Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema leo na nawashukuru Wabunge wenzangu wote mlionipa pole wakati nimepata maradhi juzi; nashukuru sasa niko salama na nimejiunga na ninyi. Pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Engineer Manyanya kuwa Mawaziri katika Wizara hii, lakini pia nimpe pole sana dada yangu, Mheshimiwa Engineer Manyanya kwa msiba uliompata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima ya kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa ya Kamati yetu. Hata dada yangu, Mheshimiwa Susan naye leo kapendeza na anayafahamu kidogo mambo ya elimu kwa sababu alikuwa warden pale Chuo Kikuu akigawa vyumba kwa wanafunzi kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na jambo la kwanza, nataka kuzungumzia hili suala la ada elekezi, nasikia kwamba Serikali ina mpango wa kuja na mfumo huo. Nadhani suala la ada elekezi lazima Serikali ikae iliangalie kwa kina sana, kwa sababu hakuna mtu anayelazimishwa kumpeleka mtoto shule ya kulipia. Suala lililopo hapa ni kwa Serikali kusimamia na kuhakikisha shule zote za Serikali zinakuwa bora, lakini leo kumwambia mzazi, ama kumwambia mwenye shule, kwanza kuendesha shule ni gharama kubwa, hata yale mabasi tu wanalazimishwa kupiga rangi. Kwa kweli upo umuhimu mkubwa wa Serikali kuliangalia jambo hili na sidhani kama ni jambo la busara sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka niseme tu kwamba, kuhusu hiki Chuo Kikuu cha Saint Joseph, mimi ni mmoja kati ya watu walioathirika kwa sababu mtoto wa marehemu kaka yangu alikuwa anasoma kule Arusha. Chuo hiki kimefungwa, waliofanya makosa ni TCU, wamekifunga chuo hiki na wenyewe ndiyo waliotoa kibali cha kuanzishwa kwake. Mheshimiwa Waziri leo amesema amevunja Bodi, hivi watoto hawa walioathirika, nani atawalipa? Pia kukipa chuo kibali cha kuendesha elimu ya chuo kikuu kuna hatua zinafuatwa na hata kukifungia kuna hatua zinafuatwa. Wanafunzi wale wamepelekwa Moshi pale, wengine wamepelekwa Morogoro, leo wanaambiwa wale ambao walikuwa wanapata mikopo hawatapewa tena mikopo kwa sababu wameongezewa semester moja. Ni kosa la wanafunzi hawa au kosa la Serikali? Kwa hiyo, naomba Serikali mliangalie vizuri sana jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Waziri hebu chunguza watu wako; hivi walikifunga chuo hiki kwa halali ama kulikuwa na mbinu nyingine? Kwa hiyo, nikuombe sana, kwa sababu tulioathirika ni sisi wazazi.
Wanafunzi wanahamishwa, wengine wamekuja UDOM hapa wanaambiwa kwa sababu kule sijui walichelewa, waongezewe semester moja, waliokuwa wanapewa mikopo hawatapewa tena mikopo. Nani sasa atakayelipia hiyo gharama wakati ninyi ndiyo mlifanya kosa? Angalieni kwa kina sana; namwomba Mheshimiwa Waziri alichunguze sana jambo hili. Pamoja na hatua nzuri aliyochukua hebu awachunguze vizuri watu wake wa TCU, walitenda haki kwenye kukifunga chuo hiki ama kulikuwa na mbinu za chini kwa chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba nizungumzie kidogo suala la shule ambazo zinapewa hadhi ya kwenda A Level, hasa katika shule hizi za Kata. Shule nyingi hizi zina miundombinu duni na nimshukuru Mheshimiwa Waziri, ameniahidi kwamba atanisaidia kupata fedha ya kuchimba kisima cha maji katika Shule ya Sekondari ya Farkwa na Shule ya Sekondari ya Msakwalo. Shule hizi zina miundombinu duni sana, wakati mwingine sisi Waheshimiwa Wabunge tumekuwa sasa ndiyo kama walezi wa shule hizi, kila jambo lazima sisi tusimame kidete, wakati mwingine magodoro hakuna, Wabunge wanatoa, hiki hakuna, Wabunge wanatoa. Niiombe Serikali iziangalie vizuri shule hizi, mnapopandisha hadhi ya shule mjiridhishe kwanza, kwamba, je, inakidhi! Hili ni jambo ambalo nadhani mkiliangalis vizuri linaweza kutusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nataka kuzungumzia huu mfumo wetu wa D by D, kwenye Kamati wamesema, lakini na mimi tena nichangie. Hebu uangalieni vizuri huu mfumo, nimesema kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, nimesema kwenye Wizara nyingine, angalieni, fanyeni kwanza review, unatusaidia kiasi gani! Leo Waziri wa Elimu naweza kusema mwisho wake hapa Dodoma ni Dodoma Sekondari na Msalato, akifika kule, Waziri anayeshughulika na shule zile Mheshimiwa Simbachawene. Waziri akifika huyu kule mgeni kabisa, halafu akienda kwenye Halmashauri Waziri wa Elimu anasimamia tu kile kitengo cha ukaguzi, lakini Maafisa wengine wote wapo chini ya TAMISEMI. Nadhani kuna tatizo hapa, hebu kaeni chini muangalie namna gani, sisi kazi yetu ni kushauri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, na mimi naomba leo niseme kidogo jamani. Uchaguzi uliopita umepita na mshindi kajulikana; mshindi CCM. Mpira hauwezi kwisha, tena unataka kuja kulalamika nje, uchaguzi umekwisha. Leo mtu anasimama hapa anasema oh, tuliibiwa kura, ninyi mlikuwa wapi wakati mnaibiwa! Acheni kutafuta sababu, tafuteni chanzo cha kwa nini mlishindwa. Ninyi mnajua kabisa kwamba timu ya mpira yenye wachezaji 11, mchezaji mmoja anapoumia anaingia wa timu ile ile, ninyi ilikuwaje mkachukua mchezaji wa upinzani mkamuweka! Mchezaji wa Simba kaumia, mmechukua wa Yanga mkaweka pale, amefungisha leo mnakuja kulalamika hapa! Kabisa tu, eeh, lazima tuseme tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunakaa kimya humu sio kwamba hatuna uwezo wa kusema, tuna uwezo wa kusema. Mchawi mwenyewe, unaanza kutafuta mchawi, mchawi utatoa wapi wakati mchawi ni wewe. Kwa hiyo, niwaombe tu, muwe mnatafakari kwanza! Wewe nyoosha mdomo, fanya nini, lakini that‟s the truth, utaongea sana, utapiga kelele sana, ukweli ndiyo huo na umekuingia vizuri. Eeh! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kelele wala hainisumbui. Nataka niwaambie, nataka niwashauri in future kama mnataka kuwa chama kizuri cha Upinzani, miaka minne ijayo na miaka 20 ijayo, anzeni kutafuta wachezaji wenu.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tusikilizane. Mheshimiwa Magereli, Mheshimiwa Matiko tusikilizane. Mheshimiwa Nkamia malizia! (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Ninyi tukaneni lakini ukweli ndiyo huo. Wenye akili wanajua, wapiga kelele wanajua na najua imewaingia vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwanza naunga mkono hoja…
MHE. JUMA S. NKAMIA: Nataka niwambie tu. Kuna baadhi yenu humu…
MHE. JUMA S. NKAMIA: Ahsante, namalizia. Nataka niwape mfano mmoja. Benard Tapie aliwahi kusema kwamba, kuna baadhi ya watu wakiamka asubuhi wakijiangalia kwenye vioo, wana sura mbaya wanatamani kutapika. Sasa ninyi mnaoshangilia humu, mna sura mbaya mnatamani kutapika.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.