Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema nami niweze kuchangia Wizara hii ya Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza tu kwanza niseme kwa moyo wa dhati kabisa kwamba miundombinu ni jambo ambalo nchi za wenzetu, nchi zote za Ulaya na kule Marekani watumwa walipelekwa nchi hizi kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu. Leo hii nchi za Ulaya na Amerika zimeweza kuendelea kwa sababu ya miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nieleze kwamba kwa kasi hii ambayo tunaiona ya ujenzi wa miundombinu Tanzania, Wizara hii imefanya kazi kubwa sana. Jambo la kipekee ambalo naweza kuzungumza pamoja na kwamba kuna miradi mingi sana sasa hivi imeanzishwa katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu na ni imani yangu kwamba baada ya miaka 10, 15 Tanzania tutafikia ule uchumi wa kati 2025 na kuendelea huko kama kasi ya miundombinu itaenda hivi hivi kama ilivyo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala ambalo wenzangu wamezungumza na hasa taarifa ya Kamati imezungumzia kwa kina sana kwamba ili tuweze kuendelea hivi sasa na hata nchi za wenzetu kama nilivyotangulia kusema waliwekeza kwenye miundombinu na hasa miundombinu ya reli. Kwa muda mrefu imekuwa ikizungumzwa takriban miaka mitatu hivi sasa kila mwaka katika vitabu vya bajeti inatajwa Reli ya Kati (Standard Gauge) ambayo hii inajengwa lakini Reli ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Reli ya Kanda ya Kusini ni muhimu sana kiuchumi kwa sababu reli hii itaanzia Mtwara Mjini kuelekea Mchuchuma na Liganga ambako kuna makaa ya mawe na chuma. Hii reli kwa taarifa tulizokuwa nazo mpaka hivi sasa kwa sababu Serikali imejipanga kwenda kujenga kwa kutumia mfumo wa PPP (Public Private Partnership) na kuna wawekezaji wengi wameamua kujitokeza kuwekeza kwenye hii reli, mimi niishauri Serikali isiwe na kigugumizi cha ujenzi wa hii reli kwa sababu economic viability yake ni kubwa sana kuliko reli zote Tanzania. Tunaomba Serikali itenge fedha za kutosha isiwe kila mwaka tunaelezwa kwamba upembuzi yakinifu umekamilika, pesa tunaenda kuzitoa sijui wapi, wapewe hawa wawekezaji ambao wako tayari kuwekeza katika hii Reli ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli hii ikijengwa maana yake tunaenda kufufua ule mpango unaoitwa Southern Development Corridor yaani Maendeleo ya ule Ukanda wa Kusini. Tunaamini reli hii ikiisha kutokea Bandari ya Mtwara Mjini tutaenda kufufua uchumi na hata nchi zote za Ukanda wa Kusini watatumia reli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kwa sababu Serikali imeweka kwenye mpango kwa muda mrefu kazi iliyobaki ni kutekeleza. Tunahitaji Reli ya Kusini na hata taarifa ya Kamati imeeleza kwa kina sana kwamba reli hii inaenda kuleta uchumi mkubwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wananchi waweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza ni suala hili la usafiri katika bahari zetu. Serikali imekuwa na kizungumkuti, siku zote Serikali haiwekezi kwenye uwekezaji wa meli katika Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya nyuma wakati si tunakua, sisi tunaishi kule Pwani Mtwara, tulikuwa tunatumia sana usafiri wa meli kutoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam na maeneo mengine mpaka kule Zanzibar. Kama kweli tunahitaji kufufua uchumi wa Tanzania tusiwekeze kwenye kujenga tu barabara hizi tununue meli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunazungumzia uwekezaji, kuna ile taasisi ya Serikali inaitwa Marine Service ambayo inajenga meli katika Maziwa Makuu. Neno marine maana yake ni bahari, kwa hiyo, nashauri sana Serikali inunue meli kwa ajili ya kusafirisha cement kutoka pale Mtwara, Mheshimiwa Dangote anatumia magari kusafirisha kwa njia ya barabara ya Kilwa na inaharibika sana. Kama Serikali ingenunua meli au ingewekeza kwenye meli usafiri wa meli ni rahisi kuliko usafiri wowote duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule hakuna kutengeneza barabara, maji Mwenyezi Mungu kayaweka, kazi ya Serikali ni kusafirisha tu. Kwa hiyo, cheapest transport duniani ni usafiri wa meli, kwamba Serikali ikiwekeza kwenye meli tunaamini kabisa barabara zetu za Ukanda ule wa Kusini hazitaharibika kwa malori makubwa makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba sana Mtwara Mjini baadhi ya maeneo hakuna mawasiliano ya simu. Nimekuwa nazungumza kwa muda mrefu na nilimwandikia Naibu Waziri, Mheshimiwa Nditiye ananisikia, nilimweleza kwamba kuna maeneo ya Mtwara Mjini ambapo hakuna mawasiliano ya simu yaani ukifika kule mawasiliano hakuna. Maeneo kama ya Mkunja Nguo, Naulongo, Mkandala, Dimbuzi na Mwenge mawasiliano ya simu kule hayapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimwambia Mheshimiwa Nditiye kwamba tunahitaji awekeze ili watu wa Mtwara waweze kupata mawasiliano ya simu kwenye maeneo haya. Baadhi ya maeneo ya pembezoni ya Mtwara Mjini tunahitaji minara ya simu ili wananchi waweze kuwasiliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, tunahitaji hizi ndege ambazo Serikali imeamua kununua za ATC zifike Mtwara. Taarifa tunazoambiwa kwamba Mtwara hakuna abiria si kweli, Precision kila siku asubuhi wanakuja Mtwara na kurudi na wanajaza iweje leo ATC wanatuambia kwamba eti Mtwara hakuna abiria. Sisi tunahitaji hizi ndege kwa sababu ni za bei nafuu, kazi yake ni kutoa huduma kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wana- Mtwara tunahitaji ndege hizi tuweze kuzipanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni ucheleweshaji wa miradi. Ni kweli kuna kasi kubwa ya uanzishwaji wa miradi ya barabara lakini wakandarasi wanacheleweshwa sana kupewa fedha zao. Kwa mfano, barabara ile ya uchumi ambayo inaanzia pale Mtwara Mjini – Mnivata - Tandahimba mwaka huu nimeona kwenye kitabu hapa kwamba zimeongezwa kilomita zingine 50 lakini hiyo kilometa 50 kutoka Mtwara Mjini - Mnivata zinasuasua sana kwa sababu yule mkandarasi hapati pesa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, alikuwa anafanya kazi kubwa sana akiwa kwenye Wizara ya Maji Mheshimiwa Nditiye, Mheshimiwa Kwandikwa rafiki yangu kabisa na amekitembelea kipande kile cha kutoka Mtwara Mjini – Mnivata mkandarasi anasuasua fedha hapati kwa wakati. Naomba mumpe fedha kile kipande cha barabara kiweze kuisha na kipande kuanzia Mnivata - Tandahimba na maeneo mengine yale tunaomba mwaka huu fedha zitoke kwa wakati yule mkandarasi aweze kumaliza ili na sisi barabara hii tuweze kuitumia. Hii barabara ndiyo chanzo kikuu cha uchumi, korosho zote zinapita kwenye barabara hii kutokea Tandahimba - Mtwara Mjini pale bandarini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni barabara ya ulinzi ambayo nimekuwa naizungumzia kwa muda mrefu ambayo inaanzia Mtwara Mjini – Tangazo – Mahurunga – Kitaya - Kiromba na ukanda ule wote mpaka Mozambique. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ndiyo chanzo cha ulinzi wa Ukanda ule wa Kusini naomba nayo ipewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)