Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hotuba iliyoko mbele ya Bunge letu Tukufu. Kwanza nitoe pongezi za dhati kwa Waziri mwenye dhamana pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa na nzuri sana wanayoifanya. Pia pongezi hizi ziende kwa Watendaji wa Wizara na Mashirika yote yaliyoko chini ya Wizara hii kwa maana kwamba tunajua bila wao utekelezaji wa Ilani ya Chama ni jambo ambalo ni gumu. Kwa hiyo tunatoa pongezi na jukumu letu sasa ni kushauri kwa yale maeneo ambayo tunaona kwamba yanaweza yakawasaidia kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee kabisa naomba kwanza nitoe pongezi za dhati kwa Meneja wa TANROAD Mkoa wa Tanga, Injiania Ndumbaro kwa kazi kubwa sana anayoifanya. Mkoa wa Tanga hususan Wilaya ya Lushoto, Korogwe na Muheza ni za milima, kwa hiyo mara nyingi sana barabara zinasumbua hasa nyakati za mvua, lakini injinia huyo amekuwa halali na kuhakikisha kwamba barabara hizi wakati wote zinapitika. Mvua za mwaka jana zilileta mafuriko makubwa sana katika eneo la Lukozi lakini ndani ya kipindi kifupi aliweza kutujengea daraja pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, lakini pia nitoe masikitiko kidogo kwa watendaji wa TANROAD hasa ngazi ya Taifa kwa sababu barabara yetu ya kutoka Mlalo kwenda Lushoto, lakini pia kutoka Mlalo kwenda Mng’aro hadi Maramba kule Mkinga kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo tumekuwa tukipanga katika vipaumbele vyetu kwenye RCC kwamba ifanyiwe upembuzi yakinifu, lakini pia ifanyiwe na usanifu wa kina. Mara zote inapofika kwenye meza ya Watendaji wa Kitaifa kwa maana ya Injinia Mfugale, walikuwa hawaipangii fedha. Kwa hiyo niombe sana kwamba barabara hii ni muhimu kwa sababu inaelekeza eneo muhimu sana la kiuchumi hasa kwa mazao ya mbogamboga na matunda ambao ndiyo uzalishaji mkubwa katika eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba nitoe mchango wangu katika eneo zima la usafirishaji hasa usafirishaji wa anga. Kwanza kabisa kipekee nimpongeze sana Mtendaji Mkuu wa ATCL ndugu yangu Ladislaus Matindi amekuwa akifanya kazi kubwa sana na kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba shirika hili linasimama. Pongezi hizi pia zimuendee Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ununuzi wa ndege hizi nane ambazo kwa kweli zinafanya vizuri katika soko la ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataraji kuiona ikifanya vizuri zaidi ATCL katika soko la nje kwa maana kushiriki katika ushindani. Tumeona hapa yapo maeneo kadhaa wameanzisha safari lakini bado tunataka kuiona ATCL ikifanya kazi vizuri, itafanyaje vizuri; kwanza ni lazima tusiiweke ATCL kwenye mikono ya Wizara peke yake, ATCL lazima tuichukue kama ni mradi wa kimkakati wa nchi, tuone kama nchi tunataka kwenda wapi na shirika hili la ndege. Utaona wenzetu wa mashirika kama ya Turkish ya Uturuki, Rwanda Air na Qatar ya Doha kule wameyaweka kama ya kimkakati ni ya nchi nzima inayabeba haya mashirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukifika pale Kigali leo, wanaitangaza Kigali kama kituo cha kibiashara cha mikutano, kwa hiyo nchi mbalimbali tunaona kabisa katika forum mbalimbali za kimataifa wanafanya mikutano Kigali lakini kwa kupitia Rwanda Air. Ukifika Doha pale Qatar ni mji mkubwa sana wa kibiashara sasa hivi, lakini umechagizwa kabisa na uwepo wa Qatar Air, lakini pia ukifika kule Istanbul, Uturuki utaona kabisa sasa hivi imekuwa ni kituo kikubwa cha kibiashara kati ya Asia na Ulaya kupitia hili Shirika la Ndege la Turkish.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanafanikiwa tu kwa sababu wenzetu hawa wameweza kutoa ruzuku kwenye haya mashirika kwa sababu yamechukuliwa kama ni miradi ya kimkakati ya nchi na hayajaachiwa kwenye Wizara kama ambavyo tunafanya sisi. Utaona kwamba gharama kama za landing na navigation charges ziko chini au wamezitoa kabisa kwamba yanaruhusu sasa biashara kufanyika kwa wepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ATCL ni kweli wamenunua ndege nane, lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza hawana hata ndege moja ya kubeba mizigo. Sasa tunapozungumza Tanzania ya viwanda ambayo pia tuna mazao ambayo tunataka tuyapeleke kwenye masoko ya kimataifa, bila kuwa na ndege za kubeba mizigo jambo hili litakuwa ni gumu. Kwa mfano, tu hapa tuna viwanda zaidi ya kumi na nne katika Kanda ya Ziwa ambavyo vinachakata minofu ya samaki, lakini kwa masikitiko makubwa viwanda vyote hivi vinasafirisha minofu kwenda uwanja wa Nairobi ama uwanja wa Entebbe kiasi kwamba sisi hatuonekani kama tuna-export hii samaki kutoka katika eneo letu. Sababu kubwa ni kwamba hatuna viwanja, hatuna ndege za kubeba mizingo lakini pia viwanja vyetu vya ndege gharama za kutua ndege za mizigo ni kubwa sana kiasi ndege hazivutiki kuja kutua katika viwanja vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona hata juzi hapa Waheshimiwa Wabunge wanalalamika kwamba maparachichi yanapelekwa Kenya halafu Kenya ndiyo wanayapeleka kwenda Uchina. Hili tunaweza tu tukaliepuka kama tutakuwa na gharama rafiki kwenye viwanja vyetu, lakini pia tutakuwa na ndege zetu ambazo ni za mizigo, ili sasa hata hivi viwanja tunavyoendelea kupanua huko Songwe, huko Mwanza na kadhalika viweze kutumika kama sehemu mojawapo ya kuchochea uchumi wa nchi yetu na ndiyo maana katika hatua ya awali nilizungumza kwamba bila kuifanya ATCL kuwa ni mkakati wa kitaifa tukaiacha peke yake kwenye Wizara hii moja, ile tija ambayo tunaikusudia itakuwa haijafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza, ni suala zima la kupanua Bandari ya Tanga. Tumeona katika kitabu, ukurasa wa 117, kuna upanuzi wa Bandani ya Tanga. Hii ni bandari muhimu sana kimkakati na ndiyo maana nadhani hata Wakoloni wa Kijerumani walianza kujenga bandari Tanga kabla ya maeneo mengine na hata reli ya Tanga nadhani ndiyo reli ya kwanza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kwamba ni muhimu sana bandari hii iboreshwe kwa wakati. Pia itasaidia kwa sabau sasa hivi tumeona hata wenzetu Wazanzibar kuna baadhi ya bidhaa wanazipitishia Mombasa lakini tukiboresha Bandari ya Tanga kutakuwa na uwezo mkubwa wa kupitisha mizigo hata ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni ukarabati wa reli ya Tanga – Moshi - Arusha - Musoma. Hili nalo tunamshukuru sana ndugu yetu Kadogosa, jitihada zimeanza lakini jitihada hizi zisiishie kufufua reli hii ya zamani. Tunatamani na sisi pia tuone SGR ikiwa katika maeneo haya, inachukua mkondo huo wa reli za kimataifa ili kuboresha sasa huduma za usafiri na kuunganisha usafiri wa reli na usafiri huu wa majini. Hii ni kwa sababu kuna mizigo mingi ambayo inaenda nchi jirani ikiwemo Uganda na Kenya ikiweza kupita katika bandari hii na kupitia reli kwenda mpaka Musoma inaweza ikasaidia hata sisi kama nchi pia kuwa na mkakati wa kushindana katika soko la Sudani Kusini kwa kupitia Bandari ya Tanga na reli hii ya kwenda Moshi – Arusha - Musoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho lakini siyo kwa umuhimu ni suala zima la mawasiliano. Ndugu yangu Mheshimiwa Eng. Nditiye tumezungumza mara kadhaa kwamba kuna maeneo katika Jimbo la Mlalo bado mawasiliano ya simu hayapatikani. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ihakikishe yale maeneo mahsusi niliyowaandikia yanafikiwa na huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)