Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsantekwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Maji ni uhai na nitaanzia kwanza na bajeti ambayo tuliidhinisha kwaajili ya kuwapatia wananchi maji mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019, tulipitisha bajeti ya shilingi bilioni 672 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata maji, lakini mpaka sasa fedha ambayo imekwenda kufanyakazi kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji, imetolewa shilingi bilioni 343.4.
Mheshimiwa Spika, tunajiuliza sana kama Wabunge kwa kazi ambayo tunaifanya ndani ya Bunge ya kupanga/ kutengeneza bajeti lakini pia kuhakikisha kwamba tunaidhinisha bajeti hii ili wananchi wetu waweze kupata maji, lakini cha kushangaza fedha haziendi kabisa kwenda kutekeleza shughuli za maji. Nataka nitoe mfano tu katika bajeti hii ya bilioni 672, kuna fedha karibuni shilingi bilioni 185, hizi fedha zilikuwa zinatokana na fedha za mchango wa wananchi kwenye mafuta ya petroli na dizeli, lakini pia kulikuwa na fedha karibuni shilingi bilioni 229.9, hii ni fedha ambayo ilikuwa inatoka kwa Washirika wa Maendeleo ambayo tulikuwa tunategemea zitaingia ili kuhakikisha kwamba zinatusaidia. Pia kulikuwa na ruzuku ya Serikali karibu shilingi bilioni 285 ambayo ilitakiwa pia kuchangia ili kutimiza hiyo fedha bilioni 672 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi fedha iliyotoka ni kama nilivyosema ni bilioni 343 tu ndiyo iliyotoka. Sasa ni nusu ya bajeti yote ambayo tulikuwa tumeipitisha kwenye mwaka 2018/2019. Fedha hii ambayo tunaitenga kila wakati na tunaipitisha inakuwa ni ndogo na kila siku Wabunge tukiwepo humu tunalalamika kwamba fedha ni ndogo sana, iongezwe lakini cha kushangaza hata hii fedha ndogo ambayo inakuwa imeshapitishwa ndani ya Bunge, inashindwa kutolewa na Serikali ili kwenda kutekeleza miradi ya wananchi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi chote hicho fedha ya mchango wa wananchi kwenye mafuta ya dizeli na petroli ambayo ilikuwa imetengwa shilingi bilioni 185, imetoka shilingi bilioni 155 imekwenda kutekeleza miradi ya maji. Pia fedha ya wafadhili, kati ya bilioni 229.9, fedha iliyotoka ni shilingi bilioni 188, ukizijumlisha fedha hizi inakupa hesabu ya shilingi bilioni 343.4. Tafsiri yake ni kwamba Serikali upande wa Hazina kama ruzuku ya Serikali bilioni 285 haijaonekana katika hesabu inayoonekana sasa hivi hapa.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa napitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri hapa kwenye ukurasa wa 104 na 105, Mheshimiwa Waziri amejaribu kuongea kuhusiana na changamoto mbalimbali ambazo zimejitokeza na ni kwanini wameshindwa kutekeleza miradi mbalimbali ambayo ilikuwa imepangwa. Tatizo kubwa wanalolizungumzia kama Wizara wanalalamika kwamba fedha hazitoki kwa muda na fedha haziendi ili kutekeleza miradi na hii imesababisha kukwamisha miradi mingi isiweze kutekeleza. Sasa kama Wizara Serikali imeanza kulalamika kiasi hiki, ni wajibu Wabunge sasa kuchukua hatua kujaribu kuiambia Serikali itoe fedha ili Wizara ikaweze kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo lazima tusimame tuangalie Waziri wa Fedha pamoja na Hazina waangalie ni namna gani wanaweza kuwa wanatoa fedha ambazo tunakuwa tunazipitisha ndani ya Bunge hili ili ziende kufanya kazi na Watanzania waweze kupata maji. Hatuwezi kuwa kila siku tunatengafedha halafu baadaye hizo fedha haziendi kufanyakazi. Hili ni jambo ambalo linatushangaza sana na ni wajibu wetu kama Wabunge, ni wajibu wako kama kiongozi wa Bunge kuhakikisha kwamba unalisimamia hili jambo na fedha zinatoka, maana yake nakumbuka mwaka uliopita ulijaribu kumweleza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba kwanini hupeleki fedha katika miradi ya maendeleo kama ambavyo tumepitisha.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi ningeomba Bunge lako hili lihakikishe kwamba Serikali wakati wote tunapokuwa tumetenga bajeti yetu,ni lazima bajeti hii ikatekeleze miradi kama tulivyokuwa tumepanga. Sasa miradi iliyotekelezwa mwaka 2018/2019 ni nusu ya fedha ambazo tulikuwa tumeshazitenga. Tafsiri yake ni kwamba mwaka 2019/2020 tunakwenda kutekeleza viporo ambavyo tulitakiwa kutekeleza katika mwaka uliopita. Kwahiyo, naomba sana jambo hili lazima tulifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika,nilimsikiliza Mheshimiwa Musukuma pale amesema kwamba hataki Sh.50 iweze kuongezwa. Watu wengi wanaweza kuona hii ni hoja dhaifu, lakini si hoja dhaifu, ni hoja nzuri na inaendeleza kutukumbusha kwamba tunavyozidi kuongeza tozo kwenye mafuta kwa ajili ya maji tafsiri yake ni kwamba tunawaongezea wananchi mizigo, tunaendelea kuongezea gharama wananchi badala ya kuwapunguzia gharama wananchi. Hawa Watanzania ambao tunawazungumza leo kuwaongezea kila siku mafuta hawa wananchi wanalipa kodi, hawa wananchi kila siku tunaosema kwamba tuwaongezee ni wananchi ambao tayari wanalipa kodi katika Taifa hili.
Mheshimiwa Spika,kwahiyo lazima tuangalie tunachokizungumza tunamaanisha namna gani, je, kodi wanazozitoa wananchi na ambazo tunatenga kwenye bajeti hii kwanini Serikali inashindwa kutoa fedha hizi na kwenda kufanyakazi. Nimeshasema kuna fedha bilioni 285 zilitengwa mwaka jana ambazo Hazina walitakiwa wazitoe mpaka sasa hivi tukisema kwenye mahesabu ambayo tumeyapiga hapa kufikia bilioni 343 hutaiona fedha iliyotoka Hazina. Sasa tunataka fedha za wananchi ziweze kutumika kama ambavyo tunapitisha bajeti katika Bunge hili.
Mheshimiwa Spika,madhara ya kutokuwa na maji safi na salama kwa wananchi ni makubwa sana katika Taifa kwasababu wananchi wengi sasa wanaumwa matumbo na matumbo haya yanasababishwa sana na kupata maji ambayo ni machafu. Sasa Serikali inaingia gharama kubwa sana ya kununua madawa na tumekuwa tunajinasibu ndani ya Bunge hili kwamba Serikali inatenga fedha nyingi kwaajili ya kununua madawa. Kununua madawa kwa fedha nyingi sio sifa ni kwamba Watanzania wengi ni wagonjwa, Watanzania wengi wanaumwa na ndio maana tunatenga fedha hizi, lakini fedha hizi tunasababisha kuzitumia vibaya kwenye madawa kwasababu hatutaki kutengeneza mazingira mazuri ya kupata maji safi na salama. Ni lazima tujikite kuhakikisha kwamba tunawapatia wananchi wetu maji safi na salama na bajeti zingine hizi zitakwenda kufanya kazi zingine ambazo zinahitajika zaidi, lakini hiki tunakihitaji wenyewe.
Mheshimiwa Spika, pia kuna kiasi cha maji kwa mtu kwa mwaka, ukiangalia katika takwimu mwaka 1961 kiasi cha matumizi ya maji kwa mtu mmoja mmoja kwa mwaka ilikuwa ni ujazo wa mita za ujazo 7,862, lakini mpaka mwaka 2018, sasa hivi zimeshuka mpaka 2,300. Hii inatoa picha gani? Ni kwamba Serikali haijaweka uwekezaji mzuri ili kuweka uwiano mkubwa kulingana na ongezeko la Watanzania katika Taifa hili. Ni lazima tuone na ndiyo maana mjumbe mmoja jana amesema tunakoelekea Tanzania sasa hivi tuko kwenye mstari ambao uko kwenye hatari ya kukosa maji kabisa kwasababu wananchi wanazidi kuongezeka, lakini uwekezaji unazidi kushuka. Angalia katika bajeti ya mwaka huu, bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Waziri anahitaji bilioni 610 ili kutekeleza miradi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA:…lakini kila mwaka bajeti inazidi kushuka. Ahsante sana. (Makofi)