Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, ni aibu kubwa sana kwa taifa hili kuwa na wanasheria ambao wanafanya negotiation kwa miaka saba. Hii inadhalilisha sana wanasheria hapa nchini au wale wote ambao wapo katika tume ya kufanya negotiation kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, uliunda Kamati ya Tanzanite hapa pamoja na Kamati ya Almasi. Wabunge walitumia miezi mitatu tu kuishauri Serikali na kufanya marekebisho katika mikataba ambayo ilikuwa ni mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kupitia matakwa ya Ibara ya 63 ya Katiba na marekebisho ya sheria tuliyoyafanya mwaka jana ambayo yanalipa mamlaka Bunge kupitia mikataba mbalimbali, nikuombe unda Kamati. Kama tatizo ni mkataba kwenye suala zima la Bandari ya Bagamoyo, unda Kamati, Wabunge wako vizuri, hatutatumia miaka saba. Tunahitaji miezi miwili, miezi mitatu na tutaishauri Serikali na pengine tutawaita wahusika. Kama mkandarasi anayejenga hana uwezo, basi tutafute mkandarasi mwingine ambaye atahusika na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ikizingatiwa kwamba bandari hii ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anguko kubwa la kiuchumi la watu wa Pwani limetokana na ubovu wa miundombinu. Wewe ni shahidi, Pwani ya Kusini, kuanzia Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Kilwa miaka 700 iliyopita walikuwa na uwezo wa kutengeneza coin yao. Juzi katika Pwani ya Australia wameokota coin ambayo ilitengenezwa Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, tumekwenda pamoja Russia, tumekutana na wananchi wa Fiji, wao wanasema walitokea Rufiji, Pwani ya Tanganyika ambako ndiko kunatokea Nyamisati na maeneo mengine. Wewe ni shahidi tulikuwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Pwani siyo goigoi bali tatizo kubwa tulilonalo ni miundombinu mibovu. Iwapo miundombinu itaboreshwa, Pwani ya Kusini tutaweza kulisha Tanzania hii.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi ulikuwa Kingupila na Ngarambe, Rufiji kuna viwanja vya ndege vitatu, ndiyo wilaya pekee hapa nchini ambayo ina viwanja vya ndege vya kutosha. Mkoloni asingejenga viwanja vya ndege kama eneo hili lilikuwa halifai kiuchumi. Kule Ngarambe kuna vipepeo mamilioni ambavyo duniani hakuna lakini watalii watafikaje Ngarambe, ubovu wa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya miundombinu imefanya Warufiji washindwe kuzalisha. Tunaona ni bora tulime vyakula vitakavyotufaa wenyewe kuliko kulima vyakula vingi ambavyo inatugharimu kusafirisha kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, tarehe 4 Machi, 2017, Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete. Sitakuwa na mchango wowote iwapo nitashindwa kutaja barabara ya Nyamwage – Utete ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi.

Mheshimiwa Spika, sisi wanasheria tunatambua, zipo ahadi wakati wa kampeni, ahadi hizi wakati mwingine zinaweza zisitekelezeke kwa sababu ni ahadi ambayo mtu anaahidi ili aweze kupata. Mheshimiwa Rais aliahidi 4 Machi 2017 kwamba barabara hii itajengwa. Mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, anakuwa Rais wa kwanza kujenga barabara hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kwa kuridhia barabara hii ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Warufiji wamechoka na maneno, tumebadilisha Wabunge zaidi ya tisa, mimi ni Mbunge wa tisa ukianzia Bibi Titi Mohamed, kule ni miaka mitano mitano na Wabunge wamehukumiwa kwa sababu ya barabara hii ya Nyamwage – Utete. Unaweza ukawa ni Mbunge mzuri sana, ukawa na mchango mzuri sana kama mimi lakini kama tutashindwa kujenga barabara ya Nyamwage – Utete, hatutoki. Katika sehemu ambayo kuna siasa, kule mtu hajasoma darasa hata moja lakini ni profesa kwenye siasa, anayajua tusiyoyajua. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimpongeze Waziri kwa kuridhia lakini kusema peke yake Warufiji wamechoka na maneno. Nimesema sana, Waziri anajua, nimekwenda sana ofisini kwake na yeye ameridhia barabara hii sasa inakwenda kujengwa, Warufiji wanaomba kuona vitendo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameridhia sasa kufungua Pwani ya Kusini, tunakwenda kwenye utalii wa picha, tunakwenda kwenye mradi wa umeme wa Stiegler’s lakini huko kote hatuwezi kufika kama barabara zetu hazitaboreshwa. Barabara ya kutoka Kibiti – Mloka kama haitajengwa kiwango cha lami mradi wa Stiegler’s utachelewa sana, pengine utachukua miaka kumi kukamilika. Kwa sababu ukarabati uliofanywa ambao Mheshimiwa Waziri ameuzungumzia kwenye kitabu chake hiki, ukurasa wa 15, ukarabati ule sasa hivi kutoka Kibiti - Mkongo unatumia saa nne, kilometa 15, niombe Serikali kukarabati barabara hii.

Mheshimiwa Spika, zipo barabara ambazo iwapo zitafunguliwa Pwani kutakuwa kuchele kwelikweli. Nikuombe barabara ya Kisiju – Mkuranga; Vikindu – Vianzi; Nyamwage – Utete nimeshaisema; Ikwiriri – Mloka, Mloka – Kisarawe, Mloka – Kisaki, Utete – Ngarambe, Kibiti - Mloka pamoja na Bungu – Nyamisati. Barabara hizi zikifunguliwa Pwani tutazalisha na tutailisha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna bonde kubwa lenye ekari zaidi ya laki tano ambazo hazijalimwa; watalimaje? Kutoa mazao kutoka shambani kupeleka sokoni tunatumia saa nane au kumi. Niiombe Serikali, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amedhamiria kuifungua pwani, tuifungue pwani kwa kuboresha miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, katika ukurasa wa 15 amezungumzia barabara ya Chalinze, express way. Mheshimiwa ndugu yangu, Mheshimiwa Serukamba, amesema sana, nimuombe Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mchengerwa. Nakushukuru sana kwa mchango wako, umenikumbusha mbali, kweli nayaelewa maeneo haya.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)