Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kushukuru kupata nafasi hii, ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara nyeti ambayo inaongoza mustakabali wa elimu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia katika Sera yetu ambayo iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inazungumzia elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea elimu bure kwa watoto wetu, lakini hii elimu bure imekuwa na changamoto kubwa. Jimbo la Segerea tuna shule 37 na tuna wanafunzi ambao wamejiandikisha kwa sasa ni 8,949. Katika Jimbo la Segerea ukitembelea hizi shule Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe utaona huruma na utashangaa. Najua wewe utasema kwamba, unasimamia sera na hii iko kwa TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ni sera Mheshimiwa Waziri naomba usimamie hizi shule zipate miundombinu ambayo tunaihitaji kwa sababu mwaka 2013 mlikuja na programu ya kila kata kuweka maabara, lakini kabla hamjamaliza maabara zile kuweka vifaa tumekuja na programu nyingine ambayo ni elimu bure, lakini katika hiyo elimu bure tunaanza sasa kutafuta madawati, tunatafuta miundombinu, tunatafuta mambo ambayo sisi wenyewe inaonekana tulikuwa hatujajipanga vizuri. Na hii inasababisha na inaweza ikatuletea matatizo katika elimu yetu na baadaye kuleta matabaka katika elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Segerea kama nilivyosema lina shule 37, lakini kuna madarasa mengine watoto wa darasa la kwanza wako A, B, C, D yaani ina maana kuna wengine wanaingia asubuhi, wengine wanaingia saa 07.00 mchana, wengine wanaingia saa 10.00 jioni, sasa hii yote ni kuwatesa watoto! Mheshimiwa Waziri tunaomba Waziri wa TAMISEMI hili jambo la elimu bure alishughulikie kwa makini sana kwa sababu, tunapoliachia hili jambo tuna miaka tisa na baadaye tutaona madhara yake. Baadaye mtoto atakayemaliza form four atakuwa hawezi kusoma au kuandika jina lake, lakini sisi tutaanza kushangaa kusema kwamba pengine ni wazazi au ni walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu tunawapa mzigo mkubwa. Unakuta mwalimu amesimama anafundisha hana hata nafasi ya kufundishia. Amesimama hapa wanafunzi wameanzia hapa kukaa chini. Mtoto amekaa chini anaandika, hawezi hata kuona anaandika kitu gani. Halafu baadaye tunasema kwamba elimu yetu imeshuka. Elimu yetu inashuka, sisi wenyewe hatuna msingi, hatujajenga msingi mzuri wa kuboresha elimu ya Tanzania.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri kwanza uangalie zile maabara ambazo tumejenga mwaka 2013 mpaka sasa hivi ziko kama mapambo, hakuna kitu chochote kinachoendelea katika maabara zetu. Naomba usimamie hilo ili hizo maabara ziweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine Mheshimiwa Waziri naomba niongelee wanafunzi wahitimu wanaohitimu wanaomaliza shule kutoka vyuo vikuu. Hapa tuna wahitimu wa aina nyingi, lakini wahitimu ambao wamepata mafunzo ya vitendo ni madaktari, wauguzi na walimu. Hatuwezi kufikia uchumi wa kati wakati sisi hatujawaandaa wahitimu wanaotoka vyuo vikuu waje kupambana na kutengeneza ajira na kuajiri watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba sana, pamoja na mkakati wako wa kusema kwamba unaboresha miundombinu ya vyuo na mambo mengine, ningeomba pia uwaangalie na hawa vijana wahitimu wanafanyaje kupata ajira au kujitengenezea ajira kutokana na hiyo elimu yao ambayo wameisoma na sio tu kwamba ni elimu wakimaliza wanakuja huku mtaani, na mtaani tunajua kabisa kwamba, Serikali uwezo wake wa kuajiri hatuwezi kuajiri wahitimu wote, lakini kama mhitimu atakuwa ametengenezewa uwezo wa kujiajiri na kuajiri yeye mwenyewe, basi tunaweza tukapunguza matatizo ya ajira za kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ninataka niongelee ni kuhusiana na changamoto ambazo zinawapata walimu. Walimu sasa hivi ambao wanafundisha shule za msingi, lakini pia na shule za sekondari; kuna walimu wengine wanashindwa kuingia kwenye vipindi kufundisha kwa sababu ya kudai madai yao. Kuna walimu wengine ambao unakutana nao Manispaa hawaelewi wanaenda kumdai nani na kama tunavyosema sasa hivi tunasema Hapa Kazi Tu, lakini mwalimu kama hajapata mshahara wake hawezi kukaa akamfundisha mtoto, inabidi afuatilie pesa zake, ili aweze kula na familia yake.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri uangalie kwanza masuala ya walimu, lakini pia, uangalie miundombinu ya shule pamoja na kwamba inasimamiwa na TAMISEMI, lakini cha tatu uangalie mitaala ya vyuo vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hawa wahitimu wanavyohitimu vyuo vikuu, lakini pia, muwaandae waweze kupambana na soko la ajira kwa sababu sasa hivi huwezi kumlinganisha mhitimu aliyemaliza chuo kikuu cha Tanzania na mhitimu wa chuo kikuu cha nje, obvious huyu wa kwetu hapa atashindwa kwa sababu hajafundishwa kwa vitendo.
Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, najua wewe ni mtaalam na ni mfanyakazi mzuri unaweza ukayasimamia haya mambo na sio mwanasiasa, unaweza ukasimamia vizuri haya mambo yakakaa vizuri ili kesho na keshokutwa tusije tukapata tabaka la watu ambao wamesoma vizuri na watu ambao hawajasoma vizuri ikawa ni matatizo kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.