Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru ili na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Elimu, Wizara muhimu sana na awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya ambayo anayoendelea kunijaalia ili niweze kutoa mchango wangu katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Babati Mjini ambao wamenipa dhamana ya kuwa Mbunge wao wa Jimbo na niwaahidi sitowaangusha na baada ya Bunge tutaendelea kuwa pamoja ili tuendeleze Jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niombe Waziri anisaidie kwa sababu hapa tunazungumza suala zima la bajeti. Naomba tu anisaidie katika bajeti yake kabla sijaenda mbele zaidi katika kitabu chake cha Development, kwenye Vote 1003, amezungumzia suala zima la rehabilitation of the schools and colleges. Ametenga shilingi 8,153,000,000 lakini ukienda kwenye randama hii, Mheshimiwa Waziri ulichokiandika huku kwamba unafanya marekebisho ya shule zetu sicho ulichoandika, unaomba na nafikiri umefanya hivyo kwa sababu mkijua wengi Wabunge hatusomi randama, umeandika fedha hizo shilingi bilioni nane unajenga ujenzi wa ofisi ndogo ya Wizara Dodoma pamoja na ukarabati wa Makao Makuu ya Wizara shilingi 6,153,000,000 lakini ukaandika kwamba ni ukarabati na upanuzi wa Taasisi ya elimu ya Watu wazima shilingi bilioni mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo shilingi 8,153,000,000 huku ulivyotuandikia kwamba unafanya rehabilitation ya schools, sicho kabisa ni uongo na niombe majibu ya kina kwa sababu shilingi bilioni nane ukigawa kwa idadi ya madarasa ni zaidi ya madarasa 1,000 yanatakiwa yajengwe kwa fedha hizo na nasema hivyo kwa sababu mmekuja na sera ya elimu bure, watoto wanakaa chini Mheshimiwa Waziri kipaumbele chako ni kujenga ofisi yako kwa shilingi bilioni sita na shilingi bilioni mbili ilihali ukijua watoto wa Kitanzania wanakaa chini, chini ya Wizara yako.
Kwa hiyo, nahitaji uniambie ni kwa nini Waziri mwenzetu, mwanamke mwenzetu, mwenye uchungu kwa watoto wa Kitanzania unatenga fedha zaidi ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya ujenzi wa ofisi yako ilihali watoto wanakaa chini na Wizara hiyo unaongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa la Kitanzania literacy level yetu ni asilimia 67. Watanzania wengi zaidi ya asilimia 30 bado kusoma na kuandika ni tatizo. Lakini kwa hali ya kawaida Taifa hili ambalo linapigana vita, maaskari hawa ambao wako vitani wamesahauliwa kwa asilimia zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu kama Mbunge wa Jimbo nilikaa na walimu wangu kuwafikia kwenye shule zote zaidi ya 30 katika Jimbo la Babati Mjini. Wala haya ninayoyachangia siyabahatishi na maaskari na walimu hawa ambao wanapambana na ujinga katika Taifa la Tanzania na naamini haya nitakayosema ambayo nimeambiwa na walimu wangu wa Babati ndiyo wanayopata walimu katika nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la madaraja walimu wetu. Mmetoa miongozo kwa miaka mitatu mnapandisha madaraja lakini walimu wanaofundisha huko katika shule zetu wanakaa miaka minne hawajapandishwa madaraja, lakini Mheshimiwa Waziri mnawapandisha madaraja kwa ceiling ya bajeti. Mimi naomba niishauri Serikali, kwanini mnawagawa walimu na maaskari hawa ambao wanapigana katika Taifa la Tanzania kuondoa ujinga? Kama hakuna fedha msiwagawe walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu wanaajiriwa pamoja, kwenye madaraja wanatofautiana, kwenye mishahara wametofautiana, kwa nini? Mnapeleka wachache eti ukomo wa bajeti wengine wasubiri, nani kakwambia hivyo Mheshimiwa Waziri? Huu ni ubaguzi, walimu hawa kama hakuna fedha subirini mkipata muwapandishe hata kwa miaka mitano wote au miaka minne badala ya kuwagawa, hilo naomba majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanaohamishwa kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine, Halmashauri nyingine kwenda nyingine akifika anaanza upya, daraja halipandi, anaambiwa huko ulikotoka ndiko ambako mambo yako yamekosewa, hebu Waziri tuambie leo hivi kuhamishwa ni dhambi kwenda kusaidia sehemu nyingine? Kwa nini walimu hawa wakihamishwa kwenda Halmashauri nyingine madaraja yao wanaanza upya, hawaendelei na madaraja waliyonayo? Unaongoza hiyo Wizara tupe majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti lakini lingine, hivi Serikali haina mpango kazi kwa walimu? Transport allowance? Leo anaibuka Makonda anasema walimu wapande mabasi bure. Msiwalipe transport allowance kwa nini? Yaani Serikali mmeacha walimu yeyote aamue kwamba hawa leo wapande bodaboda, hawa wapande mabasi bure, hawa wakejeliwe hivi kwa nini? Muwalipe walimu wetu transpot allowance. Sitting allowance hamuwalipi, yaani mwalimu hana shift yoyote, kwanza wanalalamika muda wanaingia saa moja wanatoka saa kumi, hawana wa kuwapokea wakati madaktari, manesi na fani zingine wana-shift lakini pia wanalipwa on call allowance, mwalimu halipwi housing allowance, sitting allowance wala transport allowance, umempeleka kijijini kule hakuna nyumba. Hivi kweli Mheshimiwa Waziri umekaa kwenye Wizara hiyo kwa muda mrefu, haya matatizo unayafahamu, leo nahitaji majibu kwa ajili ya walimu wa Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Waraka wa Elimu Bure, sawa, mmeiga kutoka kwetu UKAWA elimu bure mkakurupuka mkaanzisha. Haya mtuambie na mimi niliuliza swali kwa Waziri Mkuu, ni kwa nini mmekurupuka katika hili la elimu bure? Mnachokifanya sasa hivi shule zetu hakuna pesa. Shule ya wanafunzi 800 mnapeleka OC ya shilingi 200,000. Madeni katika shule zetu, Mheshimiwa Waziri tangu mwaka jana shule zinadaiwa pesa za ulinzi, za maji, za umeme kila shule yangu niliyopita inadaiwa zaidi ya milioni tano. OC ya shilingi 200,000 inaendeshaje shule? Mnaua elimu ya Tanzania. Mmetuachia huko kwa TAMISEMI mnasema kwamba huko tutafute pesa, hakuna. Mnabadilishia gear angani. Mlituambia kwenye waraka kwamba madawati wazazi hawatachanga leo wazazi wa Babati wanachangishwa Madawati, mnageuzia gear angani. Mtuambie kwanini mnatudanganya? Na hizi fedha mnapeleka lini tunahitaji mtuambie msitudanganye Watoto wetu wanakaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa walimu wa sayansi. Mheshimiwa Waziri, zaidi ya walimu 30,000 wanahitajika wa sayansi katika nchi hii. Nimepita kwenye shule za sekondari, ninauliza hata mwalimu aliyesoma BAM (Basic Applied Mathematics) A-level aniambie kama yupo afundishe mathematics, hakuna mwalimu wa hesabu kwenye shule za sekondari halafu Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako unasema ujenzi wa maabara katika shule zetu za sekondari utakamilika mwaka 2018/2019 ndiyo vifaa vya maabara utapeleka huko. Tunapataje walimu wa sayansi ilihali hata maabara huko hakuna vifaa na hampeleki? Mnajenga ofisi zenu kwa shilingi bilioni nane, mnataka walimu wa sayansi wa mathematics, wa chemistry hawapo kwenye shule zetu, mnategemea mtabadilisha Taifa hili kweli elimu ya nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha shule hatuna walimu wa sayansi. Mheshimiwa Waziri nikushauri tu, walimu wa arts tunao wakutosha. Boresheni VETA, pelekeni vijana wetu huko VETA muwadahili walimu wa sayansi, mtupelekee walimu wa sayansi kwenye shule zetu. Msitegemee watapatikana huku juu, huku chini hata hayo maabara mmeshindwa kujenga. Waziri nakupa tu ushauri wewe ni Mwananmke mwenzangu naomba tu nikupe ushauri labda utanielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine niurejeshaji wa mikopo. Mheshimiwa Waziri Bunge lililopita tulikuwa tunalipa, mimi ni-declare interest, mimi nimelipa nimemaliza. Lakini Bunge lililopita tuliandaliwa mpango hapa, Wabunge wote tumelipa, tumekuwepo Bunge lililopita. Hivi nchi hii kodi mpaka ikusanywe mpaka Magufuli aende na polisi na mbwa kama alivyoenda bandarini ndiyo mkusanye? Ndiyo mtakusanya?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti mbona sijaona mkakati wa ninyi kukusanya fedha hizi, mtuambie wazi wazi, halafu mnasema mtu akichelewa kulipa eti mnampiga interest ya 10% kwa sababu amechelewa, ajira ziko wapi? Wamekaa mtaani hawana ajira baadae unampiga eti penalty ya 10%, kweli Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani muache kuimba Serikali ya Magufuli, hii nchi ni ya kwetu sote! Isiwe ni one man show kwamba Magufuli asipofikiria ninyi Mawaziri mnasubiri leo anaamkaje anasemaje, njoo na mpango kazi wako wa kukusanya hizo fedha, hata hapa basi ungetuita Wabunge wote hapa tujue nani anadaiwa, tulipe hizo pesa. Lakini pia utuambie na hao wengine ambao wameajiriwa kwenye sekta ambazo sio rasmi wanalipaje, sio tunamsubiri Rais akisema basi wote ndiyo tunaenda huko, hapana! Hatuwezi mkaendesha nchi kwa show ya kiasi hicho! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la shule za awali. Mheshimiwa Waziri najua utasema iko TAMISEMI, jamani mmechukua sera ya elimu bure, basi tembeleeni! Mtoke na Simbachawene muende hizo shule. Walimu kwanza hawana mitaala na watoto wetu wanakaa chini ya miti, hakuna darasa, mmewaambia Wakurugenzi watafute hizo fedha wajenge, hawana! Collection za Halmashauri ndiyo hizo mnasema mnaenda kukusanya wenyewe, mpaka zitoke lini? Watoto wananyeshewa na mvua!
Naomba leo mniambie Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Elimu iko chini yako, sera na mambo mengine naomba leo utuambie kwenye hili Bunge, una mkakati gani kwa ajili ya watoto wetu wazuri? Wale wa miaka mitano ambao wanakaa chini, mkituachia Halmashauri tujenge hayo madarasa tutajenga kwa muda gani kama Serikali ya CCM mmejenga VETA kwa miaka 10 hata VETA moja kwa Wilaya haijakamilika! Mnategemea hao watoto…
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Mnategemea watajenga shule hizi za msingi….
MWENYEKITI: Mheshimiwa ni kengele ya pili hiyo!