Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu kwa hotuba nzuri sana aliyoitoa leo asubuhi na yenye kuleta matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, natoa pongezi nyingi sana kwa chama chetu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna ambavyo wameweza kutekeleza Ilani katika Jimbo langu la Mafia. Kwa uchache tu nimeangalia kwenye kitabu humu, Mheshimiwa Waziri anasema gati la Nyamisati limekamilika kwa asilimia 32, lakini nilikuwa pale wiki iliyopita, lile gati limeshakamilika kwa asilimia zaidi ya 90 na naamini mwezi ujao atalifungua. Kwa hiyo, napongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Jemedari Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kile kivuko ambacho tuliahidiwa mwaka jana hapa, kivuko cha kati ya Nyamisati na Kilindoni; nimekiona kwenye kitabu humu pamoja na matengenezo ya maegesho ya Nyamisati na Kilindoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja ambalo nililizungumza mwaka jana kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara hii. Mwaka jana hapa zilitengwa shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kivuko cha Nyamisati – Kilindoni bilioni tatu na bilioni nne kwa ajili ya maegesho upande wa Nyamisati na milioni 400 maegesho upande wa Kilindoni. Nilisema mwaka jana hapa, alikuwa Waziri Mheshimiwa Mbarawa, nikamwambia Mheshimiwa Waziri wanaokuangusha ni watu wako wa TEMESA, kuna tatizo TEMESA. Mwaka jana zimetengwa bilioni 3.8, leo tunamaliza bajeti hii hazijatumika kwa sababu sijui michakato imefanyaje, sijui mkandarasi kafanya vipi, imekwenda huko tenda imekosewa, imefutwa tumeanza upya. Labda hilo inaweza tukawa tumeelewa, vipi kuhusu maegesho milioni 400 Nyamisati na milioni 400 Kilindoni na yenyewe nayo tatizo ni nini mpaka mwaka umekwisha fedha zinatengwa tena kwa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa mwakani turudi tena hapa tukute wanatenga pesa nyingine kwa ajili ya kivuko na maegesho ya Nyamisati na Kilindoni. Mheshimiwa Waziri nikasema tatizo naliona lipo TEMESA, nimewaona wameandika humu kwamba wanashughulikia maegesho hayo, maegesho ya milioni 400 Kilindoni, maegesho ya milioni 400 Nyamisati, mwaka mzima? Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, watu wake waTEMESA wanamwangusha na nilisema kwenye hotuba kama hii mwaka jana. Sasa nisingependa turudi mwakani tuzungumzie habari hii tena ya kivuko na maegesho ya Nyamisati na Kilindoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kivuko hiki ambacho kinatengenezwa pale na TEMESA. Kila tukiendelea kufuatilia pale unaambiwa sijui mkataba upo kwa Mwanasheria Mkuu, mara unaambiwa sijui tenda ile ilifutwa, mara unaambiwa subiri kuna vifaa vimeagizwa kutoka nje vinahitaji exemption, tatizo lipo kwa Waziri wa Fedha. Sasa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hotuba yake atuambie na atuhakikishie watu wa Mafia kivuko hiki kinatengenezwa na kipo katika hatua gani, maana yake hii habari ya kusema ya kwamba tunasubiri exemption kutoka kwa Waziri wa Fedha, ukimuuliza Waziri wa Fedha anasema jambo hilo halijui. Ukienda ukizungumzia baadaye unakuja unaambiwa aah kuna tatizo kwenye procurement kule wamefuta tenda yenyewe; sasa tushike lipi? Sasa ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie pale na watu wa TEMESA. I wish watu wa TEMESA wangejua tabu, dhiki, mashaka na adhabu wanayoipata watu wa Mafia kusafiri kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza kuna watu zaidi ya wiki nzima wako pale, vyombo vile vya mbao vimechoka havina uwezo wa kubeba watu wengi, watu wamekaa pale stranded wiki nzima, halafu mtu anatoa majibu mepesi tu kwamba sijui tenda imefanya hivi, mkataba sijui upo kwa Mwanasheria Mkuu, sijui Wizara ya Fedha haijatoa exemption; ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up atuambie kwa mapana yake kivuko hiki sasa kitakuwa tayari lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni barabara; barabara ya Rasimkumbi mpaka Kilindoni kilometa 45. Tulinong’ona asubuhi akaniambia kwamba hiyo hukuiona humo lakini msiwe na wasiwasi. Naomba sana na nilizungumza zaidi ya mara tatu hapa, ile barabara tatizo kubwa Mafia ni kisiwa periodical maintenance inabidi utafute udongo, udongo kule umekwisha, sasa wasipoitia lami ile barabara watakuja kujikuta kwamba wanaitengeneza kwa gharama kubwa sana. Ningeomba zile kilometa tano alizoniahidi basi azitekeleze Mheshimiwa Waziri namwamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Uwanja wa Ndege wa Mafia, nimeona humu kwenye kitabu viwanja vyote vya ndege humu vinafanyiwa ukarabati lakini Uwanja wa Ndege wa Mafia una matatizo makubwa manne. Tatizo la kwanza runway ile ni fupi, hairuhusu ndege ndefu, tunaomba iongezwe. Tatizo la pili, terminal building lile ni kama hakuna, limechoka, linavuja na Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuja aliona. Tatizo la tatu, hakuna taa pale; sisi ile ndiyo escaping route yetu, ikifika usiku upo Mafia imetokea dharura ya mgonjwa, huna namna ya kum-evacuate kuja Dar es Salaam lazima aende na ndege na kama ndege yenyewe uwanja hauna taa, ina maana kwamba huyo mtu anaweza akapoteza maisha pale akisubiri evacuation siku ya pili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwetu sisi kutuwekea taa uwanja wa ndege wa Mafia siyo luxury wala siyo kwamba ni kitu cha anasa, ni necessity kwetu sisi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie basi hatima ya Uwanja wa Ndege wa Mafia na kuwekewa taa sambamba na kuongeza eneo lile la kupaki ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ATCL; tulizungumza hapa Mafia ni kisiwa cha kitalii, kwa siku kuna flight pale zaidi ya nne zinakwenda ndogo ndogo na zote zipo full. Nashangaa kwa nini bombardier haiji Mafia, abiria wapo wa kutosha, lakini watu wa ATCL bado wanasuasua kutuletea usafiri wa ndege kubwa pale kwa ajili ya Kisiwa cha Mafia. Nataka niwahakikishie kwamba watakapoleta bombardier pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia malizia

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kusisitiza kuhusu suala la kutuletea bombardier kwa ajili ya kupunguza tatizo la usafiri Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii na naunga mkono hoja. (Makofi)