Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii ya kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote napenda kumpongeza Waziri wa Elimu na Naibu Waziri pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Elimu kwa kutayarisha Hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa pole Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye amefiwa na mama yake mpenzi, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Kabla sijachangia kwenye hotuba hii kwanza kabisa ninalo ombi, ombi langu ni kwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na Waheshimiwa Mawaziri. Wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanatumia dehumanizing terminologies kwa mfano vilema, siyo wote nimesema baadhi na pia kuna baadhi ya Mawaziri wanatumia neno kama vilema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotumia neno vilema, maana yake vi ni non-living object yaani ni kitu ambacho hakina uhai tunasema viti, vikombe, vijiko lakini watu wenye ulemavu ni watu. Kwa hiyo, naomba tutumie lugha ya kuwathamini na kuwapa utu watu wenye ulemavu, kwamba ni watu wenye ulemavu na sio vilema. Ahsante naona hilo limeshakuwa noted. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kuchangia hotuba, kwanza napenda kumshukuru Waziri alipokuwa akitoa Hotuba yake alisema kwamba, elimu maalum ameipa kipaumbele katika Wizara yake, hiyo nashukuru. Katika kuipa elimu maalum kipaumbele, napenda kuchangia kwa kuanzia ule mtambo wa kuchapisha vitabu vya nukta nundu ambapo upo chini ya Wizara ya Elimu, upo pale Uhuru Mchanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mtambo ulianzishwa katika miaka ya 70 kwa msaada wa Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la CIDA kwa ajili ya kuisadia Wizara ya Elimu iweze kutoa maandishi ya nukta nundu kwa wanafunzi wasioona pamoja na maandishi makubwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu, pamoja na kutengeneza zile hearing aids kwa wale wanafunzi ambao wana upungufu wa kusikia. Hata hivyo, baada ya Shirika la Sweden kusitisha msaada wake kwenye miaka ya 80, ufanisi wa ule mtambo wa kuchapisha vitabu vya maandishi ya braille ambao ni mtambo pekee hapa Tanzania, Tanzania nzima, mashule yote ya msingi pamoja na sekondari yanategemea mtambo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanisi wa mtambo huu umekuwa ni duni, jengo limechakaa, mashine ni mbovu, Mheshimiwa Waziri mwenyewe alishafika pale anajua. Wafanyakazi wanaopelekwa pale ni wafanyakazi wasiokuwa na uwezo na mara nyingi Wizara ya Elimu imekuwa ikipeleka wafanyakazi ambao wana matatizo, wale wanaohitaji light duty ndiyo wanapelekwa kufanya kazi pale. Matokeo yake hivi tunavyoongea katika shule zote za watoto wasioona na wale wenye uoni hafifu, msingi pamoja na sekondari hawana vitabu vya text book na hawana vitabu vya kiada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria mwanafunzi anaingia darasani, wenzake wanapata vitabu vya masomo yote jiografia, historia, lakini mwanafunzi asiyeona hana kitabu chochote anachosoma, anaingia pale kusikiliza na kuondoka bila kupata vitabu, ni kwa sababu uzalishaji wa vitabu vya namna hiyo umekuwa ni duni na umekuwa na matatizo, mashine hakuna zilizopo ni mbovu, rasilimali hakuna wenye uwezo. Kwa hiyo, production ya ile Braille Press imekuwa chini kiasi kwamba shule zetu sasa hivi wanafunzi wetu wasioona na wale wenye uoni hafifu hawana vitabu vyovyote vya kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ambaye hili suala analijua afanye jitihada kuona kwamba ule mtambo umekuwa equipped, jengo limetengeneza, wanapelekwa pale wataalam wenye uwezo wa ku-produce hiyo braille press ili supply ya vitabu vya nukta nundu mashuleni liweze kutosheleza, ambapo sasa hivi hakuna kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo la kile chuo kimoja tu Tanzania nzima, Chuo cha Patandi ambacho kinatoa elimu maalum kwa Walimu wa elimu maalum. Mpaka 2010 Tanzania hii ilikuwa na shortage ya Walimu wa elimu maalum 16,000 na sasa hivi wameongezeka. Chuo cha Patandi ambacho kina miundombinu ambayo ni mibaya, inahitaji matengenezo, hawana vifaa vya kufundishia wala vya kujifunzia, kinahitaji kupewa vipaumbele na Wizara ya Elimu ili kiweze kutoa Walimu wa elimu maalum wa kutosha. Kwa mwaka wanatoa Walimu kati ya 150 mpaka 250 tu, lakini nimesema upungufu hadi sasa ni zaidi ya 16,000 wa elimu maalum wanaohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo shule za msingi ambazo zinakaribia 90 ambazo zinachukua wanafunzi mbalimbali wasioona na walemavu wa aina nyingine. Tunazo shule za sekondari, lakini pamoja na hayo Walimu wa elimu maalum ni wachache na chuo ni kimoja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009, Wizara ya Elimu ilitoa inclusive and special need education frame work ambapo ilisema kati ya 2009 mpaka 2017 vyuo vingine vitakuwa vinatoa dozi ya elimu maalum kwa ajili ya kwamba Walimu wanapohitimu wanakuwa na ufahamu wa jinsi ya kuwashughulikia au jinsi ya kuwapokea na kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpaka sasa hivi ile frame work bado haijatekelezwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri afuatilie hiyo education frame work ya inclusive education ili tuweze kuona inafanya kazi na vyuo vingine vyote vinapata component ya special education ili waweze kuwapokea wanafunzi wenye elimu maalum katika shule zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija suala la elimu bure, Waziri sijaona ni mipango gani ameiainisha kwenye hotuba hii, jinsi wanafunzi wenye ulemavu nao watakavyofaidika na huu mpango wa elimu bure. Wapo wengi ambao wana umri wa kwenda mashuleni wapo majumbani, shule zilizopo hazitoshelezi na sijaona mikakati ambayo ipo kwa ajili ya kuwafaidisha wanafunzi au watoto wenye umri wa kwenda shule wenye ulemavu na wao wafaidike na hii elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la wanafunzi viziwi, mpaka sasa hivi wanafunzi hawa wana matatizo ya kupata Walimu wakalimani wa lugha ya alama wa kuwafundisha katika mashule. Kwa hiyo, naomba pia kuwe na mkakati wa kuimarisha mafunzo ya lugha ya alama ili wanafunzi hao nao wapate nafasi ya kupata elimu kama wanavyopata wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa Elimu awasiliane na Waziri anayeshughulika na sera kuhusu watu wenye ulemavu. Kuna Treaty ya Kimataifa ambao inaitwa Marrakesh Treaty, hii Treaty inatakiwa iwe ratified na nchi 20 ili iweze kufanya kazi na inasema kwamba inawalazimisha publishers au wachapishaji waweze kutoa maandishi ya vitabu vyao wanavyochapisha katika accessible format.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ikiwa imeshasaini na kuridhia, Serikali ina uwezo wa kuwalazimisha publishers waweke maandishi yao katika maandishi ambayo yanaweza kusomwa na watu wasioona pamoja na watu wengine ambao wana matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida kama watu wenye Dyslexia au kama watu wenye down syndrome ama kama watu wenye uoni hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii sheria kama itaridhiwa itasaidia pia ile wanaita cross border literature, ni kwamba kama kuna nchi moja inatoa vitabu ambavyo vinaweza kutumia katika nchi nyingine, hiyo sheria inawataka wale watu wenye copyright waruhusu kazi zao ziweze kusafirishwa katika nchi nyingine ili wanafunzi wenye matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida waweze kupata nafasi ya kusoma vitabu hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itilie mkazo somo la computer kwa wanafunzi wenye ulemavu waweze kwenda na teknolojia. Wanafunzi wenye ulemavu wakipata nafasi ya kujua teknolojia, ya kujua kompyuta watakuwa na uwezo zaidi wa ku-access information, wataweza kwenda kwenye vyuo vikuu bila matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.