Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia kwa maandishi hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa ununuzi wa ndege sita, ujenzi wa reli ya mwendo kasi na mambo mengi sana ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia kuhusu barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki (Morogoro Vijijini) kwa kiwango cha lami. Wabunge wa Morogoro tumekuwa tunachangia mara kwa mara na kuambiwa kuwa itatengenezwa lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sikuweza kuiona kama kweli imetengewa fedha. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze wananchi wa Morogoro Vijijini ni lini barabara hii ya Bigwa – Mvuha - Kisaki itajengwa kwa kiwango cha lami na ikakamilika?

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa kutengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 2,020.00 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Dumila – Kilosa – Mikumi sehemu ya Rudewa – Kilosa (km 24). Barabara hii nimekuwa nikiizungumzia mara kwa mara na hasa kipande cha Kilosa – Mikumi. Kipande hiki wakati wa mvua kinakuwa kibaya sana na kupitika kwa shida. Maelezo ya mara kwa mara ni kuwa wafadhili hawajapatikana. Je, ni lini kipande hiki kitatengewa fedha na Serikali au kitapata wafadhili kwa ujenzi wa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, napongeza kwa fedha zilizotengwa shilingi 12,135.00 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Kidatu-Ifakara (Barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha – Songea). Nashauri fedha zilizotengwa 2019/2020 zitolewe zote na kwa wakati kwani mpaka sasa ujenzi huu unafanyika polepole au unasuasua.

Mheshimiwa Spika, Serikali chini ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, imefanya mambo mengi mazuri. Hata hivyo, nakumbushia barabara muhimu sana ya Lupiro – Mahenge – Mwaya kwa ujenzi wa kiwango cha lami. Kwenye hotuba hii sijaona kuwa barabara hii imetengewa fedha. Barabara hii nimekuwa nikiisemea pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ulanga kwani kuna faida zinazopatikana Ulanga kama madini, utalii pamoja na mazao mbalimbali kama mpunga. Naomba maelezo ni lini barabara hii itaanza kuongelewa, kutengewa na kupatiwa fedha na ujenzi wa lami kuanza?

Mheshimiwa Spika, barabara ya Magole – Turiani – Mziha – Handeni. Nianze kwa kutoa pongezi kwa barabara hii, ujenzi wake unaenda vizuri na wananchi wa Wilaya ya Mvomero wanaipenda na kuishukuru Serikali yetu inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru Serikali kwani mradi huu umetengewa shiling milioni 1,170.00 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya barabara ya Turiani – Mziha – Handeni (km104). Naamini kuna wakati barabara hii itakamilika na wananchi wa Mvomero na Handeni watafurahi zaidi kwani miundombinu itakuwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa ujenzi wa reli ya mwendokasi. Wananchi wanaisubiri kwa hamu ikamilike, hasa wa Mkoa wa Morogoro Vijijini, Morogoro Mjini, Kilosa na Mkoa mzima wa Morogoro kwa ujumla. Wananchi waliopisha umeme wa reli hii ya mwendokasi wanaulizia ni lini watalipwa fidia yao? Ni vyema wakaelezwa kwani ni muda sasa umepita tangu evaluation imefanyika.

Mheshimiwa Spika, natoa hongera kwa Mheshimiwa Rais kwa ununuzi wa ndege sita na ukarabati wa viwanja vya ndege unaoendelea. Tuliahidiwa ujenzi wa viwanja vya ndege sehemu za utalii, Mkoa wa Morogoro ujenzi wa kiwanja cha watalii Selou Kisaki (Morogoro Vijijini). Kwa kushirikiana na Wizara husika ya Utalii, nashauri uwanja huu ujengwe.

Mheshimiwa Spika, mawasiliano. Kuna orodha ya vijiji na kata vya wilaya ya Mkoa wa Morogoro ambavyo amepewa Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba wakajengewe minara ili waweze kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, usalama wa usafiri kwenye barabara ya Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma. Kuna magari makubwa/malori mengi na baadhi ya ajali husababishwa na magari haya. Nashauri mwenendo wao barabarani udhibitiwe.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.