Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushurkuru sana kwa kunipa nafasi. Pia naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Kamwelwe; Naibu Waziri, Mheshimiwa Nditiye pamoja na mtani wangu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii ya miundombinu. Vile vile naomba nichukue fursa hii kusema kwamba naungana na taarifa ya Kamati, taarifa ya Kamati imekuwa nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa maoni ya Kamati, imeelekeza kwa Serikali na Wizara kwamba umefika wakati kuwe kunatengwa bajeti ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwa barabara zinazounganisha mkoa na mkoa. Katika Jimbo la Mufindi Kaskazini nina barabara kubwa tatu; barabara ya kwanza inaanzia Kinyanambo C, Itimbo mpaka Kihansi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi, ndiyo kwenye bwawa la Kihansi ambalo linatoa umeme megawatt 180, lakini cha kusikitisha barabara hii haina hata kilometa moja ya lami. Pia barabara hii inaunganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Morogoro kwa maana ya Wilaya ya Mufindi na Wilaya ya Kilombero, sasa ufike wakati Serikali ione kuna haja ya kupeleka barabara ya lami kwenye eneo hili ambako kuna umeme wa uhakika na siyo umeme tu, hata eneo mkubwa wa msitu wa Sao Hill liko katika Tarafa ya Kibengu. Kwa hiyo, uchumi mkubwa katika Jimbo la Mufindi Kaskazini unalala katika barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la barabara kutoka Kinyanambo A, Isalavanu, Igombavanu, Sadani mpaka Ludewa, barabara hii ina kilomita za mraba 151. Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005, sisi CCM tulisema barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami, tukarudia 2010 na tukarudia 2015 -2020, lakini cha kusikitisha hakuna hata kilomita moja ya lami iliyojengwa katika eneo hili. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha aje hapa atueleze sababu zipi zinapeleka barabara hii isijengwe kwa kiwango cha lami. Mwaka 2009 ilifanyika tathmini ya kuangalia zile nyumba zote ambazo ziko kando kando ya barabara ambazo mpaka leo wananchi wamekaa mkao wa kula lakini miaka kumi imepita, hakuna hata mwananchi moja aliyelipwa fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atatuambia wale watu waendelee kusubiri au kuna utaratibu mwingine ambao Serikali imejipanga kuhakikisha watu wanalipwa fidia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ambayo ni barabara muhimu inaunganisha tena Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Morogoro, ni barabara inayoanzia Kijiji cha Mtili, Ifwagi, Mdabulo, Ihanu, Isipii mpaka TAZARA mpaka Mlimba. Barabara hii ina kilometa za mraba 136, lakini barabara hii haipitiki kabisa, ni tatizo katika Jimbo la Mufindi Kaskazini. Kwenye barabara hii nako kuna uchumi mkubwa, kuna bwawa ambalo linatoa umeme megawatt saba, barabara hii kuna uchumi wa chai, uchumi wa msitu na uchumi wa pareto, lakini barabara haipitiki kabisa. Sasa ni vyema Serikali ikaona kwamba kuna haja barabara hii kuihamisha kutoka TARURA kuipeleka TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA hawana uwezo hata wa kutengeneza kilomita 20 kwenye barabara hii. Kwa hiyo hali imekuwa mbaya, hivyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri alione hili. Mheshimiwa Rais alipokuwa Waziri wa Miundombinu alikuwa ameshaanza mkakati wa kutaka kuihamisha barabara hii kuipeleka TANROADS, lakini hilo zoezi limekufa ghafla na sielewi tatizo liko wapi. Vilevile Mheshimiwa Rais alipokuwa amekuja pale Mufindi aliahidi kwamba atahakikisha yale maeneo yenye utata kama barabara hii inachukuliwa na kuwa ya TANROADS. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwaa anahitimisha atuambie anatusaidiaje watu wa Mufindi ili tuendelee kuwa na uchumi uliokuwa imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nataka kulizungumzia ni eneo la mawasiliano. Katika Jimbo la Mufindi Kaskazini kuna matatizo ya mawasiliano katika Kata tatu au nne hivi; ya kwanza Kata ya Ikweha hakuna mawasiliano kabisa; pili Kata ya Mapanda hakuna mawasiliano kabisa; tatu Kata ya Ihanu; na nne Kata ya Mpangatazara. Tumekuwa tunauliza maswali mara kwa mara hapa na Waheshimiwa Manaibu Waziri wameniahidi mara nyingi kwamba watakuja kutembelea na kuja kuangalia matatizo ya mawasiliano katika hayo maeneo, lakini mpaka leo hawajafika. Sasa nataka wanapohitimisha hapa wanihakikishie mbele ya Bunge lako Tukufu, ni lini watakuja kwenye maeneo haya kusudi waweze kujua matatizo ya mawasiliano katika maeneo haya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)