Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja hii muhimu kwa uchumi wa nchi yetu, hasa kwenye transport economy. Muda umefika sasa Serikali kuhakikisha inajenga ama kukarabati viwanja vya ndege katika Wilaya zote nchini. Kama bajeti hairuhusu, lazima ihakikishe basi mikoa yote ya nchi yetu ina viwanja vya ndege ambavyo vina hadhi za kupokea ndege za abiria ili kuweza kuharakisha safari toka sehemu moja ya nchi kwenda nyingine.

Mheshimiwa Spika, mfano, Mkoa wa Mara ni mkoa wenye fursa nyingi za kibiashara kama vile samaki toka Ziwa Victoria, biashara ya utalii maana tuna mbuga pale, tuna migodi na zaidi tuna kumbukumbu ya Baba wa Taida ambapo Mataifa mbalimbali wangependa kutembelea na kuweza kuingiza fedha kwenye mkoa wetu pamoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni aibu kwa kweli kuona mkoa ambao ametoka Baba wa Taifa hili na Rais wa Kwanza hadi leo hatuna uwanja wa ndege wenye hadhi na ambao ungepitika kwa maana ya ndege kutua muda wote. Nakumbuka kuna mwaka tulishashindwa kutua pale sababu ya mvua na uwanja ule runway yake siyo ya lami na ilikuwa ni Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikiongelea huu uwanja tangu Bunge la Kumi. Tunaomba sasa fedha ziende ili wale wananchi walipwe fidia na hatimaye uwanja ukarabatiwe na kupanuliwa ili wananchi wa Mara waweze kurahisishiwa usafiri wa kutoka sehemu mbalimbali za nchi kama ndege za Precision Bombadier na hata Dream Liner kutua. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati wa majumuisho atueleze wananchi wa Mara juu ya hatua ya uwanja wa Mara, Musoma.

Mheshimiwa Spika, noamba pia kuzungumzia kuhusu usikivu hafifu wa mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo Wilaya ya Tanze na hasa Jimbo la Tarime Mjini maeneo ya Mofabiri, Nkende ambapo Mheshimiwa Naibu Waziri alifika na kuahidi kushughulikia hasa Kata ya Ketave, Nbende, Ngendoto na Kuyananyori. Vilevile Jimbo la Tarime Vijijini hasa maeneo ya Mpabani, Sirari na kule Nyamundu, ni muhimu sasa hili lishughulikiwe maana tunapata Safaricom ya Kenya.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu round about iliyopo Tarime Mjini ambayo ni junction ya kwenda Sirari, Nyamagana, Mwanza na Soko Kuu. Ile round about inasababisha ajali nyingi sana na hasa kwa wageni maana sehemu ni finyu sana kuweza kuruhusu mzunguko wa magari hasa makubwa (kama lori na mabasi). Pia ukifika unashindwa kujua unaanzia wapi wala unaelekea wapi. Tumeshazungumzia sana hili kwenye Road Boad tangu mwaka 2017 na TANROADS Mara iliahidi kulishughulikia.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kuondolewa ile round about na kuwekwa taa za barabarani ili ziweze kuongoza magari pale kama ile ya Mwenge inavyoruhusu magari ya kutoka Kawe/Lugalo, Mikocheni kwenda Ubungo na kwenda Posta (hii junction ndiyo mfano). Hizi taa zitasaidia kuondoa ajali nyingi sana zinazopoteza maisha ya Watanzania lakini pia zitasaidia kupandisha hadhi Mji wa Tarime ambao unakua kwa kasi sana na upo jirani na nchi ya Kenya.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunaendelea kupata adha ya mtaro hasa kwenye barabara ya Nyamwaga kujaa hasa mvua inaponyesha, mitaro midogo haikidhi haja kabisa. Vilevile, maungio ya barabara za TANROADS kuingia kwenye mitaa zinaachwa bila maingilio kwa barabara nyingine, kukatika kwa mawasiliano kati ya barabara za TANROADS na zile za TARURA.

Mheshimiwa Spika, naomba sana kujengewa daraja la Nyandogo linalounganisha watu wa Kata ya Nyandogo na Bunera pamoja na ukarabati au upanuzi wa daraja la Movi linaloenda uwanja wa ndege wa Magena.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni kuhusu ATCL. Kwanza kabisa ieleweke kuwa naunga mkono uboreshaji wa Shirika la Ndege, ambapo kimekuwa ni kilio changu cha muda mrefu na tunatumia fedha za walipa kodi kulifufua. Naishauri Serikali kuiacha Menejimenti ya ATCL iwe huru kujiendesha kibiashara.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imeshauri vyema. Ili Shirika liwe na ufanisi, Serikali haina budi kuwaacha menejimenti waweze kupanga na kulisimamia Shirika, maana wao ndiyo wana utaalam wa biashara hii ya ndege kuliko sasa wanavyoingiliwa kibiashara, hili Shirika kuendeshwa kisiasa na siyo kibiashara. Ona wenzetu wa KQ, Ethiopia, Emirate, Shirika lolote la operation, mawasiliano na mengineyo.