Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nianze kwa kuungana na Taifa zima kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Dkt. Reginald Mengi kilichotikisa Taifa zima. Dkt. Mengi amefanya mengi katika Taifa hili, hivyo tumuenzi kwa kuendeleza mema na wema wake. Aidha, kifo chake kimetokea kikifuatana na cha kijana mahiri Ruge Mutahaba na Ephraim Kibonde. Ni pigo kubwa pia jana tu tumempoteza Mtanzania mwingine Prof. Robert Mabele kilichotokea Hospitali ya Mloganzila. Profesa Mabele amewafundisha wengi na hata Waziri wetu wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango ni mwanafunzi wake. Tuwaombee wote pumziko la milele.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika hoja ya leo ya afya. Nami naungana na wengi kupongeza kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na msaidizi wake Mheshimiwa Dkt. Ndugulile. Wote wametembelea Wilaya ya Muleba na kuona maendeleo na changamoto ambazo naomba niziorodheshe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua tuna Hospitali Teule ya Wilaya ya Rubya, aliitembelea. Tatizo ni kwamba utaratibu wa PPP katika kutoa huduma unaweza kuleta mkanganyiko ikiwa utaratibu wa kulinda uwezo uliojengwa hautawekwa bayana. Hospitali Teule ya Rubya imepoteza wafanyakazi muhimu na vifaa, wamehamishwa. Kwa hiyo, hakuna degree holder tena katika ukurasa wa tatu utaona hakuna maabara wala generator.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mashine ya viral load imehamishwa na kwenda Bukoba. Hii inadhoofisha uwezo wa hospitali teule kuhudumia wananchi takriban 700,000 katika Wilaya. Upanuzi wa hospitali mpya usimaanishe kudhoofisha zile za zamani. Naomba kujua mkakati wa kuepusha jambo hili, tusipoteze uwezo uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rubya pia kitengo chake cha meno hakitoshi kabisa, ni kama hakipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile uboreshaji wa vituo vya afya viwili; Kaigara na Kimeya tumeshuhudia na sasa upasuaji unaendelea. Hata hivyo, bado kuna upungufu wa maboma. Ninaomba jambo hili liangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ujenzi wa zahanati kadhaa kwa nguvu za wananchi unaendelea karibu katika kata zote. Tatizo ni fedha za kununua vifaa vya viwandani; saruji, nondo, vioo na kadhalika. Naomba Wizara iangalie jinsi gani ya kupata fedha kukamilisha ujenzi wa zahanati hizo ikiwemo zifuatazo: Buhangaza, Buganguzi, Kishando – Muleba, Burunguna, Muzinga – Nshamba, Kashanda – Kubirizi, Kasindaga – Kata Kamombi – Kangazo – Nyakabango.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaona kwamba mahitaji ni makubwa sana. Bila Wizara ya Afya na TAMISEMI kutuwekea nguvu itakuwa vigumu kumaliza zahanati hizi. Eneo linalohudumiwa ni kubwa. Sina budi kuwashukuru TANAPA kutusaidia katika ujenzi wa zahanati kisiwa cha Ikuza. Ni Ukombozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy kutusaida kupata ambulance ya Hospitali ya Rubya. Pia, tunazo kwenye vituo vyetu vya afya, lakini wakati mwingine ambulance inasimama kwa sababu ya kukosa dereva. Ni suala la TAMISEMI, lakini ninaamini Wizara ya Afya ni mdau mkubwa katika jambo hili. Jamani hospitali kusimama kwa sababu tu hakuna dereva! Kama haupo utaratibu, tunaomba mwongozo utolewe wa kumewezesha Mkurugenzi kuhakikisha kamwe ambulance haisimami kwa kukosa dereva.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ajira kwa Madaktari na Wauguzi. Ni jambo la kushangaza kuwa baadhi ya Madaktari wanahitimu lakini wanahangaika kutafuta ajira na wengine kukata tamaa na kwenda nje ya nchi. Ninaomba kujua, hivi sasa tuna Madaktari wangapi ambao bado hawajaajiriwa, huku uhaba wa Madaktrai na Wauguzi mbalimbali wakiwa hawatoshi katika hospitali zetu. Naomba mkakati wa manpower planning kwa Sekta hii uwekwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mloganzila imekamilika na ninapongeza juhudi za Awamu ya Nne zilizoijenga, lakini naamini ni muhimu sasa kuwa na mpango wa kujenga hospitali town. Hivi sasa madaktari hawana makazi na sijui kama dharura ikitokea itakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, MSD ya Kanda ya Ziwa Magharibi ipo Muleba. Mheshimiwa Waziri anajua kulikuwepo na tetesi kwamba itahamishwa kwenda Bukoba. Mheshimiwa Waziri Dkt. Ndugulile alitembelea MSD hiyo na kuona athari za kuihamisha. Aidha, mantiki ya kuiweka Muleba ni kwa kuwa ni katikati ya eneo la huduma; Kagera, Geita na Kigoma Kaskazini. Naomba hofu hii ya kuhamisha MSD ya Kanda iondolewe ili maendeleo yaliyopangwa yaendelee. Eneo la kutosha ekari tano zimetolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima ya Afya ni mkombozi na tunapongeza maendeleo yake. Changamoto zinazojitokeza ni ngazi ya referral system. Inaonekana hakuna manual ya recommended drugs kwa Hospitali za Rufaa. Hicho hicho cha hospitali za kawaida ndicho kinatumika Hospitali za Rufaa. Hii ina ukakasi, kwani Hospitali za Rufaa zina utaalamu zaidi na wanaweza kukubadilishia dawa. Sasa kuna Wakaguzi wa NHIF na uthibiti wa abuse, ni muhimu kwa sababu wakaguzi hao wanaweza wasikubaliane na daktari bingwa, inaleta ukakasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nilimwomba Mheshimiwa Waziri Ummy atambue Hospitali ya Mkoa ya Bukoba haikidhi viwango vya referral kutoka Hospitali Teule ya Rubya. Kwa hiyo, Bima ya Mkoa wa Kagera referral iwe Bugando, hata kwa Bima ya jamii, yaani zahanati - wilaya - Bugando hadi Rubya Hospitali ya Mkoa itakapoboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri huduma za saratani ziendelee kuboreshwa. Tunapongeza Ocean Road na Bugando kwa huduma zao lakini hazitoshi. Pia tuwekeze katika kuzuia kuenea kwa saratani, tupime afya, tusingojee mionzi. Prevention is better than cure. Inahitaji Wizara kupiga kampeni ya rollback cancer.