Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwakupata hii fursa uya kuchangia Wizara muhimu sana, Wizara ya Maji, maana bila maji hakuna uhai. Nianze kwa kumpongeza Profesa, Mheshimiwa Waziri maana yake juzi nililia kidogo kuhusiana na mradi wangu wa Nguruka Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wamenisaidia lita 2,000 za mafuta. Nawashukuru sanaMheshimiwa Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa namna ambavyo walivyoweza kuwasaidia akinamama wa Tarafa yangu ya Nguruka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie suala la miradi yangu ya maji iliyoko jimboni. Naomba nizungumzie Mradi huo wa Nguruka, namwomba Mheshimiwa Waziri, natambua kwamba ule mradi ni wamuda mrefu na kiasi fulani umekamilika, lakini bado ile extension ya kutoka pale Nguruka kwenda Kijiji cha Bweru na Kijiji cha Mlyabibi haijaanza kutekelezwa. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri,kwa sababu waliahidi wenyewe kama Wizara kwamba mradi ule chanzo chake cha maji kinatosha kupeleka maji yale mpaka Mlyabibi lakini sio tu Mlyabibi na Kijiji cha Bweru. Sambamba na hilo nimwombe tu Mheshimiwa Waziri ajaribu kumwomba Mkandarasi aweze kumaliza basi hayo maeneo mawili kwa maana ya Bweru, pamoja na Mlyabibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili naomba nizungumzie Mradi wangu wa Kandaga. Ninao Mradi waKandagaambao utekelezaji wake ulikuwa ni bajeti 2013/ 2014, lakini hadi leo hii Mheshimiwa Waziri ni shahidi tulifanya naye ziara, tulienda pale, maji yanatoka kiasi, lakini wananchi bado hawajapata maji. DP zimewekwa, tanki lipo, maji yanatoka, lakini wananchi hawajapata maji, kwa hiyo wananchi wa Kijiji cha Kandaga wamenituma, wanasema wanaomba sana kama mama niko hapa, waliniamini na wanataka waniamini tena hapo baadaye, kwa hiyo naomba Mradi ule wa Kandaga uweze kutoa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu naomba nizungumzie Mradi wangu waKijiji cha Rukoma. Tunao mradi mkubwa katika Kijiji cha Rukoma lakini kwa bahati mbaya mradi ule una chanzo kikubwa cha maji, chanzo chake ni Mto Luegele, mto huu una maji mengi sana kiasi kwamba hata wenzetu wa Wizara ya Nishati wanatarajia kufua umeme kupitia chanzo hiki. Sasa ombi la kwanza naomba aidha niMheshimiwa Waziri au ni Mheshimiwa Naibu Waziri watafute siku tuambatane waende wakashuhudie ule Mradi wa Rukoma lakini wakashuhudie hicho chanzo cha maji. Chanzo kipo, tatizo ni utekelezaji wa ule mradi umesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba nizungumzie Mradi wa Ilagala, tunao Mradi mkubwa wa Ilagala lakini mradi ule unaonekana kwamba ulitekelezwa chini ya viwango. Kwa hiyo Ilagala sio mbali Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenda Rukoma nitaomba pia tuambatane twende Ilagalailiaweze kuona tunafanyaje hapo kuwasaidia wananchi wa Vijiji vya Ilagala na vitongoji vyake kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwenye kitabu chake ni jinsi gani Wizara wanajipanga kutekeleza Mradi wa Usambazaji Maji kutoka kwenye Maziwa Makuu kwa maana ya Ziwa Nyasa, Ziwa Victoria pamoja na Ziwa Tanganyika. Mimi najiuliza maswali sipati majibu, Ziwa Tanganyika maji yake ni baridi, ni kama tu maji haya ya Kilimanjaro na maji mengine, kwa nini hakuna mkakati maalum wa kuvisaidia vijiji 34 ambavyo vinapakana na Ziwa Tanganyika. Ukiangalia wananchi wale wanakaa karibu na Ziwa lakini hawana maji safi na salama. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri watakapokuwa na mkakati wa makusudi, naomba basi watambue kwamba Jimbo langu lina vijiji 34 vinavyopakana na Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mpango mkakati wa Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo by that time, kwamba wanataka kutekeleza mradi mkubwa wa Mto Malagarasi. Sasa sijajua Mheshimiwa Waziri mradi ule umefikia wapi? Labda Jumatatu akija hapa kuhitimisha atuambie ule mpango mkakati wa Mradi huu mkubwa wa Mto Malagarasi umefikia wapi, kwa sababu kama sisi watu wa Kigoma tukiweza kupata Mradi kutoka Ziwa Tanganyika pamoja na wenzetu wa Katavi na Rukwa, lakini tukapata pia Mradi wa Mto Malagarasi hata wenzetu wa Kaliuwa, wenzetu wa Urambo pia watapata maji safi na salama kupitia katika Mradi huu mkubwa wa Mto Malagarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niiombe sana Serikali iangalie namna ya kuwaongezea pesa wenzetu hawa wa Wizara ya Maji. Nasema hivi kwa sababu kwenye bajeti ya 2018/2019, Wizara hii ilipangiwa takribani shilingi bilioni 697 na ushee, lakini kwenye bajeti hii Wizara imepangiwa pungufu ya shilingi bilioni 66. Sasa niiombe sana Wizara ya Fedha, najua kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri yupo hapa, hii Wizara ni Wizara nyeti sana, wengi wameongea kila mtu ameongea kwa hisia zake kwa sababu sisi Serikali yetu kupitia Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tunasema kwamba tutamtua mwanamke ndoo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri Mheshimiwa.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwakuunga mkono hoja nakuzidi kuwapongeza Mawaziri pamoja na Katibu Mkuu. (Makofi)