Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru wka kunipa nafasi niwe wa kwanza leo, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na wafanyakazi wa wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya. Naanza, nina mambo matatu kwa kweli, moja ni suala la barabara ya kwangu kule Mwandiga kwenda Kabunga ni barabara mpya barabara ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi kwenye kampeni, ningetamani sana tutakapoenda kwenye kampeni mwaka kesho hilo lisiwe swali, naomba sana waziri tujitahidi barabara hii tuweze kuimaliza na barabara hii ina faida zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hii ikiisha maana yake Gombe watu hawataenda kwa njia ya boti; barabara hii ikiisha TPA wamejenga bandari kule Kagunda ili bandari ile iwe na maana lazima barabara hii iishe TPA na halmashauri wanajenga soko Kagunga ili soko lile liwe na maana kwa biashara ya Burundi na Uvira, lazima barabara hii iishe, niombe sana Wizara tujitahidi barabara hii iishe kwa kweli ni barabara ya kiuchumi ni barabara ya kiulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni suala la PPP. Nimesoma kitabu hiki cha Waziri sijaona popote tunapoongelea barabara za PPP au mradi wowote mkubwa wa PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ningeomba sana watu wa Serikali watusaidie. Mimi naamini tunapoongelea barabara Tanzania, Rais Nyerere alijenga barabara, Mwinyi alijenga barabara, Mkapa alijenga barabara, Kikwete alijenga barabara, Magufuli anajenga barabara. Mimi leo nataka tumtenganishe Magufuli na Marais wote waliopita kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kumtenganisha lazima tuje na mawazo mapya. Umefika wakati barabara za nchi hii tuanzishe super high way ambazo hatutumii fedha zetu. Tutajenga barabara ambazo tutalipa kwa road toll. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu fulani Serikalini wanasema kwa kujenga standard gauge barabara haina maana, siyo kweli.

MBUNGE FULANI: Siyo kweli.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, Dodoma Jiji, ili Dodoma iwe accessible lazima tujenge super high way from Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha. Maana yake ni nini? Kama kuja Dodoma ni saa nane, maana yake Dodoma haiwezi kukua kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nasema reli hata ikiisha kazi yake ni mizigo. Kama mnadhani tunajenga reli kwa ajili ya kusafirisha watu nadhani siyo sahihi. Kwa hiyo, tunasema tujenge barabara na hizi barabra duniani kote wanatumia hela za PPP, Malaysia, Marekani na China wanatumia PPP, tatizo letu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi na wewe tulikwenda kwenye mkutano wa IPU, Urusi. International Airport ya Urusi (Moscow) ni ya mtu amejenga, siyo Serikali lakini service zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua sana mambo ya barabara kwa sababu na mimi nimekulia humo ndani, naombeni tumfanye Magufuli awe tofauti na wenzake. Namna bora ya kuwa tofauti ni moja tu: Amekuwa tofauti kwenye reli, wote hawakujenga reli yeye anajenga reli; amekuwa tofauti kwenye umeme wa Stiegler’s wote hawakufanya yeye anafanya, naombeni tumpe na utofauti wa barabara, tujenge super high way nchi nzima ambazo watu watakuja kwa kulipa. Chalinze high way tumeiondoa, why? Ukiwauliza watu wa Serikali wanasema Chalinze high way tumeiondoa kwa sababu kuna standard gauge, hapana, havina mahusiano hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo lazima watu wote watapanda reli. Haiwezekani kilometa 100 tunakwenda saa tatu, kiuchumi siyo sawa. Kwa sababu infrastructure ndiyo inayoleta uchumi, ndiyo enabler wa economy. Sasa kama infrastructure ndiyo enabler wa economy lazima tufanye vitu ambavyo vitasababisha goods zifike mapema, tuweze kwenda kwenye maeneo yetu mapema, twende kwenye biashara tuwahi kurudi. Sielewi kwa nini Serikali haitaki miradi ya PPP. Naamini kama tunataka twende haraka lazima twende kwenye PPP. Wenzetu wote wanatumia fedha za watu, hii kwamba lazima tufanye wenyewe siyo sawa.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya kufanya wenyewe ni haya yafuatayo. Barabara ya kutoka Nyakanazi kwenda Kabingo Kilometa 50 tunajenga huu mwaka wa 10. Barabara ya kutoka pale Kidahwe - Kasulu huu mwaka wa 10. Maana yake ni nini? Tuna shida nyingi sana tunataka kufanya yote. Namna bora ili tuweze kwenda kwa kasi, maeneo mengine tuwaachie wengine wafanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini Watanzania hawawezi kushindwa kulipa road toll, hawawezi. Kama natoka na basi Kigoma saa 12.00 asubuhi, nina uhakika nitakuwa Dar es Salaam saa 10.00 kuna shida gani ya kuweka toll? Nani atakataa kulipa toll? Sielewi kuna nini Serikalini. Sielewi why Serikali hawataki miradi ya PPP, sielewi.

Mheshimiwa Spika, napenda Waziri atakapokuja atuambie hivi sisi ni tofauti na watu wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukienda Marekani hata uki- google, mtu pekee anayekumbukwa kwenye barabara Marekani ni Rais Franklin Roosevelt? Kwa sababu gani? Baada ya vita kuu ya pili ya Dunia aliamua kuunganisha states zote 50 kwa super high way na watu wanalipa kwenye toll. Kwa nini hatutaki kufanya hivyo? Kwa hiyo, mimi ningeomba sana Serikali, najua jambo hili linawawia ugumu lakini sioni ugumu wake ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni viwanja vya ndege. Mimi hili naleta ushauri Serikali mlitafakari upya, nadhani umefika wakati viwanja vya ndege viachiwe kazi ya kujenga na kuendesha. Habari ya kuchukua viwanja vya ndege unapeleka TANROADS, inawezekana ni nia ya kudhibiti lakini kuna ucheleweshaji. TANROADS wana kazi kubwa, wana madaraja, barabara na kila kitu. Ningeomba suala la viwanja vya ndege tuvirudishe. Pale tumepeleka CEO mzuri sana, Engineer Ndyamkama is one of the best, tumpe kazi hii ataifanya na kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuweke taa kwenye viwanja vyetu. Tumenunua ndege lakini ili ziweze kufanya kazi mara nyingi tunahitaji taa. Hii kusubiri jua tu maana yake ndege zetu hazifanyi kazi at its capacity. Kwa hiyo, naomba sana hili nalo liangaliwe.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la bandari. Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana viongozi wa bandari kwa kazi kubwa wanayofanya. Hata hivyo, kazi kubwa inayofanyika bandarini naomba tuwasaidie tuondoe vizingiti barabarani.

Mheshimiwa Spika, kwenye transit trade, biashara hii tupo na wenzetu sasa kama kila baada ya dakika tano kuna Polisi, tunaifanya bandari yetu isiwe attractive. Kwa sababu gani? Bandari itafanya kazi vizuri, inatoa mizigo kwa wakati lakini lori likishaingia mpaka kufika Tunduma ni shughuli ya siku nne au tano. Wafanyabiashara wanataka waende haraka warudi, hii ndiyo maana ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kwetu kuna point nyingi za kukaguliwa unapotoka Dar es Salaam mpaka Kigoma na unapokwenda kwenye mipaka yetu nawahurumia wale wanaoendesha haya malori kwa sababu wanasimamishwa kila baada ya kilometa 3 au 4, trafiki wapo. Rais amesema jamani eeh, Polisi haiwezekani mkasema kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kuna point mbili za kukagua, huku kwingine kote wanasimamishwa, biashara haiwezi kutusubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa bandari yetu inapambana na ushindani wa Mombasa na Beira kwa sababu bandari ina-perform lakini kama wale wengine hatuisaidii itaonekana imeelemewa. Kwa hiyo, naomba sana watu wa Serikali tuwasaidie sana watu wa bandari kwa maana ya ku-enable ili kazi yao iweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni suala la fedha za barabara hasa za GOT. Naomba sana Serikali, ukiangalia trend yetu, barabara ambazo zinajengwa na GOT zinatumia muda mrefu sana. Maana yake ni nini? Zikitumia muda mrefu, interest rate, idle time, kwa barabara ambayo ungeijenga kwa shilingi bilioni 50 unaijenga kwa shilingi bilioni 100, siyo sawa. Atakuja mtu siku moja tutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba na mimi niunge mkono hoja, nakushukuru sana.