Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja hii ya Wizara ya Maji. Kwanza kabisa, naiunga mkono kwa asilimia mia moja. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya kwa ajili ya kuhudumia Watanzania hasa miradi ya maji.
Mheshimiwa Spika, la kwanza ni tatizo la maji katika Mji wa Mpwapwa. Mji wa Mpwapwa maji tunayo lakini hayatoshi. Idadi ya watu inaongezeka sasa ni zaidi ya laki moja na bado vyanzo vya maji vinavyotumika ni vile vile vya zamani na usambazaji wa maji Mji wa Mpwapwa kuna maeneo mengi sana maji hayafiki. Kwa mfano, maeneo ya Ving’hawe, Namba 30, Mang’hangu, Ilolo, Kwamshangoo, Behelo pamoja na Majumba Sita na Mbuyuni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile maji ni shida sana hasa kwenye taasisi kwa mfano Shule ya Sekondari ya Mpwapwa na Chuo cha Ualimu Mpwapwa wanafunzi wanapata matatizo makubwa, wakati fulani wanabeba ndo kwenda kutafuta maji maeneo mengine. Mheshimiwa Waziri, maji yetu ni ya chumvi lakini sina maana kwamba ayabadilishe yawe baridi (soft water), hapana, lakini Wizara mwaka 2008 mimi nikiwa Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Serikali iliahidi kuchimba visima sita vya maji baridi maeneo ya Ilolo na Kwamshangoo, mpaka sasa hakuna kilichofanyika. Walishafanya survey na wakagundua kwamba kuna maji baridi eneo la Ilolo na Kwamshangoo. Sasa naomba kwa Mheshimiwa Waziri, Wizara yake ilitekeleze, visima sita vichimbwe ili kuongeza wingi wa maji katika Mji wa Mpwapwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni miradi ya maji katika Jimbo langu. Kuna miradi minne ambayo inaendelea mpaka sasa, Kijiji cha Bumila, Iyoma, Mzase na Mima. Sasa ni mwaka wa tatu miradi haikamiliki, wakandarasi wapo site, sasa kama hawawalipi hawa wakandarasi hii miradi itakamilikaje? Wananchi wa vijiji hivyo wanaendelea kupata shida ya maji, hiyo miradi itakamilika lini; wawalipe wakandarasi ili miradi hiyo ikamilike, namwomba sana sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri afike katika vijiji hivi na yeye mwenyewe awaeleze kwa nini miradi haikamiliki. Nimeeleza sasa nimechoka na siwezi kukosa kura katika vijiji hivyo kwa sababu miradi haikamiliki, afike yeye mwenyewe kuwaeleza wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tatu, katika bajeti ya mwaka 2018, Wizara ya Maji iliahidi kuchimba visima katika vijiji vifuatavyo:-
Kijiji cha Kisima, Kijiji cha Mgoma, Gulwe, Lupeta, Chitemo, Igoji I, Iwondo, Kazania, Kiegea na Ng’hambi lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika na tayari Mhandishi wa Maji wa Wilaya ya Mpwapwa alishatoa orodha kwamba mpango wa kuchimba visima upo na mpaka sasa hata kisima kimoja hakijachimbwa. Sasa nielezwe hizo hela ambazo zilitengwa zimekwenda wapi, naomba anieleze Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, maji ni uhai, maji ni uchumi na maji ni maendeleo. Kwa hiyo, naomba sana miradi inayopangwa na fedha ambazo zinapitishwa na Bunge ziende kwenye miradi husika. Jambo la kushangaza, Bunge kama Bunge tunapitisha fedha katika Bunge lako Tukufu lakini fedha hizo nyingi hazifiki kwenye maeneo husika. Kwa hiyo, inakuwa Bunge hapa tunafanya kazi ya bure na miradi mingi sana siyo maji tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tupo hapa miezi mitatu kupitisha bajeti ya Serikali kwa ajili ya miradi na matumizi mengine lakini fedha zinazotolewa hata asilimia 50 hazifiki, sasa hizo fedha zinakwenda wapi na kuna miradi mingi sana viporo, kwa mfano, miradi ya maji ni mingi sana haijakamilika.
Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara hii miradi inayopangwa itekelezwe. Maji ni siasa, ukishasema kwamba Serikali imeahidi kuchimba kisima cha maji katika kijiji na mradi haujatekelezwa, hii ni siasa na uchaguzi ni mwaka kesho tutapata shida sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nikushukuru, nirudie tena kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Maji lakini naomba sana miradi hii itekelezwe ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)