Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kushiriki kwenye mjadala huu.
Mheshimiwa Spika, la kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia zote. Mchango wangu utakuwa na sehemu mbili, kwanza ni shukrani na pongezi kwa yale ambayo yamefanyika Jimboni Sengerema, lakini la pili nitakuwa na ushauri kwa yale mambo ambayo naona ni kazi zinazoendelea kwa sababu hazijakamilika.
Mheshimiwa Spika, katika pongezi, naomba niungane na wenzangu kusema kwamba Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa pamoja na wenzake Mheshimiwa Naibu Waziri Jumaa Aweso, Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu, Eng. Kalobelo pamoja na Wakurugenzi na wataalamu wenginge wanaopambana kadri inavyowezekana, wanajitahidi sana.Tumeona na inawezekana kukawa na udhaifu katika baadhi ya maeneo lakini dhamira yao naiona kabisa.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mmoja wa mashahidi kwa namna ambavyo wanajitahidi kutatua kero katika nchi yetu. Mheshimiwa Waziri ameshafika Jimboni Sengerema, Mheshimiwa Naibu Waziri anaendelea kutembelea maeneo mbalimbali nchini, pia Katibu Mkuu mwenyewe alishafika Sengerema, Naibu Katibu Mkuu ameshafika na Wakurugenzi wanaendelea kufanya ziara mbalimbali kutatua kero za maji. Kwa hiyo nachosema ni kwamba wanapambana na sisi Mkoa wa Mwanza Mamlaka ya Maji MWAUWASA inaendelea kufanya kazi nzuri, ingawaje ziko changamoto.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Sengerema wamenituma niipongeze Serikali kwa haya yafuatayo. Tumekuwa na kilio cha muda mrefu cha upatikanaji fedha lakini hivi karibuni Sengerema tumepata shilingi milioni 502 kwenye mradi wa maji unaohusu Kijiji cha Buyagu, Kalangalala hadi Bitoto. Pia tumepata shilingi milioni 58 kuhusu uchimbaji wa visima katika Vijiji vya Ilekanilo, Kasomeko na Igulumuki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukisoma ukurasa wa 121 kwenye kitabu cha hotuba cha Mheshimiwa Waziri, unaona katika mgao wa fedha za miradi ya maji vijijini. Sisi Halmashauri ya Sengerema tumetengewa shilingi milioni 886, asiyeshukuru kwa kidogo hawezi kushukuru hata kwa kikubwa. Tunasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye ukurasa wa 63, ambao unahusu miradi ya maji katika vijiji vilivyomo pembezoni mwa Maziwa Makuu, ukisogea kidogo chini ukurasa wa 64(iii), kuna mradi mkubwa umebuniwa na Serikali, unahusu kutoa maji Ziwa Victoria na kuwafikia walengwa katika Vijiji 301. Hapa nazungumzia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita, Mara pamoja na Mkoa wa Simiyu. Sisi kwenye Halmashauri ya Sengerema tuna zaidi ya vijiji 26, tunasema ahsanteni sana kwa kuiweka Sengerema katika ramani ya huo mradi mkubwa na tunaamini fedha zikipatikana za kutosha mradi huu utatekelezwa. Serikali imetoa commitment hapa, kwamba baada tu ya kukamilisha zoezi ambalo linaendelea sasa hivi la usanifu, ujenzi wa mradi huo, utaanza, ni jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo kuna kazi zinazoendelea, naikumbusha Serikali, nimekuwa na mawasiliano mazuri, nashukuru tumepata hizi fedha ambazo nimesema zaidi ya shilingi milioni 500 lakini kuna fedha zingine tunazisubiria kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi ya kufikisha maji kwenye kijiji cha Ibondo kwa Mwarabu, Mwabalugi kule na hasa eneo la Zanzibar, kule Sengerema pia kuna Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, pia tuna miradi ambayo tunasubiri fedha kama mradi unaohusu Vijiji vya Mwaliga, Kang’washi na Sima, pale kuna ujenzi wa kisima pamoja na kisima cha Kijiji cha Nyamahona. Haya ni maeneo ambayo tunasubiri tu fedha, Serikali ilitoa fedha hivi karibuni round ya kwanza, lakini itatoa tena fedha nadhani labda kufikia mwishoni mwa mwezi huu ili tukaikalimishe miradi hii. Tunasema ahsanteni sana Serikali kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna kazi zinazoendelea na hapa naikumbusha Serikali kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Nyasigru, Bungo na Ngoma. Mradi huu unahusu kutoa maji Ziwa Victoria umebuniwa zaidi ya miaka miwili iliyopita na utaratibu wa kumpata mkandarasi, atakayeshughulikia mradi huu ulikamilika Mei, 2018, leo ni mwaka mzima.
Mheshimiwa Spika, naelewa sana baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaposema ziko changamoto katika Wizara hii. Imagine tumempata mkandarasi kwa utaratibu wa kawaida wa Serikali Mei, 2018 na hapa katikati mimi sijalala, nimekuwa nina mawasiliano na Serikali mazuri tu lakini mpaka leo mkandarasi hajaingia site. Bado kuna reservation, technically wanasema kuna hili na lile lakini kwa nini ichukue mwaka mzima? Haya ndiyo mambo ambayo tunasema yanahitaji kuongezewa kasi ya utatuzi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nikumbushe MWAUWASA wako hapa wanasikiliza, pale kwenye mradi mkubwa Mjini Sengerema pale na vijiji vingine ambavyo vinapitiwa na mradi ule kuna eneo la Kizugwangoma, Misheni pamoja na Bujora kuna ahadi ya kujenga booster ili kufikisha maji maeneo hayo. MWAUWASA waliahidi kwamba ujenzi ungekuwa umeshaanza toka Aprili, 2019, mpaka ninavyozungumza bado na mimi nafuatilia kila siku. Kwa hivyo, unaweza kuona hizi changamoto zilizopo, tunaamini kwamba fedha zipo lakini katika kasi ya utekelezaji kuna mahali hatuendi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, tuna Mradi wa Nyampanda ambao tayari taratibu zote za kumpata mkandarasi zimeshakamilika, tarehe 25 Aprili, ilikuwa tushuhudie kusainiwa kwa mkataba kwa mkandarasi aliyepatikana. Hivi karibuni Serikali iliahirisha tusisaini tarehe 25 Aprili hadi tarehe nyingine itakapopangwa.
Mheshimiwa Spika, najua nina wito wa kukutana na Watendaji wa Wizara hii baada ya hapa tukayajadili haya tupeane update lakini nawaomba wajiandae kunipa majibu kwamba ni nini mkandarasi wa Nyasigru, Bungo, Ngoma yeye hajapatikana? Ujenzi wa hii booster niliyosema ili kuyafikisha maji kwenye maeneo ya Misheni, Kizugwangoma, Bujora lakini lini mtasaini mkataba wa kuyafikisha maji katika Kijiji cha Nyampande? Pia tuna Kijiji cha Sima ambako kinaingia kwenye programu ya kuanzia mwezi Julai lakini kuyafikisha maji katika Kijiji cha Tunyeng’e.
Mheshimiwa Spika, kwenye sehemu ya ushauri nina jambo la kusema ukisoma ukurasa wa kumi wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu alivyokuwa anaelezea hali halisi ya upatikanji wa maji katika nchi yetu na nijielekeze hata katika maeneo ya vijijini. Kwenye ukurasa huu wa kumi wa hotuba hii anasema kufikia mwezi wa nne mwaka huu upatikanaji wa maji katika vijiji ulikuwa ni asilimia 64.8 lakini lengo ni kufikia asilimia 85 ili tufikie lengo lile kuu la kuhakikisha kwamba wannachi hasa vijijini wanapata maji ndani ya mita 400.
Mheshimiwa Spika, wakati huo huo ukisoma ukurasa wa 106 hadi 108 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri anakubali kwamba kinachotukwamisha kufikia malengo yetu ni changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati na fedha za kutosha. Pia hotuba ya kamati inayoshughulikia wizara hii Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ukurasa wa tano wamezungumzia changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, katika hili nimeshindwa kuelewa sitaki kuwa vuguvugu ama baridi ninashindwa kuelewa tunakwama wapi kwa sababu hapa tumezungumza na katika hili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema ninasimama na wote wale wanaounga mkono tuongeze shilingi 50 katika ule mfuko ili tuongeze kasi ya kuwafikishia maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninafahamu wasiwasi uliopo lakini nataka ni-share uzoevu kidogo nilionao. Baada ya mdororo wa uchumi kuikumba dunia mwaka 2007 hadi mwaka 2009 mwaka mmoja au miwili baadaye sisi kama Taifa tulikumbwa na tatizo kubwa sana la uchakachuaji katika mafuta hasa bidhaa ya petrol kwa maana ya diesel na petroli. Na tatizo lililokuwa limesababisha kutufikisha hapo ni kwa sababu katika bidhaa zile tatu, mafuta ya taa, diesel na petrol kwenye ushuru sisi tulikuwa tumetoa exemption kwenye mafuta ya taa, kwa hivyo uchakachuaji ukawa ni mkubwa sanan zaidi ya asilimia 87. Lakini tukajadiliana sana na jambo likawa gumu
Mheshimiwa Spika, wakati huo nikiwa Waziri wa Nishati na Madini na-share huu uzoevu tulinganishe hofu iliyokuwepo. Tulikwenda mara ya kwanza tukapa ushauri na Mheshimiwa Shabiby sijui yuko wapi alikuwa hapa alishauri kwamba ondoeni tufanye harmonization ya ushuru katika bidhaa zote hizi petrol, diesel na mafuta ya taa. Tulivyorekebisha tulivyounganisha ule ushuru hapakuwepo na uchakachuaji na tukasonga mbele na hofu kubwa ilikuwa kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watanzania kwa maana ya Nishati ya Mwanga wanatumia mafuta ya taa lakini…
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ngeleja.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, hapakuwa na shida hiyo ndio maana nasema, nashukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja lakini Serikali tu itafakari tu ushauri wa Wabunge naamini kwamba tutaelewana tutafika mahali pazuri na sio lazima tuongeze mafuta tunaweza kuongeza kwenye maeneo mengine pia kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge, asante sana. (Makofi)