Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo iko mbele yetu. Pia nimshukuru Mungu pia kunipa kibali kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia wananchi na kutumikia taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka sera ya kuwasaidia kujenga uwezo kwa makandarasi wa ndani kwa maana ya kwamba zile barabara ambazo ziko chini ya kilometa 30 wanapewa wakandarasi wa ndani ili kujenga uwezo wao, pia kuendelea kuenzi kazi zao za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na tatizo kubwa sana la udhaifu mkubwa sana la utekelezaji wa kazi zinazofanywa na wakandarasi wa ndani. Na hapa ninasema kwamba hatuwachukuii wakandarasi wa ndani tunawapenda, lakini tunaangalia matatizo tuliyokuwa nayo pia miradi ambayo inapangwa iende kwa muda na kazi iende kwa muda unaotakiwa. Leo kazi ya mwaka mmoja inafanyika kwa miaka mitatu, wapo wakandarasi ambao kiukweli ni dhaifu uwezo ni mdogo na unapoambiwa kwamba washirikiane na wenzao pia wanakuwa ni wagumu, ninaomba Serikali ituambie tutaendelea kuwabeba wakandarasi wa aina hii mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wantanzania wanapata shida mfano mmoja ni barabara Kaliua Urambo, kilometa 28 tu wamepewa wakandarasi wamepewa mwezi wa 4 mwaka 2017 ilikuwa ni kazi ya mwaka mmoja, leo ninapoongea na wewe na hapa Bungeni hata robo haijafika na wako site, na visingizio kila siku mara mvua, mara jua mara hiki ukienda pale kazi inayofanyika haieleweki, lakini wakati huo huo wenzao wa nje, wenzao wa CHICO walipewa kandarasi pamoja wamejenga barabara ya Neuya hapa kwenda Tabora kila siku wako kazini na kazi yao ni nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ituambie tutaendelea kuwabeba hawa wa ndani mpaka lini? Kama lengo ni kuwasaidia tunawatesa wananchi, tunawaonea wanachi. Kaliua ni Wilaya yenye uzalishaji kubwa sana asilimia 60 ya tumbaku yote Tanzania inatoka Kaliua mazao mengi mpunga, mahindi, karanga, lakini ukiona barabara ambavyo magari yanapita unaona huruma, pia Kaliua sasa hivi hatuna hospitali ya Wilaya, ukiona mtu akipewa rufaa akienda Tabora unamuonea huruma ile barabara jinsi ambavyo ni mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ituambie sasa baada ya mkandarasi wa pale barabara ya Kaliua Urambo kuongezewa muda tena karibu mwaka mzima ni lini ile barabara itakamilika kwa kiwango kinachotakiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni barabara inayoungasha Mkoa wa Tabora, na Katavi pamoja Shinyanga, barabara inayoanzia Katavi inakuja Kaliua inakwenda Uliyankulu inakwenda mpaka Kahama, barabara hii ni barabara muhimu sana kwa uchumi na pia ni barabara kuu ni barabara ambayo iko kwenye TANROADS, lakini kuna kilometa 60 kutoka Kangeme kwenda mpaka kilometa 120 kwa maana ya mpakani haijaguswa wala kufunguliwa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini sasa kile kipande cha kilometa 60 kutoka Kangeme, kwenda mpaka pale mpakani mwa Katavi itafunguliwa? Kilometa 60 zingine zimefunguliwa, lakini barabara hii ni lini sasa itatengezwa kwa kiwango cha lami sababu ni barabara ya uchumi, barabara kuu, barabara ya Mkoa kati ya Mkoa na Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la barabara zilizopo pale Kaliua Mjini ahadi Mheshimiwa Rais ambaye alituahidi wakati uchaguzi, pia ameahidi 2017 alifanya ziara Kaliua kwamba kilometa saba za pale Mjini zijengwe na aliagiza kwa haraka mpaka leo barabara hizo bado hazijajengwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa waziri atakapokuja ku-windup atuambie barabara za pale kilometa saba za pale Mjini zitajengwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la mitandao, maeneo mengi ya Kaliua tena maeneo ambayo yana uchumi mkubwa wa kilimo hayana mawasiliano ya simu hivi tunayoongea kuna watu wanapanda kwenye mti ili aongee hata aseme shida yake apande juu ya mti aongee ndiyo Mhehimiwa Mbunge aweze kupata shida yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuambiwe maeneo mbalimbali ya Kaliua yatapata mitandao ya simu lini? Mheshimiwa Waziri nimezungumza sana kwa habari ya maeneo haya, maeneo ya Pandamloka ambapo mchele mwingi unaolimwa Kahama unapatikana Pandamloka, hakuna mawasiliano ya simu, Pandamloka, Mwahalaja, Kombe, Shela, Maboha, Luenjomtoni, Usinga, Ukumbi Kakonko, Mkuyuni, Mpilipili, Igombe maeneo yote haya ni muhimu kwa uchumi, yanalima sana lakini kwa miaka yote kiukweli wanateseka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana maeneo haya yaingie kwenye bajeti. Naomba tuambiwe sasa ni lini minara itajengwa maeneo yale ili wananchi wa Kaliua ambao wanalima sana, wanachi wa maeneo mengi ya nchi hii waweze kupata mawasiliano na waweze kuwa na huduma nyingine kama wananchi wengine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)