwe. Hivi kweli mainjinia ambao tunao kweli katika Tanzania hii wanashindwa kwenda kufanya usanifu hata hivyo vijiji ambavyo viko nje ya kilometa 12 na wenyewe wakapata maji? Mimi sidhani na gharama siyo kubwa hivyo ili mradi ukipita upite moja kwa moja na mambo hayo yawe yamekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana Tinde mmeiingiza ilikuwa imerukwa. Mheshimiwa Aweso nakushukuru sana, Mheshimiwa Waziri tuliongea hayo mambo sasa hivi umetupa kibali Tinde vijiji vyake vyote vinapata maji ya Ziwa Victoria. Jana nimepata taarifa kwa maana ya kwamba tulikuwa tunahangaika kijiji kimoja cha Weleza kinapata maji sasa hii kimoja kimoja hapana, tufanye kwa pamoja mambo yote yaishe kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Solwa litakuwa ni mfano, hata National Housing wanavyojenga nyumba wanajenga nyumba moja wanasema hii ni ya mfano anapokuja mteja anaitizama ili aweze kuvutika kununua nyumba. Jimbo la Solwa mradi huu ukiisha nakwenda kuwa na vijiji zaidi ya 86 vyenye maji ya Ziwa Victoria na ni Jimbo la kwanza kabisa naweza ku-declare tumefika asilimia 85. Kwa hiyo, ni jambo jema sana, niishukuru sana Serikali yangu pamoja na Mheshimiwa Rais wetu. Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Mwakitolyo na Mwasekagi wa mwaka 2017. Mradi huu uko asilimia 85, tuna fedha kidogo sana imebaki bilioni 150, tume-raise certificate kwa ajili ya shilingi bilioni 63 ili zile kazi ndogo ndogo zikamilike. Sasa hivi wanatumia maji lakini kuna kazi ndogondogo za kumalizia ili mradi huu uishe moja kwa moja katika eneo la Mwakitolyo na Mwasekagi kwenye Kata ya Solwa. Naomba sana hili mlifanyie kazi, Katibu Mkuu unanisikiliza, tulipe hii bilioni 63 mkandarasi akamalize kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Mwakitolyo kwa kipekee kabisa Mheshimiwa Naibu Waziri nikushukuru sana na Mungu akubariki sana na kama una mke mmoja akupe wa pili, wa tatu na wa nne. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Mwakitolyo, huu mradi wa maji ni wa shilingi 1,400,000,000, ilikuwa fedha zake zimelipwa na mradi haukuweza kufanya kazi. Umekuja pale, ukaongea na Katibu Mkuu kwa simu na wananchi wanakusikia. Katibu Mkuu akajibu vizuri, nafahamu kazi iko vizuri, Tume imeenda na mpaka sasa mmeshachukua hatua. Ombi langu nataka sana uende haraka kwa maana najua kuna usanifu na design mpya inafanyika itengwe fedha ili wananchi wale wa Mwakitolyo ni wengi, pale kuna wachimbaji wadogo wadogo wengi sana, ni mji unaokuwa haraka sana, una fedha watu wanajenga nyumba za kisasa kabisa, nafikiri umeshanisikia suala hili utalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Keissy masuala ya mabwawa kuna changamoto makubwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza?
MWENYEKITI: Ya pili, malizia sentensi yako.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, duh, naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)