Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia kwenye hotuba hii muhimu sana ya jambo muhimu sana la maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuipongeza Wizara; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu na wataalam wote wa Wizara kwamba pamoja na kwamba bado changamoto ya maji ni kubwa, lakini kuna kazi kubwa ambayo inaonekana inafanyika kwa hiyo nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha uliopita kwa maana ya 2017/2018, Halmashauri yangu ya Nzega DC kupitia Mpango wa Water Sector Development Programme (WSDP) ilipata karibu one billion ya kutekeleza miradi ya maji. Kwa hiyo, pale halmashauri sisi tulifanya usanifu tuka-engage wakandarasi wa miradi mikubwa mitatu ya visima virefu, lakini tangu wakati huo tulikuwa hatujapata go ahead ya Wizara ya kuwaruhusu wakandarasi wale waanze sasa kufanya kazi. Tulifuatilia, niliwasiliana na Mheshimiwa Naibu Waziri na naipongeza Wizara kwamba sasa hivi, muda mfupi tu, kama mwezi mmoja uliopita, Wizara imetoa go-ahead ili wakandarasi wale sasa waanze kutekeleza ile miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilichotokea hapa ni kwamba wakandarasi wale tuliwa-engage mwaka wa fedha uliopita mwezi Juni, 2018 na karibu mwaka sasa umekaribia kuisha, kwa hiyo wakandarasi wale sasa hivi wanaomba review ya mikataba kwa sababu wanadai kwamba bei za vitu zitakuwa zimebadilika na vitu kama hivyo. Sasa rai yangu kwa Wizara ni kwamba kwa sababu Wizara wamechelewesha huo mchakato, kwamba badiliko lolote ambalo litatokea kwa maana ya bei basi Wizara iwe tayari kuli-accommodate ili fedha ziweze kutosha na miradi ile ifanyike. Kwa sababu ni kweli tuliwa-engage mwaka sasa umepita na huenda kweli baadhi ya bei zimebadilika.

Mheshimiwa Spika, angalizo lingine ni kwamba kwenye kitabu cha Wizara ya Maji mwaka huu halmashauri yangu imepangiwa shilingi milioni 620 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya maji. Kwa hiyo, hofu yangu ni kwamba isije ikawa hizi milioni 620 za mwaka huu zikatumika kulipia ujenzi wa miundombinu ya hii miradi ya mwaka wa fedha uliopita. Ninaomba Wizara wawe makini kwamba hizi milioni 620 zilizopangwa zilizo kwenye kitabu hiki zitumike kwa ajili ya miradi mipya, miundombinu mipya itakayojengwa na wala zisije zikatumika tena kwa miradi hii ya mwaka wa fedha uliopita kwa sababu hii ilikuwa na fedha zake na hizo fedha zake ndiyo zitumike.

Mheshimiwa Spika, kama ni kuchelewesha ni Wizara ilichelewesha na ninaamini kwa sababu fedha zilikuwa zinatoka Wizarani basi wanazo kule na zilezile ndiyo zitekeleze hii miradi ya nyuma na hizi milioni 620 zitekeleze miradi mipya ambayo tutaisanifu kwa ajili ya mwaka huu wa fedha unaoanza mwezi Julai unaokuja.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu mradi wa Ziwa Victoria; nimeona kwenye kitabu cha bajeti zimetengwa milioni 500 za ndani lakini na bilioni 23 za nje kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyafikisha Tabora Mjini na Igunga kupitia Nzega. Tulilalamika kwamba usanifu wa mwanzo wa mradi huu uliruka baadhi vijiji lakini naipongeza Wizara kwa sababu imelizingatia hili, vile vijiji vilivyorukwa vimeingizwa kwenye usanifu lakini tatizo ni kwamba baada ya kuingizwa vijiji hivi vingi vimepewa gati moja tu au magati mawili.

Mheshimiwa Spika, vile vijiji vya zamani vilivyokuwemo kwenye usanifu wa zamani unakuta kijiji kama kina vitongoji saba kimepewa magati saba, kama kijiji kina vitongoji nane kimepewa magati nane, lakini hivi vilivyorukwa ambavyo sasa vimeingizwa unakuta kijiji kimepewa gati moja, sasa unakuta kijiji kina vitongoji nane lakini kimepewa gati moja tu, maana yake ni kitongoji kimoja tu ndiyo kitapata maji. Kwa hiyo hofu yangu ni kwamba tukiacha hivi ilivyo badala ya kuona kwamba wananchi wamepelekewa maji kitakachotokea ni malalamiko makubwa kwa sababu vile vitongoji vingine vyote vitakuwa havijapata maji na tutakuwa hatujafikia lengo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ushauri au ombi langu hapa ni kwamba hivi vijiji ambavyo vilikuwa vimerukwa na sasa vimeingizwa na vyenyewe vipatiwe idadi ya magati kama vile vijiji vya mwanzo kulingana na vitongoji ambavyo viko kwenye vijiji husika. Vijiji ambavyo vilikuwa vimerukwa ni Ilagaja, Bulambuka, Isalalo, Mizibaziba, Mwamalulu, Mabisilo, Mihama, Ilela Mhina, Kiloleni na Kipugala. Vijiji hivi vipatiwe magati ya kutosha ili kwa kweli waweze kufurahia na wao maji ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, tulifanya ziara na katika ziara yetu tulifanya ukaguzi wa miradi ya maji, miradi mingi ilikuwa ni ya maji, hasa ya vijijini. Nashauri maeneo ya vijijini Wizara ije na mwongozo kwamba usanifu wa miradi ya maji ya vijijini basi usanifiwe kwa namna ambayo utaendeshwa kwa pampu zitakazotumia umeme wa jua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ya vijijini hizi pampu za dizeli zina gharama kubwa na unakuta watumia maji wa vijijini wameshindwa kabisa kuendesha miradi hii na hata kunufaika na hayo maji kwa sababu maji yamewafikia, wameyapata, lakini gharama zinakuwa kubwa na kuna vijiji vingine mradi hautumiki kabisa kwa sababu wananchi wameshindwa. Mimi kwangu kule nina Miradi wa Mahene, Nawa, Buhondo, Sojo, Ikindwa, ni miradi mikubwa, mirefu, inafanya kazi lakini hata bei ya shilingi 100, 200 kwa ndoo wananchi kule vijijini bado wanasuasua kuweza kuimudu. Kwa hiyo napendekeza kwamba usanifu wa miradi ya maji ya vijijini usanifiwe kwa namna ambavyo itaendeshwa kwa pampu za umeme wa jua badala ya dizeli, dizeli bado ni gharama na wananchi wanashindwa kuimudu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine ni kwamba maeneo mengi ya vijijini tu-focus kwenye visima vifupi badala ya virefu kwa sababu kisima kirefu kimoja ambacho kinagharimu milioni 300, 400 unaweza ukapata visima zaidi ya kumi, 15 vifupi. Kwa hiyo katika maeneo mengi ya vijijini, kwa mfano kule kwangu nime-experience, ukijenga kisima kirefu unanufaisha kijiji kimoja unatumia milioni 400, milioni 400 hizo hizo ukisanifu visima vifupi vya pampu ya mkono unapata visima kumi mpaka 15 na eneo ambalo unahudumia linakuwa pana kwa maana ya vitongoji na vijiji vingi.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile gharama ya kuendesha pampu ya mkono kwa wananchi wetu wa vijijini ni nafuu haihitaji fedha kulikoni kisima kirefu ambacho kinahitaji fedha za dizeli na kuendesha. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba visima vya vijijini visanifiwe kwa…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)