Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya maji. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya na kuweza kusimama mchana huu wa leo. Kipekee kabisa niungane na wewe katika kuwapa pole Watanzania na wanafamilia wote kwa kuondokewa na mzee wetu, Mzee Mengi na Mungu amlaze mahali pema Peponi, amen.

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri Naibu Waziri, na jopo lote la maji kwa kazi ambayo wamekuwa wakiifanya katika kuwasaidia wananchi suala la maji. Ni ukweli usiopingika kwamba changamoto ya maji bado ni kubwa katika maeneo mengi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nizungumzie suala la Kigoma, kwa sababu tunasema charity begins at home. Sasa nami nianze kuwapigania wananchi wa Kigoma ingawa changamoto ya maji ni Tanzania nzima.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ambayo natokea ya Kigoma DC, tuna miradi miwili ya maji; tuna Mkongolo I, tuna Mkongolo II. Miradi hii imeachwa, imetelekezwa, miundombinu ni mibovu. Pia miradi hii inahudumia zaidi ya watu 50,000 Vijiji vya Mwandiga, Bitale, Mkongolo, Nkungwe, Kiganza na maeneo mengine ya Kigoma DC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kigoma tunateseka, hatuna maji. Leo nimefikisha miaka 30, lakini mama zangu wanabeba maji kuanzia sijazaliwa mpaka sasa. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri wasaidieni wamama wa Kigoma. Kama kweli tunasema ni Serikali ya wanyonge, kama kweli tunataka kumtua mama ndoo kichwani, tuwasaidie akina mama ambao nywele zimeisha katikati kwa sababu ya kubeba ya ndoo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Kijiji cha Mwandiga. Hapo Mwandiga kuna Mzee mmoja anaitwa Mzee Sheni, ni Mhindi. Huyu amechimba kisima, anawasaidia watu hawa wa hapo, ndoo shilingi 100/=. Sasa leo tunaposema kwamba mtu kama huyu atoe tozo kwa sababu ya kuchimba kisima, sidhani kama tunamtendea haki. Kwanza amewasaidia wananchi, ambao kwa miaka zaidi ya 30 tunatumia maji ambayo siyo safi na salama. Mwandiga tumekuwa ni kinara wa ugongwa wa kipindupindu kwa sababu hatuna maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naungana na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba tozo hii kwa sababu ya kuchimba visima, iweze kuondolewa. Kaka yangu, Mheshimiwa Nape alielezea vizuri kwamba hawa ambao wanauza maji labda haya ya kunywa ambayo wanafunga kwenye makatoni, sawa; lakini hawa ambao wanachimba visima kwa sababu ya kuwasaidia wananchi, kama tutawatoza tozo, kiukweli hatuwatendei haki. Kwanza wanawasaidia wananchi.

Mheshimiwa Spika, yuko mwingine amechimba nyumbani kwake kwa sababu ya matumizi yake binafsi. Haiingii akilini tunapomwambia atoe shilingi 700,000/=, atoe kiasi cha fedha kwa sababu ya kuchimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongezee suala lingine katika Mkoa wa Kigoma. Nashukuru katika Kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kuna mradi wa Ziwa Tanganyika Naomba sana huu mradi utekelezwe na ukamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kuna maji ambayo yako katika Manispaa ya Kigoma Mjini kwa kaka yangu Mheshimiwa Zitto, lakini haya maji yanakuja yanaishia katika mpaka wa Mwandiga na Kigoma Mjini ambako panaitwa Ntovye. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, haya maji ambayo yanaishia pale yasiweze kupotea yapande katika Kijiji cha Mwandiga, yapande katika Kijiji cha Bitale na Kijiji cha Kiganza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mwaka 2018 nakumbuka niliuliza swali kwamba Serikali ina mkakati gani wa kuleta maji ya Kigoma Mjini yapande mpaka Vijiji vya Mwandiga na kuendelea? Kaka yangu Mheshimiwa Aweso alinijibu akaniambia kwamba wapo kwenye mkakati. Nafahamu juhudi ambazo zinafanywa, sasa nawaomba sana wasichelewe, tusaidieni wamama wa Mwandiga na maeneo mengine tuweze kuondokana na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Nizungumzie suala lingine. Ndani ya Halmashauri ya Kigoma DC kuna vijiji ambavyo mpaka sasa kwenye miradi tunatumia dizeli na mafuta, kitu ambacho tunasababisha hasara kwa Serikali yetu kutokana na gharama ambayo tunaitumia. Sasa katika Vijiji kwa mfano, mradi katika Kijiji Nkungwe, Kalinzi kule kwetu na Kandanga tunatumia dizeli na umeme, ni gharama kubwa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kama tungepata solar naamini ingeweza kutusaidia na wakafanya kazi kwa ufanisi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisisitize, mbali na kwamba nimeongelea Kigoma, lakini bado kuna maeneo mengine hata Dar es Salaam, suala la maji ni changamoto, kwa mfano, Goba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakazi wa Goba, wamekuwa wakiteseka, hakuna maji ya uhakika na ninatambua kuna mradi pale unaendelea. Sasa huu mradi ambao umekuja umeishia Kinzudi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri huu mradi uweze kusambaa katika eneo lote la Goba, wakazi wa Goba waweze kupata maji safi na salama, lakini tuondokane na kero ambayo wakazi wa Goba wamekuwa wakiipata kwa kukosa maji kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine nizungumzie changamoto ya watumishi; Kigoma suala la maji katika Idara ya Maji bado tuna changamoto ya watumishi. Niombe sanawatusaidie watumishi waongeze nguvu katika halmashauri zetu tupate Wahandisi wakutosha. Kipekee kabisa Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni na kama mtu anafanyakazi apongezwe, nampongeza Mheshimiwa Waziri, baba yangu Mbarawa anafanyakazi. Sasa naomba Mhandisi Mkoa wa Kigoma nikijana kama mimi, anafanyakazi kwa kujituma, naomba tumuunge mkono mpaka sasa bado anakaimu, lakini amekuwa ni kinara katika kushirikiana na wananchi wa Kigoma kutatua kero mbalimbali za maji. Sasa kama anatusaidia wananchi wa Kigoma na anafanya kazi vizuri, basi Mheshimiwa Spika kipekee kabisa naomba huyu kijana aweze kupewa haki yake na asibaki kukaimu kwa muda mrefu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kuongea nafikiri nitakuwa narudia ambayo wenzangu wameshaongea, naomba sana Mheshimiwa Waziri haya ambayo nimemwomba Mji wa Mwandiga tupate maji, lakini vijiji vingine ambavyo havijawahi kuona maji kabisa kwa mfano Kiziba, Kalalangabo naMatyazo hawajawahi kuona maji kwenye mabomba wala maji safi na salama. Naomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kuwasaidia watu hao wapate maji na waone faida ya kuwa na Ziwa Tanganyika katika mkoa wao.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niseme nakushukuru.(Makofi)