Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MENRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nichangie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji ni suala la kipaumbele, bila maji hatuwezi kuifanya kitu chochote. Kwanza kabisa namshukuru sana Waziri pamoja na Naibu kwa kazi nzuri mnayoifanya. Na sisi Wabunge inabidi tukusaidie kwa kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inahitaji kupata fedha nyingi sana. Sisi Wabunge tuliangalia tozo ya mafuta ile shilingi 50 lakini tunaona kuna ugumu wake na ili Wizara ipate fedha nyingi, nilikuwa napendekeza kwa sababu kila Mbunge akisimama tunaomba maji, kuna vijiji, kata, kuna sehemu nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa mapendekezo kwamba mnaonaje kwenye Wizara hii vitu vyote vinavyohusiana na maji tufute kodi, tufute kodi vyote. Kwa mfano, vifaa vya maji tufute kodi, watu wanaochimba visima tufute kodi, miradi mikubwa ya maji, tufute kodi ili Wizara iweze kupata fedha za kutosha na watu wengi sana wanajitolea. Kuna mashirika mengi sana yanajitolea kuleta maji katika nchi yetu. Mtu yeyote anayeleta maji hafanyi biashara, hii ni huduma ya jamii. Sasa ili tuweke kipaumbele na wananchi wapate maji ya kutosha, basi vifaa vya maji inabidi viwe vya bei ya chini sana, hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya maji ambayo tumewapa wakandarasi wazawa, kuna uzembe mkubwa sana. Serikali inatoa fedha lakini miradi haiishi kwanini? Kuna miradi mingine imetengenezwa lakini haitoi maji. Ukienda kuangalia mabomba yanakaa siku mbili/tatu yameharibika. Hili ni tatizo kubwa sana. Unaweza ukaona fedha nyingi sana imekwenda lakini ukaenda kuangalia utekelezaji wake sio imara! Hilo ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwenye usimamizi wa miradi ya maji inabidi uongezeke mara tano, tusimamie vizuri sana kwenye miradi hii. Kwenye jimbo langu kuna miradi mikubwa ya maji Serikali ilitoa fedha, nataka nikuambie kuna mradi wa Mtwango ule, wa Sawala Mheshimiwa Waziri aliyepita alikuja na akasaini mkataba mbele ya wananchi. Naibu Waziri umekuja wewe ni shahidi, umeona pale mradi mpaka Serikali imeshatoa zaidi ya millioni 700. Mpaka leo tunavyoongea hivi, maji bado hayajatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mtiririko wa fedha, zinakwenda lakini mkandarasi hafanyi kazi na Serikali bado tunaangalia tu. Mkandarasi yule hafanyi kazi mpaka leo wananchi wa Kata ya Mtwango, vijiji karibu sita havina maji na Serikali imepeleka pesa. Zaidi ya miaka miwili, mradi unakwenda, mkandarasi yuko site. Ni tatizo! Tutafanyaje kulitoa hilo tatizo na tumesema wazawa, wakandarasi lazima wapewe kazi hii lakini hawafanyi kazi ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine kwenye Kata ya Itandula pale Kiliminzowo Serikali ilipeleka nilioni 800, milioni 800 zilikwenda pale, mradi ule mpaka leo unatoa maji ya kusua sua tu ya wasi wasi. Serikali imepeleka pesa, wakandarasi wako pale wananunua vifaa sijui vifaa gani vile, vinakaa siku mbili vimeharibika. Tunafanyaje hilo, ni tatizo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu nina matenki karibu saba yalishachakaa, miundombinu imechakaa. Kwa mfano ukienda pale Nyololo, Waziri siku ile umekuja na uliniahidi kwamba watoe tenda pale mkandarasi aingie site. Nakupongeza sana Waziri, ulitoa bilioni 1.4 kwa Kata ya Nyololo lakini mpaka leo hii hawajatangaza tenda ile na wewe kibali ulishatoa. Wewe umetoa kibali tarehe 15 lakini tenda haijatangazwa mpaka leo na fedha zipo watu wanasuasua, tunafanyaje hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bilioni 1.4 iko Nyololo kwenye Jimbo langu, Waziri umetoa kibali, watu hawafanyi kazi wako ofisini. Hili ni tatizo kubwa sana hili. Kata ya Igowole ni kata kubwa sana, pale ni mjini, tenki la maji liko pale, lina miaka zaidi ya 10. Wananchi wanakunywa maji Mbunge nilichimba visima pale ambavyo mimi nilisaidia lakini na tenki la maji liko pale, kwenye bajeti tulitenga milioni 400, mpaka leo hakuna mradi pale, wananchi wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vyanzo vya maji Mufindi vimejaa, ni vingi! Sisi tuna vyanzo vya maji vingi sana, ile ya kuchimbachimba visima mimi Mbunge, nimechimba visima vingi pale kwenye jimbo langu lakini kuna vyanzo vingi vya maji ambavyo tunaweza tukatengeneza maji ya gravity system. Naiomba Serikali tusimamie vizuri sana kwenye miradi hii ya maji. Sasa hivi Serikali inafanya vizuri kwa kutoa fedha, naishukuru sana, Serikali ya Awamu ya Tano fedha inapeleka lakini usimamizi sio wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hatuwezi kuilaumu Serikali jinsi ya kupeleka fedha kwenye majimbo, inapeleka! Lakini usimamizi mbovu sana na hii haitakubalika Serikali iwe inapeleka fedha halafu kuna watu wengine wanafanya mchezo hawafanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ampongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Yule huwa anawaweka ndani wazembe wa kazi, safi kabisa! Mkuu wa Mkoa wa Iringa, uendelee na mtindo huo. Weka wengi tu ili wajifunze kwa sababu sisi tunataka watu wafanye kazi inavyotakiwa na katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tunatekeleza vizuri na hakuna mtu anaweza akabishana na Ilani, imekaa vizuri lakini watendaji wanatudondosha hasa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba kwenye Jimb o langu la Mufindi Kusini, Kata ya Mtambula, Itandula, Idunda, Mbalamaziwa, Malangali, Mtambula, Igowole, Mninga, Mtwango, Luhunga, sehemu zote zipewe maji. Bahati nzuri nawapongeza na wafadhili wangu RDO walipeleka mradi mkubwa sana Kata ya Luhunga, nawapongeza sana walifanya vizuri. Nawapongeza sana watu wa UNICEF wako vizuri, wametengeza mradi pale Ihowanza umekaa vizuri sana. Nalipongeza Shirika la Water for Africa ambalo tulianzisha pamoja na ninyi, wanafanya kazi nzuri sana nawaombe tuwapunguzie kodi ili wafanye kazi vizuri. Wafadhili wanaojitolea kwanini umtoze kodi na anatoa maji bure yeye hafanyi biashara. Kuna mashirika mengine ya dini yanatoa msaada wa maji, kwanini tuwatoze kodi? Wale hawafanyi biashara ni kwa wananchi. Hili lazima tuliangalie vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji tukiwekea unafuu wa vifaa itakuwa vizuri, wala hakuna inflation, wengine wanasema labda inflation itaharibu, hakuna hiyo! Na kipaumbele cha kwanza kwa wananchi ni maji. Maji ni uhai, hakuna kitu kingine. Hapa hata tukipiga kelele ni kipaumbele cha kwanza cha wananchi ni maji vijijini. Mijini sasa hivi Serikali imejitahidi sana hata hapa Dodoma naona watu tunapata maji. Lakini vijijini tatizo ni kubwa, kuna watu bado wanatembea kilometa nne kilometa tatu wanatafuta maji. Kuna watu wengine wanachota maji na punda. Ukipita hii njia ya Iringa, ukitoka hapa kwenda Iringa utakutana na punda humo njiani wanatafuta maji huko na huko. Hili tatizo lazima tulifute kabisa lisiwepo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)