Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuweza kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Elimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nguvu kwa kuniwezesha mimi kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati na kumpongeza ndugu yangu Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri ambayo ameanza nayo katika kipindi hiki kifupi na kuleta matumaini kwa wale wanohitaji elimu bora katika nchi hii, ahsante sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda kutoa shukrani kwa dada yangu Stella Manyanya Naibu Waziri. Awali ya yote tunamuomba Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema mama yetu mpenzi na mwanga wa milele umwangazie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita katika suala zima la msingi wa elimu. Elimu ni kila kitu ndugu Waheshimiwa Wabunge, hakuna kitu ambacho kitakachoanzishwa ama kitakachofanyika katika nchi au mahali popote pale pasipokuwa na elimu, kwa hiyo elimu ndio msingi wa maisha yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninapenda kuzungumzia kwenye suala zima la elimu ya awali. Tumeweza kuanzisha madarasa katika shule za msingi madarasa ya awali lakini bahati mbaya walimu husika na kufundisha madarasa yale ya awali hawapo walimu hao na kama wapo hawatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia kwamba, hawapo ni kwa sababu katika shule zetu walimu wakuu wanachukulia sifa ya kumpatia mwalimu kufundisha darasa la awali ni mwalimu ambaye amefundisha kwa muda mrefu au ni mwalimu ambaye amebakiwa na miaka miwili au mitatu ya kustaafu ndio anayoelekezwa kwenda kufundisha watoto wa somo la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hilo sio sahihi, tunaomba Serikali ijipange na ijitoe kuhakikisha ya kwamba inaandaa walimu wa kwenda kufundisha watoto wetu wa madarasa ya awali kwa sababu ndio msingi wa elimu. Bila kuwa na msingi bora ni dhahiri kusema ya kwamba uinuaji wa elimu bora na mafunzo bora katika nchi yetu hautawezekana kwa sababu watoto hawa watakuwa hawajapata msingi bora wa ufundishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Serikali, ninaomba Wizara iweke utaratibu maalum wa kufuatilia kwanza, kufatilia katika shule zetu za msingi kuona ile elimu inayotolewa kwa watoto wetu kama inaafiki ama inaswii katika kuhakikisha kwamba wanapata elimu bora. Hapo ndipo tutakapoonda kwamba kweli tumedhamilia kuinua elimu bora na mafunzo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu watoto wasichana, wasichana ni kwa maana ya kwamba, hao ndio watakaokuwa wakina mama wa kesho kama sio wakina mama wa leo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia ni ujenzi wa mabweni ya shule za sekondari. Ninawaomba Serikali iliweka msukumo wa kujenga sekondari kila kata na tumejenga sekondari kila kata na katika sekondari zile kuna watoto wasichana na watoto wa kiume, lakini hawa watoto wasichana ambao akina mama wa kesho wanakuwa na mitihani walimu wanawapa mimba, wananfunzi wenzao wanawapa mimba, sisi wenyewe wakubwa tunawapa mimba kwahiyo hawa watoto wanakuwa na mtihani mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali ione umuhimu wa kukamilisha mabweni ya watoto wasichana katika mashule yetu kuhakikisha kwamba samani zinakuwemo ndani ya mabweni hayo vitanda, magodoro na kadhalika ili kujenga mabweni yale yawe ni rafiki kwa watoto wetu wasichana ili angalau wapunguze ile taratibu ambayo wanaopata mimba ambazo zisizokuwa na wakati muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la hawa akina dada, wale wanaowapa mimba wanapobainika ninawaomba wapatiwe adhabu kali tena kali sana. Kwa sababu wanapunguza muonekano wa wale akina mama katika mafunzo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba ninaiomba Serikali hawa watoto wanaopata mimba ninawaomba wawaandalie fursa muafaka wa kuwawezesha hawa watoto wanapomaliza kujifungua, watoto wabaki wazazi wao, wao waendelee na masomo jamani, hili limekuwa ni kilio cha kila mara sasa limefikia wakati kwa Mama Ndalichako nafasi kwa Mama Manyanya mmepewa ninyi wanawake kwa sababu mnauchungu na watoto.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuwaonee uchungu hawa watoto wa kike, tuwaonee uchungu hawa watoto wa kike na tunajua ya wazi kwamba, ukimuelimisha mwanamke mmoja umeelimisha jamii nzima. Sasa kwanini tuwapoteze hawa kwa kuweza kuja kuendeleza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuweke fursa maalum ya kuhakikisha hawa watoto wa kike wanapomaliza kujifungua watoto wanawaacha nyumbani wao wanaendelea na masomo ili tuweze kupata maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kulizungumzia suala zima la wanasayansi. Tumesema nchi yetu itakuwa ni nchi ya viwanda, tuanze na viwanda vidogo vidogo, lakini hatuwezi kuwa na viwanda endelevu ikiwa hatuna wataalam wa kisayansi, ni lazima tuandae wanasayansi wa kuja kuendesha hivi viwanda vyetu, ili viwanda vyetu visiweze kufa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanyaje basi, tumeanzisha maabara katika shule za sekondari zote, lakini maabara hizi katika mashule yetu yana changamoto, changamoto iliyopo ni walimu wa sayansi hatuna. Vifaa vya sayansi katika maabara yetu havipo na ukiachia Halmashauri uwezo wa kununua vifaa vile ni aghali sana hawawezi Halmashauri kuweza kutekeleza na kuweka katika maabara zote za Sekondari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali natunamuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho atuaeleze amejipangaje na uwekaji wa vifaa au samani za maabara katika mashule yetu ili tupate walimu wa kutosha na hatimaye tupate wanasayansi wa kuja kuendeleza viwanda vyetu hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa ushauri ni vyema wakaweka utaratibu maalum wa kuweka vivutio kwa walimu hawa wa sayansi, na kuweka vivutio kwa wanafunzi hawa wanaopenda sayansi, vinginevyo tutaweza kupoteza maana ya kuhakikisha kwamba, tunajenga viwanda katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika suala la walimu, walimu wanaokuja katika maeneo yetu kama sisi Mikoa yetu ya pembezoni Mkoa wa Rukwa, kwenda kule vijijini wamekuwa na taratibu za kuja ku-report wakishaingia kwenye payroll wale walimu wana-disappear katika yale maeneo kwa sababu mazingira yale ni mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulikuwepo utaratibu na hata na baadhi ya Mikoa walijaribu kuanzisha taratibu hizo za kuwawezesha walimu hawa kwenda kuishi kule mfano Rukwa walianzisa Nyerere Fund ambayo kwamba sasa hivi hai-operate vizuri, lakini vilevile na Serikali wangeweza kuweka package nzuri ya kuhakikisha kwamba huyu mwalimu anapokwenda kule anakwenda katika ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Rukwa walikuwa wanapewa vitanda, magodoro, vyombo na sehemu kidogo ya kwenda kuanzia maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Wizara iweze kuona suala hili ili tuwe na walimu hawa katika shule zetu, katika ukamilifu. Walimu wanafanya kazi moja kubwa mno, sisi sote hapa tusingekuwepo kama kungekuwa hakuna mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi tunachokiomba hii Wizara ya TAMISEMI imepewa mambo mengi mno, kwa sababu changamoto zote za walimu, changamoto za wanafunzi zipo TAMISEMI, lakini wanaolaumiwa ni Wizara ya Elimu, tunaomba hii Wizara ya Elimu ijitegemee kwa sababu ina mambo mengi ya kuweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wameanza Tume ya Walimu lakini bado haitoshelezi mahitaji, tunahitaji elimu iwe na Wizara inayojitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenykiti, lingine ni kuhusu na VETA Mkoa wa Rukwa umeanzishwa nadhani ni mwaka 1974 ama ni 75 lakini mpaka hivi leo Mkoa wa Rukwa hatuna VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vijana wengi wanaomaliza darasa la saba, tunao vijana wengi wanaomaliza darasa la 12 lakini wanakuwa hawana mahali pa kushika, hawawezi kujiajiri na wala hawawezi kuajiriwa. Kwa hiyo tunaomba katika Bajeti hii ya 2016/2017 katika mipangilio yao wafanye utaratibu wa kuanzisha VETA katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na napenda kuunga mkono hoja.