Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi siku ya leo kuweza kuchangia Wizara hii muhimu sana katika maisha ya wanadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mungu ambaye ametuumba na kutupa uzima na uhai na ametupa kibali siku ya leo, tu wazima tukiendelea kutenda kazi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwenye sekta hii ya afya. Mkoa wa Katavi tunajivunia sana jinsi pesa za Wilaya pamoja na Mkoa zilivyokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Ummy hongera sana kwa kazi. Mwanamke mwenzetu unafanya kazi lazima tukusifie na tunaendelea kukuombea Mungu aendelee kukupa nguvu kwa sababu Wizara hii ni ngumu, inahusu wanadamu, tunaendelea kumsihi Mungu aendelee kukutetea katika kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa Mkoa wa Katavi tushukuru katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tuliletewa shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa. Vilevile katika Wilaya za Tanganyika na Mlele pamoja na Jimbo la Kavuu tumeletewa pesa kwa ajili ya kujengewa Hospitali ya Wilaya. Tunaishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kwa ajili ya kuwatibu Watanzania hususan wa Mkoa wa Katavi. Sisi tunajivunia sasa vifo vya akina mama wajawazito na vifo vya utotoni vitapungua kwa asilimia kubwa sana kwa sababu tulikuwa tuna asilimia kubwa sana. Kupitia jitihada kubwa za Serikali mambo yataendelea kuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi, Manispaa ya Mpanda tuna Hospitali Teule ambayo imeteuliwa kama ndiyo sasa Hospitali ya Mkoa. Hii hospitali ina mabweni manne tu. Katika wodi ya wazazi kuna sehemu wameweka kwa ajili ya kulea watoto njiti. Naomba sana Wizara itusaidie kwa sababu hospitali zote za Mkoa na hii tayari teule Mheshimiwa Ummy na wewe uliniahidi kuwa utatujengea bweni moja katika Hospitali ile Teule ya Mkoa wa Katavi, Manispaa ya Mpanda. Wale watoto njiti wanakaa pamoja na mama zao humohumo watu wakienda kuwatizama, nafikiri unajua watoto njiti wanatakiwa wakae katika hali ya usalama zaidi ili waweze ku-survive.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na matatizo ya mabweni haya kuwa machache, wodi ile ya magonjwa mchanganyiko ipo moja tu. Wodi ile wanalazwa watu wazima, watoto kuanzia miaka 5 mpaka 13, ina maana hawa watoto ni wadogo. Pia wagonjwa wanaoingia katika wodi ile ni mahtuti watoto wale wanashuhudia vifo vya wagonjwa mle ndani, ina maana tunawapa woga wakiwa wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Katavi hususan Wilaya ya Mpanda Manispaa tunaomba Mheshimiwa Ummy utujengee mabweni mawili mengineā¦
MBUNGE FULANI: Ni wodi.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Wodi ndiyo mabweni Waheshimiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tujengewe wodi mbili ili hawa watoto umri wa kuanzia miaka mitano wawe wana wodi yao kwa sababu kisaikolojia tunawapa uwoga kwa sababu wakati mwingine wako kitanda kimoja na mkubwa yule mkubwa anafariki pale yeye anaendelea kuweweseka. Katika maisha yake anakuwa na uwoga, tunamjenga hofu katika maisha yake yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ummy alishakuja Mkoa wa Katavi Manispaa na aliona hospitali ile jinsi ilivyo tunaomba tujengewe wodi mbili. Tunashukuru mmetuletea shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na jumla ya fedha zote mpaka hospitali iishe ni shilingi bilioni tisa. Mmetupa shilingi bilioni 1 nafikiri na sasa hivi mtatupa shilingi bilioni 1 ina maana mpaka ujenzi uishe ni miaka tisa ijayo tutakuwa bado tuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Waziri utuongezee fedha ili Hospitali ya Mkoa iweze kuisha haraka. Tukipiga hesabu ya shilingi bilioni moja moja ile hospitali itaisha baada ya miaka tisa mbele ya safari. Ina maana kuwa lazima tupate msaada wowote ili ile Hospitali Teule iweze kurekebishwa mambo mbalimbali ili iweze kukidhi haja ya wananchi wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya hospitali hii watumishi ni wachache sana na ndiyo teule na tunaitegemea kama Hospitali ya Mkoa. Hatuna madaktari bingwa wanaokidhi haja ya kutibu magonjwa mbalimbali. Ndiyo maana unakuta wananchi wengi wa Mkoa wa Katavi wanahangaika sana. Wengine wanafia nyumbani kwa sababu akienda hospitali kumefurika, hapati matibabu halisia, vifaatiba hatuna na manesi ni wachache. Tunaomba mtusaidie ili hospitali hii iweze kukidhi vigezo vinavyohitajika kimkoa. Wakati mnaoendelea kutuletea pesa na hii hospitali iendelee kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja upande wa bima ya afya. Bima ya afya ni kiwango kikubwa sana na Watanzania uwezo wao bado ni mdogo, Sh.1,500,000 mtu aweze kukata bima ya afya ni pesa nyingi sana. Wengi wanakufa wakiwa nyumbani kwao na mimi mwenyewe nashuhudia. Sasa hivi tuna maradhi makubwa makubwa ya moyo, kansa, figo aje Benjamin huku na hana bima matokeo yake huyu mtu anakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ile bima ya afya tuliweka ya vikundi ya Sh.79,000 tuichanganue akate mtu mmoja mmoja mwenye uwezo, tumpe fursa akate hiyo bima. Naomba niipongeze Serikali mmeleta bima ya mkoa ya Sh.30,000 wananchi wameitikia lakini sasa unakwenda kwenye Hospitali ya Mkoa hakuna vile vifaa mfano moyo umepanuka wanakwambia nenda Muhimbili, ukienda Muhimbili ile bima haifiki kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii bima tui- separate tufanye hata Sh.100,000 yule mwenye uwezo aweze kukaa Bima hii ya Taifa ili aweze kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye kitabu chake ukurasa wa 85, Mheshimiwa Ummy anataka kuleta sheria kwa ajili ya bima ya afya. Naomba nikupongeze sana, tuletee hii sheria tuweze kurekebisha yale mapungufu ili Watanzania waweze kupona. Watanzania wengi wanakufa majumbani, kuna wagonjwa majumbani mpaka unashangaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye magari ya wagonjwa ndani ya Mkoa wetu wa Katavi. Jiografia ya Mkoa wa Katavi ni ngumu mno. Tunaomba mama yetu atupe hata ambulance tatu tu ziweze kutusaidia kwani tuna shida. Mheshimiwa Ummy ni msikivu naamini atatusaidia haya magari ya wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wale mabinti zako wa Kalema Girls Mheshimiwa Waziri wanakukumbusha ile bajaji uliowaahidi kwa ajili ya matibabu ya asubuhi. Usisahau, naomba nalo unijibu utawaletea lini hiyo bajaji. Nafikiri ulisahau, naomba nikukumbushe bajaji Kalema Girls.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende maendeleo ya jamii. Ndani ya Mkoa wetu tuna Chuo cha Msaginya na safari hii kimepata bahati mbaya kimeshaungua mara mbili. Katika hotuba ya Waziri kuna vyuo ambavyo vimepatiwa pesa ya marekebisho na amesema vimefanya kazi nzuri kwa ajili ya hamasa mbalimbali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri utusaidie hiki Chuo cha Msaginya kiweze kufanya kazi kama Vyuo vingine vya Maendeleo ya Jamii. Chuo hiki kwa Wanakatavi ndiyo kitakuwa msaada mkubwa sana kwa sababu tumeona vyuo vya wenzetu vimefanya kazi nzuri. Ukitupatia fedha na kikafanyiwa marekebisho mazuri, nafikiri Wanakatavi wanaoishia darasa la saba wataenda kujifunza kozi mbalimbali na kupata manufaa ya Chuo hiki cha Msaginya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100.