Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupewa nafasi nami kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri wote, na Watendaji wote wa Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa namna wanavyofanya shughuli zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, niongelee tu suala la barabara, suala la barabara, hasa barabara inayotoka Kibena, Lupembe, Madeke na hatimaye Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni barabara muhimu sana, ni barabara muhimu kwa sababu kwanza inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kwa hiyo, Mkoa wa Njombe na Morogoro ulikuwa haujaungana muda mrefu sana, lakini kupitia barabara hii sasa utaweza kuunganishwa na hatimaye wananchi wa Njombe wataweza kusafiri kirahisi kwenda Morogoro na kusafirisha mazao yao na mambo mengine. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mchane tu.
MHE. JORAM I HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana kwa sababu mazao mengi yanayozalishwa Mkoa wa Njombe yanatokea Lupembe. Mazao kama, mbao, miti, chai, kahawa, matunda parachichi, matunda kama nanasi yanazalishwa sana kwenye barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama vile haitoshi, barabara hii pia kuna mazao mengine, kama mazao ya mahindi na maharagwe yanatoka kwenye eneo hili. Kwa hiyo, unaweza ukaona namna gani jinsi ilivyo ya muhimu sana, kwa uchumi wa Mkoa wa Njombe lakini pia uchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, lakini pia Halmashauri ya Wilaya ya Njombe asilimia 80 ya uchumi wake unategemea sana hii barabara ya Lupembe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama vile haitoshi, barabara hii ya Lupembe inategemewa sana, kwa maana ya wakati wa kifuku. Hii barabara huwa haipitiki, kwa hiyo mazao kama nanasi ambayo yanalimwa eneo la Madeke, ukienda Madeke utakuta kuna mashamba mengi, kuna kama zaidi ya ekari, kuna kama estates hizi zipo kule lakini wakati kama huo ambapo mvua inanyesha mazao yale kule yanaozea shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuweza kuboresha uchumi na kuinua uchumi wa Mkoa wa Njombe lakini kuuinua uchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni muhimu sana hii barabara iweze kutengenezwa, lakini nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu Waziri lakini pia na Mheshimiwa Rais kwa kuiweka sasa kwenye mpango sasa tayari kutafutiwa fedha ianze kujengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo, nawashukuru sana kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya mkishirikiana na watendaji wote wa wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, barabara hii ikitengenezwa kwa kiwango cha lami, uchumi wa Njombe utakua, lakini pia uchumi wa nchi utakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine niongee nalo kidogo juu ya minara ya simu kuhusu mawasiliano. Tuna changamoto pia ya minara ya simu katika eneo letu hasa maeneo ya Kata Mfiriga eneo la madeke, halifikiki mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo la Mfiriga, eneo la Idamba, kuna eneo la Ninga pia halifikiki mawasiliano. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na jitihada nimeziona za Serikali mmetuletea mnara kwenye Kata ya Ikondo, tayari Ikondo imefunguka japo bado kidogo kuna matatizo kidogo ya kurekebisha, nafikiri mtayarekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukipata minara hii pia, itasaidia sana kuboresha uchumi. Kwa sababu, uchumi lazima yawepo mawasiliano, mawasiliano ya barabara lakini pia mawasiliano ya simu, ili wananchi au wakulima kwanza waweze kusafirisha bidhaa hizo ambazo wanazalisha ziweze kufikia soko kwa wakati. Lakini pili waweze kuwasiliana na ambako masoko yanapatikana kwa hiyo tukiboresha barabara ikajengwa kwa kiwango cha lami, kwanza tutapunguza muda wa kusafirisha haya mazao kufikia soko, lakini pili wananchi wataweza kupata faida kubwa kwa sababu gharama za usafirishaji zitapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, niombe kwa Mwenyezi Mungu lakini pia niombe kwa maana ya Mheshimiwa Rais na Waziri, nakuamini sana Mheshimiwa Eng. Kamwelwe na Manaibu wako Waziri na Watendaji wote mtahakikisha kwamba fedha zinapatikana ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami na hatimaye uchumi wa maeneo hayo uweze kupanda na mazao yaweze kufikia soko kwa wakati, lakini pia na ikiwekwa minara ya simu itatusaidia sisi Wakulima wa Lupembe kuweza kuwasiliana na soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake, sasa hivi mambo ya ki-digitali, mambo ya teknolojia, lazima kuwe na mawasiliano na hatimaye uweze kuuza kwa wakati na uweze kufikia kujua soko liko wapi na uweze kuuza mazao yako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana najua una kazi nyingi na unafanya mengi, lakini naomba utusaidie kwa haya mambo mawili makubwa ya barabara na hili la minara ili wananchi wetu wa Lupembe waweze kuuza mazao yao lakini waweze kusafirisha mazao yao na nguzo ziweze kufikia soko na hatimaye.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hizi nguzo zinatumika kwenye usambazaji wa umeme, ili tusiwe na tatizo la nguzo, sisi tunalima miti mingi sana, na tunazalisha nguzo nyingi lakini pia zinauzwa kwa bei nzuri. Kwa hiyo, kumbe mkitengeneza hii barabara tutaweza kuuza nguzo na hatimaye tatizo la nguzo nchini litapungua kwa sababu zile nguzo zipo kule na zinapatikana na zinasafirishwa kirahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache nishukuru sana kwa nafasi lakini niunge mkono hoja iliyopo mbele yetu, ahsante sana. (Makofi)