Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu.
Mimi naomba nijielekeze kwenye mambo yafuatayo; eneo la kwanza mara baada ya kupitia hotuba nzima nilikuwa anajaribu kuangalia eneo la uboreshaji wa miundombinu katika kuboresha kiwango cha elimu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa waziri atakapokuja kusimama hapa ni vizuri niungane na wale wenzangu waliotangulia kusema ni kwa kiasi gani wamejipanga kukamilisha ujenzi wa maabara ambao ulishaanza kipindi cha nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivi lengo letu ni kuona tunawezaje kwenda kutatua tatizo la walimu wa sayansi ambalo limekuwa ni tatizo kubwa na hata hapa tunapojadili upungufu wa walimu kwa sehemu kubwa tunaangalia upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna eneo la upungufu wa madarasa na nyumba za walimu naona mkazo mkubwa tumeelekeza zaidi kwenye kujenga madarasa na hii ni kwa sababu ya ongezeko la watoto ambao tumekuwa tumewapokea mara baada ya utekelezaji wa sera hii ya elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni lazima tuangalie mazingira ya walimu wetu, tuone ni namna gani Serikali imejielekeza kujenga nyumba za walimu za kutosha, ukienda kwenye jimbo la Nachingwea ambalo mimi nakaa sehemu kubwa ya walimu wetu hawana makazi ya kudumu yenye kueleweka hivyo hii inaweza ikashusha kiwango cha elimu katika kuboresha elimu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako nilifikiri tunapojadili elimu ni lazima tuangalie stahiki za walimu. Walimu wetu wamekuwa kwenye matatizo makubwa ya kudai haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wanapandishwa madaraja lakini hawalipwi pesa zao kwa wakati. Nafikiri umesikiliza na umeona kumbukumbu ya idadi ya watu ambao wanadai na kiasi ambacho Serikali kinadaiwa, kwa hiyo naomba deni hili ili tuweze kuwatia nguvu walimu ni lazima tuweke mkakati wa kuona kupitia bajeti hii tunawezaje kwenda kulipa madeni, ili walimu waweze kufanya kazi ambayo tumewaagiza watusaidie kutufanyia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia liko tatizo, iko tofauti ya upandishwaji wa madaraja kwa walimu ambao wameanza wakati mmoja. Walimu mathalani wanaanza mwaka mmoja lakini baada ya miaka mitatu pamoja na kwamba kuna OPRAS ambayo inapima utendaji wao wa kazi lakini bado kumekuwa na variation kubwa katika upandishaji wa madaraja sasa hili ni tatizo na walimu wetu wangependa kupata majibu wakati unahitimisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini kinapelekea utofauti huu mkubwa kwa watu ambao wameanza wakati mmoja kuwa katika viwango tofauti vya madaraja yao na hivyo kupelekea kupokea pesa kidogo tofauti na wale ambao wameanza nao kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia na mimi niungane mkono na wale wote ambao wameshangazwa na maamuzi yale ambayo kimsingi jana Mheshimiwa Waziri ameshayatolea ufafanuzi. Makosa sio wanafunzi, kilichofanywa na TCU lazima Serikali iende zaidi ya pale ambapo imefanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa wako watu wamechukuliwa hatua lakini ni lazima tujiulize tatizo mpaka tumelifuga tunachukua wanafunzi, tunawapa mikopo, lazima tujue tatizo ni kwa nani lazima hatua tungependa kuishauri iende zaidi ya hapo ili kuondoa uzembe ambao kimsingi tusingependa kuona vijana wetu wanapata shida na leo tunakuja kuwabebesha mzigo ambalo wao hawahusiki lakini kumbe kuna watu wamepewa dhamana na wameshindwa kusimamia dhamana yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la mikopo, mim naomba ni-declare interest, Mheshimiwa Waziri kati ya watu unaowatafuta kulipa hiyo mikopo nafikiri na mimi mwenywe ni mmojawapo. Nimeshangaa kidogo hapa lakini nafikiri tuna kazi ya kukusaidia kwamba unatafuta waliokopeshwa wako wapi. Bado unajaribu kuangalia board toka nimeajiriwa Serikalini kabla sijaacha kazi nimejaribu kufanya mawasiliano zaidi ya mara tatu, mara nne niweze kurejesha mikopo lakini sijaona hatua zozote. Sasa hili ni mapungufu ambayo yako ndani ya Bodi ya Mikopo, ni usimamizi mbovu ambao bado haujawekewa mikakati. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, leo hii ukiamua nusu ya Wabunge walioko hapa ndani wote ni wanufaika wa hii mikopo, lakini ni Wabunge wangapi wamelipwa hii mikopo nafikiri hakuna au ni wachache watakaokuwa wamefanya hivi, lakini sio makosa yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulipaji ule mmeweka gharama za kufidia kile ambacho mmekiita wenyewe kwamba ni sumbufu sijui ni nini. Hebu Mheshimiwa Waziri, tutakaa chini tujaribu kuweka utaratibu mzuri, lengo letu sisi kama Wabunge lazima tuwe mfano tulipe hii pesa ili vijana na watoto wetu waweze kupata na wao elimu kama ambavyo sisi tulipata wakati tunasoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kukuambia mimi niikuwa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuo kikuu pale DUCE mwaka 2008/2009. Najua kinachofanyika Bodi ya Mikopo ni nini, hebu tumia baadhi wa Wabunge wenzio ulikuwa nao hapa ndani tukusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko account mbili mbili zinafunguliwa na Bodi ya Mikopo, wako watu ambao wanapewa pesa lakini kimsingi pesa hii inarudi kwa watendaji wa bodi ya mikopo wenyewe. Sasa ni jambo ambalo linahitaji utulivu, linahitaji sasa wewe ushirikishe wadau mbalimbali ili tuweze kukupa taarifa ili tuweze kurejesha hizi pesa na vijana wetu waweze kusoma na hata wapiga kura nao waweze kunufaika na mikopo ambayo sisi tumenufaika nayo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulichangia ni suala la ukaguzi wa shule zetu. Leo hii nimeipitia bajeti nzima, najaribu kuangalia kiasi cha pesa ambacho kimeombwa kwa ajili ya matumizi ya kuboresha eneo la ukaguzi wa shule zetu, bado sijaona kiasi cha pesa cha kutosha.
Mheshimiwa Waziri na hili naomba nikwambie itakapofika wakati nitakamata mshahara wako, lazima uniambia ni kwa kiasi gani tumetenga pesa kwa ajili ya Idara hii ya Ukaguzi, leo hii ukaguzi haufanyi kazi yoyote ile, shule zetu hazikaguliwi, miaka mitano, miaka kumi shule zinafundisha, walimu wanafundisha lakini hakuna mtu anayeenda kutoa ushauri ni kwa sababu Idara ya Ukaguzi haina mafuta, Idara ya Ukaguzi hawana magari, Idara ya Ukaguzi hawana vitendea kazi na imefika wakati sasa wanatamani warudishe Halmashauri labda wanaweza kupata msaada kuliko kukaa huko ambako wamekaa na hawapati kiasi chochote cha pesa cha kufanya kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, nitaomba wakati unakuja kuhitimisha bajeti yako utuambie watu wa ukaguzi umewatengea kiasi gani cha pesa na sio kiasi cha bilioni mbili ambacho kitaenda kubaki mara baada ya matumizi mengine kwa kadri ulivyoomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la mitaala. Mtaala wetu unaotumiaka na kwa kasi tuliyonayo ya kuhitaji kujenga viwanda bado haiendani. Leo tunahitaji viwanda vya kutosha lakini hatuna wataalam ambao watakwenda kufanya kazi kwenye viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Elimu ya Kujitegemea (EK) mashuleni haifanyi kazi, leo hii tunategemea tuzalishe wasomi, tuzalishe watu ambao wataenda kuhudumia viwanda vyetu, lakini mitaala yetu inapishana. Leo hii ndani ya nchi moja wako watu wanatumia mitaala ya kutoka kwa Malkia ya Cambridge, kuna Watanzania wanaotumia mitaala ya kawaida sijui tunangeneza taifa la namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tumeamua kujipanga vizuri ni vizuri sasa tukaangalia namna ya kurekebisha mitaala yetu i-match na kile ambacho tunakwenda kukitengeneza ili tuweze kusaidia Taifa hili na Watanzania kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni wakati ule mitaala inapobadilika, vitabu vinavyotumika mashuleni navyo pia haviendani. Leo hii darasa la kwanza na darasa la pili vitabu wanavyovitumia na mitaala ni vitu viwili tofauti. Wachapaji wa vitabu wamekuwa wengi, vitabu hivi vinapishana kimaudhui, vitabu hivi vinapishana katika content ambazo tungetegemea zifundishe watu wa aina moja.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwa kazi ambayo umeifanya na unaendelea kuifanya ni vizuri maeneo haya yote tukayaweka vizuri ili tuweze kutengeneza kitu ambacho kinafanana na tutengeneze Watu ambao watakuwa sawa katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingineni ufundishaji wa TEHAMA katika shule zetu. Shule za wenzetu zile ambazo Watoto wenye pesa wanaweza kusomesha leo wanapata masomo ya sayansi, wanasoma computer, wanasoma vitu vingine, lakini ukienda katika shule zetu za kawaida wanapelekewa vitabu lakini practically hawasomi haya masomo kwa ajili ya kuwawezesha na wao kumudu teknolojia hii ya mawasiliano. Kwa hiyo Mheshimiwa katika bajeti yako ni vizuri, nimeona kwamba umetenga kwa jili ya ndugu zetu walemavu lakini bado kwa Watanzania wale walio wengi nao pia ni muhimu ukatueleza eneo hili tumejiweka na tumejipanga vipi ili tuweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo ningependa kuchangia ni NECTA kwenye suala la utoaji wa vyeti vya kuhitimu masomo. Hapa katikati tumeanza na division one mpaka division zero, lakini kuna watu wamekuja kutahiniwa kwa kupewa GPA, kuna watu walikuja wakapewa ile mpaka division five, leo hii waajiri wanapata shida wakati wa kuajiri kujua ni utaratibu gani unaweza ukatumika.
Naomba nitoe ushauri Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha utuambie, Wizara yako inaweza ikaweka utaratibu gani ili vitoke vyeti vya pamoja ambavyo vitasaidia kuondoa hii sintofahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.