Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chilonwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja hii ya bajeti ya Wizara ya maji, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anazoendelea kuzifanya ambazo zinatudhihirishia na zinatupa matumaini makubwa sana kwamba mpango wetu wa kuiingiza nchi katika uchumi wa kati mwaka 2025 tutaufikia bila wasiwasi wowote kwa kuchapa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kazi zao kubwa wanazozifanya pamoja na timu yao nzima Wizarani pale. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa namna alivyowasilisha taarifa yake hapa jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Maji ni kila kitu, maji ni uhai kwa binadamu, kwa wanyama na kwa mimea, maji ni uhai kwa kila kitu chenye uhai hapa duniani. Maji safi na salama ni afya. Maji safi na salama ni afya kwa binadamu. Kwa mpango wetu tulinao wa kuivusha nchi yetu kuipeleka kwenye uchumi wa kati tunahitaji watu wenye afya njema. Bila maji safi na salama itakuwa ngumu kufika huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nichukue nafasi hii niipongeze mipango mizuri sana ya Wizara ambayo imesomwa na Mheshimiwa Waziri jana ambayo iko kwenye kitabu hiki imejieleza kwa uzuri sana. Tumeona kuna mipango inazungumzia ujenzi wa mabwawa ya mikakati. Mabwawa ya mikakati yametajwa hapa, moja kati ya mabwawa hayo liko bwawa la Farkwa lililoko Chemba hapa Dodoma. Bwawa hili linakusudiwa pamoja na mambo mengine liweze kuwa chanzo kikubwa cha matumizi ya maji hapa Jijini Dodoma na viunga vyake vyote, Wilaya ya Bahi, Chamwino na Wilaya ya Chemba yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia jinsi watu wanavyo-flow Dodoma sasa hivi, ukizingatia sasa ofisi zote za Wizara zote, Serikali nzima sasa iko Dodoma, sasa wako Mtumba, hata wale wachache waliokuwa wanazembea zembea, wanategea tegea kuja Dodoma sasa hawana namna inabidi waje. Mji huu utafurika watu sana muda sio mrefu. Maji yako wapi? Maji ya Mzakwe, sawa! Hadi wakati huu bado yanajitosheleza, lakini kwa flock ya watu itakayokuja muda sio mrefu tutaanza kulia tatizo la maji. Kwa hiyo niombe sana Wizara waangalie sana suala zima la kukamilisha miradi mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ukarabati wa mabwawa ya zamani. Yako mabwawa ya zamani na yametajwa kwenye kitabu hiki ukurasa wa 56, kati ya mabwawa hayo, yako mabwawa ya Dodoma, liko bwawa la Ikowa ambalo liko Wilaya ya Chamwino na liko bwawa la Buigiri ambalo pia liko Wilaya ya Chamwino. Mabwawa haya awali kama ilivyo leo kwenye kitabu yalijengwa kwa maana ya kudhibiti mafuriko lakini tulivyoendelea hivi kuja kilimo chetu kimekuwa shida mabwawa haya yamekuwa yakitumika sasa kama ni chanzo kikubwa sana cha kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa hayo sasa yameingia shida. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Wizara nzima kwa ujumla lakini Waziri aliyepita Engineer Kamwelwe alipata nafasi akatembelea mabwawa ya Buigiri na mabwawa ya Ikowa akayatolea kauli kwamba mabwawa haya yatashughulikiwa ili watu waendelee kufaidi na kunufaika na mabwawa yale kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, mpaka sasa kimya! Tatizo tunaweza kuwa tunalijua, ndiyo hapo tunaposema, tusione shida wakati mwingine, ni kweli kunaweza kuwa na ufisadi wa watu kuhujumu fedha za umma kwenye miradi ya maji, lakini sio kila sehemu na ukiangalia sehemu kubwa sana ni ukosefu wa fedha kufika kwenye maeneo husika. Fedha za maendeleo hazifiki jinsi zinavyopangwa, shurti zingefika hata hizo kidogo, basi tusingekuwa hapa tulipo leo. Suala hili tunaomba Wizara ihakikishe inakamilisha miradi yake mapema inavyowezekana ili watu waweze kufaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti na uchimbaji wa visima mbalimbali ni jambo zuri sana. Hii ni mikakati mizuri ambayo tunasema Wizara yetu imekuja nayo na tunaomba mikakati hii basi itekelezeke kweli kweli. Katika mikakati hii, katika utafiti na uchimbaji wa visima hivi bahati nzuri na wilayani kwangu, Wilaya ya Chamwino, tumepata visima 14. Katika visima 14, visima nane viko kwenye Jimbo langu la Chilonwa. Pamoja na visima hivi nane vilivyochimbwa juzi, leo hivi nazungumza nina visima 20 katika Jimbo la Chilonwa peke yake ambavyo vimechimbwa, sawa, maji yamepelekwa maabara yameonekana yako safi na salama kwa matumizi ya binadamu lakini maji bado yapo chini, hakuna pump, hakuna chochote, tunamaliza miaka miwili. Sasa watu wanafika mahali fulani, kama sisi wa CCM tunasema utekelezaji wa Ilani, Ilani ya CCM ndiyo inavyotuambia sasa wameNtuchimbia maji wanasema maji yako chini, yako wapi? Tunayataka maji tuyatumie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii niombe sana suala zima la kuiomba Wizara ihakikishe kwamba miradi yote iliyowekwa hapa itimie, ikamilike ili wananchi waweze kufaidi matunda ya kazi ambazo zinafanywa sasa. Nichukue nafasi hii mimi niunge mkono wale ambao wana hoja ya kusema maamuzi yetu tuliyoyafanya vikao vya nyuma kwamba tupate Sh.50 toka kwenye mafuta ili iweze kusaidia Mfuko wa Maji wa Taifa naliunga mkono kwa kweli, kwa sababu naamini hilo linaweza kusaidia upatikanaji wa fedha ili kuweza kutatua matatizo haya ya miradi isiyokamilika kwenye maeneo yetu mbalim bali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya machache, kwa nafasi hii tena niseme naiunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini naomba sana ukamilishaji wa miradi hii ufanyike mapema. Ahsante.