Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika aya ya 185 ukurasa wa 136 Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa ili kuhakikisha haki za wazee zinalindwa, Wizara imeendelea kuratibu uanzishwaji wa Mabaraza ya Wazee katika ngazi mbalimbali za Halmashauri ambapo hadi kufikia Machi, 2019, jumla ya Mabaraza ya Wazee 9,083 yameanzishwa katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Mabaraza hayo yameanzishwa huku kukiwa hakuna Sheria ya Wazee nchini wala sheria ya kuwezesha kuanzishwa kwa Mabaraza hayo. Hivyo katika majumuisho Mheshimiwa Waziri aeleze ni lini Sheria ya Wazee italetwa Bungeni ambayo pamoja na mambo mengine itaeleza kuweka muundo na majukumu ya Mabaraza ya Wazee nchini. Aidha, sheria hiyo itawezesha kuundwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Wazee Nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, ipo hoja ya kutungwa kwa Sera ya Maendeleo ya Wanawake Nchini. Sera hiyo ifuatiwe na kutungwa Sheria ya Baraza la Wanawake la Taifa na kusimamiwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake nchini na wanawake wenyewe kupitia Baraza lao. Naomba kupata maelezo ya Serikali kuhusu hatua iliyofikia katika kuunda Mabaraza ya Watoto katika Jimbo la Kibamba. Haya yatawezesha watoto kujijenga ikiwemo Stadi za Uongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imewezesha kuandaliwa kwa kanuni za mashirika yasiyo ya kiserikali za mwaka 2018 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 609 la tarehe 19 Oktoba, 2018. Baadhi ya vifungu na vipengele vya kanuni hizo umekamilika na wadau yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali. Hivyo, Wizara ikae tena na mashirika yasiyo ya kiserikali kupitia vifungu na vipengele vilivyolalamikiwa na kufanya marekebisho. Aidha, Wizara iharakishe kuweka kanzidata ya mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuwa suala hili limechukua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Maendeleo ya Jamii na Vituo vya Ustawi wa Jamii unaweza kuwa na malengo makubwa kwenye maendeleo na ustawi wa jamii. Vituo hivyo vilianzishwa wakati ambapo mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ni tofauti na sasa. Hivyo Wizara ifanye tathmini ya Mitaa na mazingira ya vituo hivyo na kuja na mapendekezo ya maboresho kwa kuzingatia hali halisi iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala ya vituo hivyo ilenge kujibu changamoto zinazokabili jamii yetu kwa sasa na baadaye. Kadhalika Wizara itoe maelezo ya athari za fedha za maendeleo kutolewa kidogo katika Fungu la 53, Idara Kuu ya Maendeleo ambapo hadi kufikia mwezi Februari, 2019 kiasi cha shilingi bilioni 1.13 tu sawa na asilimia 23.0 tu ya fedha iliyotengwa kilikuwa kimepokelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina wajibu wa kuzisimamia kwa karibu mashirika na taasisi yaliyoko chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alikagua Bohari Kuu ya Dawa MSD na kubaini kuwa vifaa tiba ya shilingi bilioni 3.55 vilivyonunuliwa kwa mfumo wa manunuzi maalum vilivyorudishwa kutokana na kuzidi kiasi walichoagiza wateja. kutokuwa na sifa zilizotakiwa na wateja au kuzidi kiasi walichoagiza wateja. Baadhi ya vifaa tiba vilivyorudishwa vilikuwa vikikaribia kikomo cha muda. Hivyo, mfumo unapaswa kuboreshwa kuhakikisha kuwa hali kama hii haijirudii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia CAG alibaini katika mwaka 2017/2018 malipo ya shilingi bilioni 480 yalifanywa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa vituo vya tiba ya afya kwa wateja ambao hawakuchangia mfuko. Hali hii kama ni kweli ni hatari kwa mustakabali wa mfuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika, yapo madai kwamba malipo ya shilingi bilioni 13.99 yalifanyika kwa wanaodaiwa kuwa watoto wategemezi, lakini ukweli ni kuwa wamevuka miaka 18, hali ambayo inahitaji NHIF kuharakisha kuanzisha kanzidata ya umri wa wategemezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara itumie majumuisho kueleza sababu ya madeni yasiyolipika (bad debts) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka shilingi milioni 941.32 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 mpaka shilingi bilioni 1.44 kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013 na 2016 palifanyika uthamini (actual valuation) mara mbili kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Uthamini wa mwaka 2013 ulionyesha kwamba uendelevu bora na mfuko kwa maana ya mfuko kuanza kupata hasara ulikuwa mwaka 2040. Hata hivyo, uthamini wa mwaka 2016 ambao ripoti yake ilitolewa mwaka 2018 unaonyesha kwamba kiwango kimeshuka mpaka mwaka 2025. Hii ni kutokana na uwiano wa malipo ya huduma za afya kukua kila mwaka ukilinganisha na malipo ya Bima za Afya. Wizara inapaswa ieleze nini chanzo cha hali hiyo na ni ufumbuzi upi wa kukabiliana na hali hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizo zihusishe pia kuboresha mfumo wa Bima ya Afya kwa wastaafu kwa kuwekeza kiwango cha michango ya wanachama ili makato hayo yaje kusaidia malipo ya wanachama katika kipindi cha kustaafu kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuanzishwa kwa Manispaa mpya katika Jiji la Dar es Salaam, Hospitali za Mikoa za Amana, Mwananyamala na Temeke zinapaswa kuhudumia Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke mtawalia. Hivyo, kuna haja ya kuanzishwa kwa hospitali za mikoa kwa Manispaa mpya za Ubungo na Kibamba. Kwa upande wa Wilaya ya Ubungo Makao Makuu mapya ya Wilaya yanajengwa katika Kanda ya Kwembe eneo la Luguruni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia patakuwa na ujenzi wa mji mpya wa pembeni (satellite town) eneo la Luguruni. Hivyo, mji unapanuka kuelekea eneo la Kibamba. Kwa mantiki hiyo, napendekeza badala ya kupandisha hadhi Hospitali ya Wilaya ya Sinza, Palestina, mchakato uanze wa kujenga Hospitali ya Mkoa Kibamba na Kwembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa upande wa Sekta ya Afya, ina jukumu la kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kutekeleza afua mbalimbali. Kwa upande wa Hospitali ya Mloganzila, nimetembelea hospitali hiyo hivi karibuni na kubaini kwamba vipo vipimo ambavyo wagonjwa wanalazimika kwenda kuvipata kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika majumuisho, Mheshimiwa Waziri wa Afya alieleze Bunge, ni vipimo na huduma zipi ambazo wagonjwa wanalazimika kutoka Mloganzila au vipimo vyao kuchukuliwa kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ni mpango gani umewekwa wa kuhakikisha vipimo na huduma hizo zinapatikana katika Hospitali ya Mloganzila?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo niliyopita ni kwamba hata huduma ya CT-Scan wagonjwa kwa sasa wanalazimika kwenda kupata kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, utaratibu wa rufaa kutoka Hospitali za Mikoa ya Dar es Salaam zinapaswa kuboreshwa. Kwa sasa hauangalii umbali toka wagonjwa wanapoishi au wanaowahudumia wanapotoka katika kupanga kama mgonjwa husika apelekwe Muhimbili au Mloganzila. Hii inasababisha mathalan mgonjwa wa Ilala kupelekwa Mloganzila wakati ambapo ingekuwa ni rahisi zaidi kwa mgonjwa kama huyo kupelekwa Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika majumuisho, Wizara ieleze ni utaratibu gani umewekwa wa rufaa kuhakikisha kwamba wagonjwa na wanaowahudumia hawaendi umbali mrefu? Aidha, utaratibu wa rufaa uzingatie uwiano ili kuwe na urari wa idadi ya wagonjwa kati ya Muhimbili na Mloganzila kwa kuzingatia miundombinu, watumishi na huduma zilizopo katika hospitali tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo mbalimbali tarehe 3 Oktoba kuhusu uendeshaji wa Hospitali ya Mloganzila. Kati ya maelekezo aliyoyatoa ni pamoja na kuagiza wagonjwa kutoka Muhimbili kutohamishiwa katika Hospitali ya Mloganzila. Wakati Mheshimiwa Rais anatoa maagizo hayo, natambua kwamba wapo wagonjwa ambao tayari walikuwepo kwenye wodi za Mloganzila na pia Hospitali haikuwa na watumishi na huduma kwa kiwango kilichopo sasa. Matokeo ya maagizo hayo ni madai ya wagonjwa waliohamishiwa wengine kufariki kutokana na udhaifu wa huduma. Aidha, wapo wagonjwa ambao walihamishwa wakiwa katika hali mbaya na kupoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika majumuisho, Mheshimiwa Waziri aeleze ni wagonjwa wangapi walifariki katika kipindi hicho cha mpito na ni hatua gani zimeweza kuchukuliwa kupunguza idadi ya vifo vilivyotokea?

Mheshimiwa Naibu Spika, panakuwepo pia mgogoro wa mipaka baina ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kuhusu wapi hasa ipo Hospitali ya Mloganzila? Naomba katika majumuisho au katika mjadala, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na suala hili, atangaze kuwa Hospitali ya Mloganzila ipo katika Jili la Dar es Salaam Manispaa ya Ubungo.