Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kuunga mkono hoja. Pili, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kufanya kazi ambayo inaonekana kwa wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake, Mheshimiwa Eng. Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa, kwa kweli wamefanya ziara kwenye eneo langu, Mungu awabariki sana, chapeni kazi, mimi nawapongeza mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia kwa minara ambayo kimsingi nimepata kwenye jimbo langu, mawasiliano walau yameanza kuonekana. Niwaombe sasa uko mnara ambao uko Maga na mwingine Dinamo haujawaka bado, imekaa miaka miwili pale. Najua mki-press kidogo tu ile minara itafanya kazi na mawasiliano yataongezeka na kwa ajili hiyo niwashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia nimeona kwenye hotuba hapa wametuwekea fedha kidogo kwa ajili ya barabara ya kutoka Dongobesh kwenda Babati itajengwa kwa kiwango cha lami na ile ya Mogitu – Haydom, niwashukuru sana. Sasa nilete ombi ambapo nimeona pia mmeweka kidogo na mmeizingatia barabara hii ya Karatu – Haydom – Sibiti, kwa kweli barabara hii tumeomba kwa miaka mingi sana; Mbulu imezaliwa 1905, mpaka leo kwa kweli haina barabara ya lami kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbulu hii imezaa Karatu ina barabara ya lami; imezaa Babati ina barabara ya lami; imezaa Hanang ina barabara ya lami. Kwa hiyo, Mbulu imekuwa wilaya mama tangu mwaka huo wa 1905, nashukuru kuona walau sasa inakumbukwa na nimeona hela kidogo mmeiweka humu. Nasikitika kuona mchangiaji mmoja ni rafiki yangu sana, Mheshimiwa Waziri wewe msamehe tu, amekuwa akisema unajenga barabara kama kitu kinachoitwa nywele, unajenga kwa huku unakata kwa huku, mimi nikuombe msamehe ni kaka yangu, hana tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe anzia kujenga barabara hapo ulipopanga. Kama tumeomba kwa miaka mingi namna hii barabara ya lami ijengwe kutoka Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti, mimi nikuombe jenga hapo ulipoanzia ukianzia Mbulu kwenda Haydom sawasawa, jenga; ukianzia labda Haydom kuja Mbulu, jenga na Mungu akubariki sana. Nimeona hela kidogo umeweka, sasa mimi nikuombe; ongeza kidogo hela hii ili barabara nayo ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mbulu imesahaulika sana. Kwa nini nasema hivi? Leo ukitaka kupita kwenda Shinyanga na hata ukitoka Simiyu lazima upite Singida, hakuna njia ya mkato kwenda Arusha, kwa hiyo kiuchumi tunaitegemea sana barabara hii ya Karatu – Mbulu
– Haydom – Sibiti. Barabara hii inakwenda kwenye majimbo tisa ambayo kimsingi hayana lami kabisa. Mimi leo ukimwambia hata mwanafunzi lami inafananaje hawezi kuijua kwa sababu wala hasafiri, ukijua hiyo basi ujue kwamba lami hakuna kwenye maeneo yetu kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimeshukuru sana na itakuwa mara ya kwanza kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu barabara hii imeonekana kwenye kitabu hiki. Kutokana na haya yaliyoonekana hapa isije ikaishia kwenye vitabu na kwa sababu Rais aliahidi na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imo, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Jimbo la Mjini, Jimbo la Singida kule Iramba na kila mahali naomba imalizike kwani inahitajika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kwanza inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara lakini isitoshe inaunganisha Mkoa huu wa Manyara na Mkoa wa Singida. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwa kuweka barabara hii utakuwa umetimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais lakini pia utakuwa umefungua eneo la uchumi ambao unatokea maeneo haya barabara ilikopita. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana na nikuombee Mungu udumu na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitafurahi sasa kuona barabara hii inajengwa, itajengwa wapi mimi sijali, anzia kipande chochote. Muungwana anasema unapoanza jambo unaonesha nia ya dhati kwamba unajenga. Naona kwamba hela ni kidogo lakini kwa kuwa mimi ni muungwana sana na ni Mkristo, naomba nikupongeze hata kama umeweka kidogo lakini nimeona umeweka na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri katika suala la mawasiliano. Leo tunasajili laini za simu kwa kutumia Vitambulisho vya Taifa lakini ukiangalia wenzetu wa NIDA, Tume ya Taifa na Uhamijaji ni kama wanafanya kazi zinazofanana. Mimi nishauri tu unaposajiliwa kwenye kitambulisho kimoja kwa mfano Kitambulisho cha Taifa wanapochukua finger prints (alama ya vidole) basi iwe tu katika kumbukumbu moja kwa sababu sisi tuna Data Center moja Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, National Data Center itumike vizuri ili huyu wa NIDA akichukua particulars (kumbukumbu) za mtu, kumbukumbu hizo zitumike kwenye NIDA, Tume ya Taifa na Uhamiaji. Kwa maana hiyo basi mtakuwa mmesaidia kuondoa usumbufu kwa mwananchi ili wakati wa kupiga kura pia alama ya vidole akishaweka inaonekana kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa nilete ombi jipya kwako; tunayo Hospitali ya Haydom ambapo kimsingi barabara ile ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti inaelekea, tuna uwanja wa ndege uko pale na ni muhimu sana. Mheshimiwa Waziri naomba kabisa utuangalie, tuwekee kilometa chache katika kujenga Uwanja wa Ndege wa Haydom ili basi wanapokuja wagonjwa, maana hospitali ile ni ya rufaa na inakwenda kuwa ya kanda, utakuwa umesaidia wagonjwa wakitua pale waweze kufika kwa urahisi katika huduma hii ya kibingwa ya hospitali, nikuombe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nishukuru sana kwa kupata nafasi hii na nirudie kukupongeza sana na Mungu akubariki kwa sababu nimeona barabara hii umeiweka. Naamini mwaka huu 2019 kwenda 2020 utajenga barabara ya lami kutoka Mbulu – Haydom – Sibiti na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)