Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii lakini niseme tu kwamba naunga mkono bajeti ya Wizara hii nyeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu. Nimpongeze sana Engineer Mfugale kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Tunaweza tukamuita huyu ni gwiji wa barabara na madaraja ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwapongeze sana ma-Engineer wa mikoa yote nchini kwa sababu tumekuwa tukiona Mheshimiwa Rais akipita huko na huko akifungua barabara au akiweka mawe ya msingi. Bila hawa ma- Engineer nafikiri kazi hii isingekuwa inafanyika vizuri. Kwa hiyo, niwapongeze sana sana Mameneja wa TANROADS wa Mikoa yote Tanzania kwa kazi nzuri mnayofanya chini ya gwiji wa barabara ndugu Engineer Mfugale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Engineer wa Mkoa wangu, Engineer Luviga kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Nimpongeze pia Kaimu Engineer wa Mkoa wa Dar es Salaam Julius Ngusa kwa kazi nzuri anazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la kwanza linahusiana na ATCL. Tumwombe CEO wa ATCL, ikiwezekana, tumeshaleta maombi upande wa kwako, tuwe na ndege ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza na Mwanza kuja Dodoma itasaidia sana Wabunge na watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 28 Januari, 2016 niliuliza swali humu ndani na likajibiwa na Serikali. Swali langu lilikuwa linasema hivi, je, ni lini barabara ya Magu – Bukwimba – Ngudu – Hungumalwa itajengwa kwa kiwango cha lami? Majibu ya Serikali yanasema: “Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016, Serikali ilitenga jumla ya Sh.200,000,000 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara yenye urefu wa kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea. Baada ya kukamilika kwa usanifu na gharama za mradi huu kujulikana, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa 2014/2015, 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018, 2018/2019 leo ni 2019/2020. Nataka
nipate majibu ya Serikali, nimeona humu mmetenga Sh.440,000,000 kwa kilometa 10 sijui ni za nini, ni za changarawe au za nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Eng. Mfugale najua kabisa barabara hii unaifahamu vizuri sana umuhimu wake. Ili Mji wa Ngudu ufunguke, barabara hii inakwenda kuunga ile barabara ya lami ya kutokea Musoma, barabara hii ukiifungua inakwenda kuunga kwenye barabara inayotokea Mwanza kwenda Shinyanga. Kwa kufanya hivyo, utakuwa unapunguza msongamano wa mabasi ya kwenda Mwanza, mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Musoma badala yake yanapitia Hungumalwa kwenda Mara, ili tupunguze huu msongamano barabara hii ni muhimu. Mji huu wa Ngudu umedumaa kwa sababu hakuna miundombinu ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Mfugale kwa utendaji wako mzuri mpaka unapewa daraja la flyover (Mfugale flyover) sifa zote hizo, unashindwa kweli ka barabara haka ka kilometa 74, kweli? Bwana Mfugale, bee kamwene bee bwana Mfugale, kilometa 74. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri barabara hii iko kwenye Ilani ya Chama chetu. Barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais alipokuja Ngudu wakati wa kampeni. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Ngudu, nafikiri wewe bwana Mfugali ulikuwepo, kama hukuwepo basi msimamizi wako alikuwepo, Mheshimiwa Rais aliahidi lakini wakati huo Rais wetu wa sasa ndiyo alikuwa Waziri wa Ujenzi. Sasa wazee na mimi mzee humu ndani hata ka heshima kadogo tu bwana Mfugale? Barabara hii ni muhimu sana naomba muishughulikie na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmefungua…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndassa, unatakiwa unitazame mimi sio Mfugale. (Kicheko)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nimekuona. Ni macho tu na unajua macho yana degree 180. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Engineer Kamwelwe, nilikuja ofisini kwako na kama unakumbuka ukaniambia niandike barua pale Water Front. Nikaandika barua na nikakuletea ya barabara hiyo, sasa leo rafiki yangu Mheshimiwa Engineer Kamwelwe unaniwekea kilometa 10 za changarawe badala ya lami wakati barabara hii imeshafanyiwa upembuzi wa kina? Nikuombe sana Mheshimiwa Kamwelwe na labda sasa nimuombe Mheshimiwa Rais barabara hii wewe unaifahamu vizuri zaidi…
WABUNGE FULANI: Hayupo humu.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Nyamazeni ninyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Rais, barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Kwimba. Barabara hii ikitengenezwa itafungua milango ya uchumi kwenye Wilaya ya Kwimba hasa Ngudu. Barabara hii ni muhimu sana, nikuombe sana Mheshimiwa Kamwelwe, utakaposimama kuja kihitimisha nipate majibu hasa kwa barabara hii muhimu kwa Wilaya ya Kwimba. Barabara hii iko kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuangalie uwezekano, Waheshimiwa wakubwa kabisa wa kujenga barabara ya kutoka Fulo – Mantale – Nyambiti Junction. Barabara hii ni muhimu sana inajumuisha Wabunge watatu kwa maana ya Majimbo matatu. Jimbo la Misungwi, Sumve na Kwimba, barabara hii ni muhimu sana ikitengenezwa kwa kiwango cha lami. Nimeshaleta mapendekezo kwenu muangalie angalau muiingize kwa mwaka ujao wa fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu inatumia pesa nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, barabara ya kutoka Mwanza kwenda Shinyanga border yenye urefu wa kilometa 102 imekuwa ikitumia pesa nyingi sana za matengenezo ya mara kwa mara. Waziri anafahamu na nafikiri Engineer wa mkoa anafahamu na Engineer wetu anafahamu kwa nini barabara hiyo isifumuliwe angalau hata kilometa 10 za kwanza baadaye kilometa 10…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)