Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nichangie Wizara hii muhimu na Wizara ambayo imepelekewa fedha nyingi kuliko Wizara zote katika Serikali hii ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka aliyotujalia ya kuweza kupatikana kwa ndugu yetu bwana Mdude Nyangari. Akiwa hai japo amejeruhiwa vibaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja kabla sijaanza kuchangia, jana ilizunguka taarifa ambayo inasemekana imetoka Ikulu, ikionyesha kwamba Mheshimiwa Rais anasikitishwa sana na vitendo vya utekaji na upoteaji wa watu vinavyoendelea katika nchi hii, na akasema kwamba vitendo hivi vinaichafua nchi na ameliagiza jeshi la polisi kufanyia kazi na ataunda tume na ikibidi…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Makamba jielekeze kwenye hoja, ambayo ko mbele yako.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye hoja. Ghafla bini vuu tukapata taarifa kutoka Ikulu ikikanusha habari hiyo…
MWENYEKITI: Makamba, jielekeze kwenye hoja ambayo iko mbele yako.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kukanusha taarifa inayotoka Ikulu ni taarifa nzuri sana…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Makamba nitakukalisha sasa hivi, jielekeze kwenye hoja ambayo ipo, kwa mujibu wa kanuni, jielekeze kwenye hoja ambayo iko mbele yako.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Nchi yetu amefanya kazi kubwa sana katika kusimamia Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano, na mtizamo wake Mheshimiwa Rais, katika kusimamia suala la ununuzi wa ndege, Mheshimiwa Rais amehamishia Mamlaka ya Usimamizi wa Ndege zote za Serikali katika Ofisi ya Rais. Jambo hili, katika miradi mikubwa katika nchi hii, katika miradi mikubwa, mradi wa ndege ni mmoja kati ya miradi mitatu mikubwa iliyoanzishwa katika hii nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vote 20, haikaguliwi na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Fedha za wananchi ambazo ndizo nyingi zinatumika katika mradi huu, zimehamishiwa Ofisi ya Rais, hazikaguliwi na Mkaguzi, na siyo tu hivyo, amesoma Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani hapa, anasema katika sehemu ambayo tunaonyesha hasara kubwa katika Taifa hili ni katika Mamlaka ya Ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja kubwa sana ya kuliangalia suala hili kwa sababu kuna kioja kimoja kiliwahi kutokea kwenye Bunge moja nilikuwa nasoma kwenye mitandao, wakati mwingine tunaweza tukawa tunapiga makofi kumbe tumetukanwa. Yule Mbunge alisimama akasema, nusu ya Wabunge walioko humu ndani ni wajinga! Watu wakasema afute kauli, afute kauli, akafuta kauli akasema, nusu ya Wabunge waliomo siyo wajinga! Wakapiga makofi! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunaweza kuwa tunalitukanisha Bunge letu bila sisi kujua kutokana na matendo yanayoendelea. Kinachoonekana, katika suala la kuhamisha mamlaka, anayenunua ndege ni Ofisi ya Rais, akinunua nzima, akinunua mbovu ni juu yake. Halafu huyo huyo ndiyo anapitisha bajeti ya matengenezo ya ndege, iwe labda alinunua nzima au mbovu! (Makofu)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akitoka hapo huyo huyo ndiyo ananunua mafuta kwa ajili ya hizo ndege bila kujali fuel consumption ya ndege kama ilizingatiwa wakati wa manunuzi. Ipo haja ya Bunge kujitafakali kwa nini tumetoa mamlaka ya usimamizi wa ndege za Serikali, kutoka Wizara ya Ujenzi, tukapeleka Ofisi ya Rais, ipo haja ya kujitafakari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye matumizi ya wakandarasi, ipo dhana potofu ambayo Serikali ya Chama cha Mapinduzi inawaaminisha wananchi kwamba wakandarasi wazawa ndiyo ambao wanapewa kazi nyingi. Nataka nilieleze Taifa leo hii, ni kweli asilimia 85 ya wandarasi wa kitanzania ndiyo wanaopewa kazi, lakini ile asilimia 15 ya wakandarasi kutoka nje, ndiyo wanaolipwa zaidi ya asilimia 85 ya fedha zinazokwenda kwenye Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuone ile asilimia kubwa inayopewa, ndiyo inayokwenda nje ya nchi, hao wakandarasi wanaoitwa wazawa, wanapewa kazi za kawaida ambazo asilimia 15 tu ya bajeti ndiyo inatumika kuwalipa. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Wanapewa kuchimba mitaro.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa…
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Katika Mamlaka ya Hali ya Hewa…
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, anapotosha.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Si una muda wa kujibu baba!
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MWENYEKITIl: Taarifa, taarifa, taarifa! Mheshimiwa Heche, Mheshimiwa Heche kaa chini, Heche kaa chini.
MHE. JOHN W. HECHE: Is wrong!
MWENYEKITI: That is not wrong, kaa chini!
MHE. JOHN W. HECHE: Is wrong!
MWENYEKITI: You are wrong kaa chini!
MHE. JOHN W. HECHE: Siyo utaratibu!
MWENYEKITI: Sikiliza Mheshimiwa Heche, Bunge linaendeshwa na taratibu zake, huwezi ukaamuka tu na mkali yako ukasimama ukasema unavyotaka, kwanza sijakuruhusu usimame. No! No! anaweza kwa any time aka-inter, aka nini, tulia. Mheshimiwa Waziri!
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kitabu cha bajeti, Wizara inanunua ndege na utaona hapa katika ukurasa wa 467, kwa hiyo, nimelazimika kusimama kwa sababu dada yangu Mheshimiwa Makamba anatupotosha, analipotosha Bunge lako.
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Makamba!
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Waziri una nafasi ya kujibu, nafasi yako itakuja mwishoni, na mimi nafanya hivi kuisaidia Wizara yako, kwa sababu, Mheshimiwa Waziri, suala la ununuzi wa ndege zote zilizonunuliwa leo hii, hakuna performance inayoonekana katika Taifa hili zaidi ya hasara. Ukitetea kwamba wewe ndiye unayenunua utakuwa answerable at the end of the day na ninasikia vibaya sana kwa sababu wewe ni baba yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee habari ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, wiki iliyopita, Waziri alikuja hapa akasema kwamba kuna hali ya taharuki katika hali ya hewa, Lindi na Mtwara watapatwa na matatizo makubwa sana, tukasema sawa. Hii mamlaka ya hali ya hewa, ku-bate kuhusu mamalaka ya hali ya hewa ni afadhari u-bate game ya Yanga na Lipuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuriko na madhara makubwa yamekwanda kutokea Shinyanga, Kahama, Mwanza, badala ya Lindi na Mtwara. Nataka kuhoji, hivi hawa watu wa mamlaka ya hali ya hewa ni wapiga lamri au ni professional people wamewekwa kwa ajili ya kutusaidia! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nihoji tu kuhusu hao watu, na kwa nini hawawajibishwi? Wanaleta taharuki kwenye hii nchi na wanamwangusha Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, mama anajitahidi kweli kuongea kwa ajili ya Chama cha Mapinduzi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu suala la ucheleweshaji wa mizigo, I do no, shida ya mitandao. Tulitenga fedha nyingi sana hapa tena mkaja kwa mbwembwe kuhusu TTCL, leo hii Mheshimiwa Waziri haoni hata aibu kusema tumewapa VIATEL, anajibu maswali ya Wabunge hapa, ananadi makampuni ya nje, hivi hii TTCL imeshindwa kufanya kazi au kuna tatizo gani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mmeshindwa, si mtoe tu tamko kwamba, jamani na makampuni mengine yaje ili waendelee kufanya kazi. Mheshimiwa Waziri, siyo uzalendo, siyo uzalendo kuja kujisifia hapa kwamba umeimarisha au umesambaza mitandao ya makampuni ya nje, wakati TTCL tumekupa fedha hapa na umeshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee kwa haraka kuhusu Mamlaka ya Bandari. Tunafahamu kuna kazi kubwa sana inafanyika na niwapongeze wafanyakazi. Katika eneo lolote la kazi, maslahi ya wafanyakazi yanakuja kwanza! Kinachotokea mamlaka ya bandari, yule Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari anawafanyisha watu kazi pale mpaka saa sita, saa saba za usiku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wabunge hapa maslahi yetu huwa yanakuja kwanza, niseme, mtu anatoka kazini saa sita za usiku, kesho asubuhi saa 12 kamili anatakiwa aripiti ofisini, hatuwezi kufanya kazi kwa kukiuka sheria za kazi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, just kwa sababu tunalazimisha mipango ambayo tuliipanga bila kufanya consultation iweze kufanikiwa. Niombe sana, Mawaziri, muangalie sekta zenu mnazofanya kazi, kufanya kazi sema punda afe mzigo ufike, Tanzania tunafanya kazi kwa kuangalia kwanza maslahi ya wafanyakazi na ndiyo maana juzi hapa, jambo la kwanza Kambi Rasmi ya Upinzani ilisisitiza ni kuhusu maslahi na mishahara ya wafanyakazi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo la mwisho, kuhusiana na suala la mitandao, tena nilikuwa nimesahau jambo la muhimu sana. Kule kwetu Kahama, zipo kata ambazo ndiyo zinaongoza kwa uzalishaji, wale watu hawawezi kutoka kata moja kwenda nyingine kwa sababu hakuna barabara, hawawezi kutoka kata moja kwenda kata nyingine kwa sababu hakuna mawasiliano ya simu, hawawezi kutoka kata moja kwenda kata nyingine kwa sababu tumewatelekeza wamekuwa kama wanaishi watu walioko kwenye ujima. Nitazitaja kata chache tu ambazo wao wamenituma kwa dhati nifikishe suala hili kwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Kata ya Wendere, tunayo Kata ya Ngogwa, Kata ya Ubagwe, Kata ya Nyandekwa na Kata ya Uleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako, ningemuomba Mheshimiwa Waziri, akija kuhitimisha hapa leo, awaahidi wananchi hawa, ambao Mheshimiwa Rais anajinadi kwamba wasukuma ndiyo wamempigia kura. Hivi leo ni mwaka 2019, ni lini mtawatengenezea barabara, ni lini mtawapelekea mawasiliano ya simu, maana wale watu wanashida zote katika nchi hii, na mimi, yaani, ningekuwa siyo mpenzi wa watanzania ningesema afadhali msipeleke ili tuendelee kuchaguliwa chama cha CHADEMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, kwa sababu nawapenda watanzania wenzangu, naomba nisisitize, Mheshimiwa Waziri, wapelekee wale watu huduma! Waonee huruma wanaishi maisha ya kijima.
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)