Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri inayofanya ya kuboresha huduma za afya nchini kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuelezea changamoto za Hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Hospitali hii inatoa huduma katika maeneo mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo hospitali ya rufaa ya zamani katika Kata ya Ipembe na hospitali mpya ya rufaa iliyopo katika Kata ya Mandewa. Uendeshaji wa hospitali hizi mbili kwa wakati mmoja imepelekea gharama za uendeshaji kuwa kubwa kwa kuwa inatumika bajeti moja kulipia bili ya maji, umeme, ulinzi na usafi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini sasa Serikali isimalizie Hospitali ya Rufaa ya Mandewa yale majengo muhimu kama maabara, pharmacy, wodi ya upasuaji kwa magonjwa ya kwaida na mifupa, wodi ya watoto, jengo la macho na jengo la meno? Iwapo majengo haya yatakamilika yatasaidia sana hospitali ya rufaa ya zamani iliyopo Kata ya Ipembe kuhamia hospitali ya rufaa mpya ya Mandewa. Naiomba Serikali itenge fedha za kutosha ili kumaliza Hospitali hii ya Rufaa ya Mandewa kwa kuwa majengo ambayo yalishakamilika yameanza kuchakaa hata kabla ya kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali yangu ya rufaa ina changamoto lukuki; haina madaktari bingwa wa kutosha, waliopo ni sita tu na kati ya hao sita hakuna daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto lakini pia ina wauguzi wachache. Wauguzi waliopo katika hospitali hii ni 144 kati ya 305 wanaotakiwa. Naomba Serikali itupatie watumishi wa kutosha wakiwemo wauguzi kwani hospitali hii ndiyo tegemeo la wananchi wa Mkoa wa Singida katika kupata huduma za afya za kibingwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali hii pia haina gari la kubebea wagonjwa (ambulance), gari lililopo lilipata accident takribani miaka mitano iliyopita. Jambo hili nimekuwa nikilileta kwenu mara kwa mara, naomba sana sana kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Sindida ifike wakati sasa Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ipatiwe gari la kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hospitali zangu zote za Wilaya ikiwemo ya Wilaya ya Iramba na Manyoni hazina magari ya kubebea wagonjwa. Naomba sana hospitali hizi za Wilaya zipatiwe magari ya kubebea wagonjwa ili kuokoa vifo vya akina mama na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naomba kuwasilisha.