Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jina naitwa Kiteto Zawadi Koshuma, ni Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Spka, kwanza kabisa, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, japokuwa muda ni mdogo lakini nitachangia kwa kiasi fulani. Kwanza naomba niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Mwanza ambao wameweza kuniamini ili kuwawakilisha katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niongelee kuhusiana na hotuba ya Rais ambayo ilikuwa nzuri sana na imeweza kugusa nyoyo za Watanzania na kuweza kuwaonyesha Watanzania kwamba Tanzania sasa tunaweza tukawa na matumaini na Tanzania yetu na tukaishi kwa amani na mategemeo makubwa sana kutoka katika nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Rais kabla sijaendelea ili muda usije ukaniishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongelea kuhusiana na mama lishe kitu ambacho kilimgusa sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alipowaongelea mama lishe alisema Serikali sasa imefikia wakati iwatambue pamoja na shughuli zao wanazofanya. Mama lishe wamekuwa wakidharaulika sana, kama ambavyo Wabunge wengine wametangulia kusema.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikazie kwamba Waziri husika wa TAMISEMI atusaidie kwa kuwasiliana na Halmashauri zinazohusika ili ziweze kuwashirikisha kuhusu ni maeneo gani ambayo ni rafiki kwao kuweza kufanya shughuli zao za mama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mchango mkubwa ambao mama lishe wanao katika jamii yetu. Wengi wetu tunakula chakula kwa hawa mama lishe, lakini pia hawa mama lishe ambao wanatupatia chakula, wanajisaidia na wao kupata kipato, ambapo wanaweza wakatatua matatizo mbalimbali. Kama tunavyojua katika familia, mama pekee ndio mtu ambaye anajua kwamba watoto wamekula nini au baba amekula nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, naomba Serikali sasa ifikie hatua ya kuwatambua hawa mama lishe na kufahamu kazi ambazo wanazifanya kwamba zinachangia katika pato la Taifa na kukuza uchumi wa Taifa, hasa ukiangalia katika kauli mbiu ya Rais ambayo inasema Hapa Kazi Tu na sasa hivi ni kazi tu, hivyo tuwatambue hao mama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia aliguswa sana tatizo la bodaboda. Bodaboda ni vijana wetu ambao, badala ya kutangatanga na kuwaibia watu kwenye mifuko yao wameamua kujiajiri kwa kupitia pikipiki ili waweze kujipatia kipato na hatimaye kutatua matatizo yao. Bodaboda hawa wamekuwa wakipata matatizo ya kuhamishwa kwenye vituo vyao ambavyo wanapaki kwa ajili ya kupata abiria.
Naiomba Serikali yangu ambayo ni sikivu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, iwasikilize hawa watu wa bodaboda, wawawekee vituo ambavyo na wao pia kwao ni rafiki ambapo wanaweza kupata abiria. Hii ni kwa sababu, nimegundua katika Halmashauri nyingi wanapangiwa vituo ambavyo siyo rafiki kwao. Boda boda hupangiwa sehemu ambayo hawezi kupata abiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu sikivu, itusaidie, mshuke kwenye Halmashauri ili muweze kuzishauri kwamba wanapotaka kuwapangia vituo hawa watu wa bodaboda, basi waweze kuwashirikisha ili wao pia wawepo katika kuchangia maamuzi kwamba ni wapi tukae ili kuweza kupata abiria na hivyo basi kuweza kusaidia katika shughuli zao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nichangie upande wa viwanda suala ambalo Mheshimiwa Rais amelipa kipaumbele sana. Suala hili kama ambavyo wengi wametangulia kusema kwamba bila viwanda Tanzania haitaweza kuendelea, lakini sasa viwanda hivi vitaendeleaje kama hatutaweza kuwashirikisha watu ambao tayari wanahusika na viwanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika Mkoa ninaotoka, Mkoa wa Mwanza ni Mkoa maarufu sana ambao samaki wa aina ya sato wanapatikana, lakini ni viwanda vichache sana ambavyo viko pale, kama vile Vic Fish, TFP na viwanda vingine lakini ni vichache sana.
Naiomba Serikali yangu inapokuwa inaleta mpango kazi wake, basi iangalie huu Mkoa wa Mwanza na kuufanya kuwa mkoa wenye viwanda. Kwa sababu gani nasema hivyo? Mwanza tunapata samakiā€¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa mzungumzaji)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie sentensi yangu. Pale Mwanza pia kuna Kiwanda cha Ngozi...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda tafadhali! (Kicheko)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)