Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali inachelewesha miradi ya maendeleo ya miundombinu ya Mkoa wa Kigoma?
Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kuendelea kuamini katika maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na hususan Mji wa Kigoma kwa kuwekeza katika ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho pamoja na ujenzi wa Bandari ndogo za Kibirizi na Ujiji.
Mheshimiwa Spika, miradi hii mitatu ikikamilika itawezesha uwepo wa gati katika eneo la mji wa asili wa kibiashara wa Ujiji na kuwezesha ndoto yetu ya kurejesha hadhi ya Ujiji katika maendeleo ya nchi yetu. Mradi wa Bandari kavu ya Katosho utawezesha mizigo ya nchi za DRC, Zambia na Burundi inayopitia bandari ya Dar es Salaam kuchukuliwa Kigoma na hivyo kurahisisha biashara na hichi hizo jirani. Mamlaka ya Bandari pia wanajenga jengo la OSBC (One Stop Center) ambayo itarahisisha shughuli za ukusanyaji kodi, biashara na uhamiaji.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kuwa TRC wanajiandaa nao ili ukamilikaji wa miradi hii uende sambamba na uwepo wa reli ya kusafirisha kwa urahisi mizigo ya Zambia, DRC na Burundi. Mambo haya yataingiza fedha kwenye mzunguko wa uchumi wa Mkoa wa Kigoma na kutoa ajira kwa wananchi wenzangu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mkurugenzi Mkuu wa TPA kwa kuendeleza miradi hii na hii ni ishara ya imani yake kwa ukuaji na maendeleo ya mji wetu na mkoa wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kumpongeza Meneja wa TANROADS Kigoma kwa kuwezesha mikataba ya Barabara ya Manyovu - Kasulu - Kibondo (mpaka Nyakanazi) kupitia ufadhili wa AFDB na barabara ya Uvinza - Darajani kupitia Kuwait Fund. Miradi hii ni muhimu kwa Mkoa wa Kigoma kwa kuwa itauunganisha Mkoa wa Kigoma na Mikoa mingine na kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na shukrani hizo kwa watu wa TPA na TANROADS bado watu wa Kigoma wanalia kwa kuwa ipo miradi yao ya msingi inayokwamishwa na Serikali. Licha ya Jumuiya ya Kimataifa kuelewa umuhimu wa Mkoa wa Kigoma kijiografia na kiuchumi na hivyo kutoa fedha za miradi ya maendeleo itakayochochea shughuli za kiuchumi, Serikali ya CCM imekuwa inavuta miguu kutekeleza miradi hiyo. Nitawapa mifano michache ya namna Serikali ya CCM inavyohujumu Mkoa wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, moja, Serikali ya Japan imeidhinisha mradi mkubwa wa kuboresha Bandari ya Kigoma wenye thamani ya dola za Marekani milioni 40 (karibu shilingi za Kitanzania bilioni 100), lakini kwa mwaka mzima sasa Wizara ya Fedha haitaki kusaini mkataba ili zabuni itangazwe na kazi ianze. Fedha hizi ni msaada, siyo mkopo.
Mheshimiwa Spika, pili, hoja ya Serikali ni kuwa Serikali ya Japan inataka msamaha wa Kodi ya VAT kwenye mradi huu, nayo haitaki. Sasa tunapewa mradi wa shilingi bilioni 100, bure, kisha tunataka na VAT kwenye vifaa vinavyofumika kwenye mradi huo huo kweli! Serikali inaweza kupata mapato mengi mno ya kodi ikiwa mradi huu wa upanuzi wa bandari ya Kigoma utafanyika. Kwa nini waukwamishe kwa mapato kiduchu tu ya VAT ya sasa? Kwa nini Serikali haioni picha kubwa?
Mheshmiwa Spika, tatu, Jumuiya ya Ulaya (EU) kupitia Benki yao ya Uwekezaji (European Investments Bank) wameidhinisha fedha, dola milioni 20 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Kigoma na kuupanua uwanja ili ndege kubwa zitue kwa ajili ya kuunganisha nchi za maziwa makuu na Mji wetu. Tangu mwaka 2018 Januari, zabuni imetangazwa, mpaka leo kazi haijaanza wakati uwanja wa ndege wa Chato ambao haukuwa kwenye Bajeti ya Serikali wala mpango wa maendeleo umejengwa na kukamilika. Serikali inataka kuwaambia nini watu wa Kigoma? Wao sio Watanzania kuliko ndugu zao wa Tabora?
Mheshimiwa Spika, nne, hata miradi ambayo fedha tayari zipo, haifanywi. Kwa mfano, Manispaa ya Kigoma Ujiji tuna mradi mkubwa wa kuweka pavements kwenye mitaa yetu ili kutoa maarifa ya ufundi na kisha ajira kwa vijana. Lengo la mradi huu ni kutumia shughuli za ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana na mzunguko wa fedha kwa wananchi kwa vijana na wanawake kupewa mafunzo ya ujenzi wa hizo barabara za mawe (pavements) na kisha kupitia vikundi vyao kupewa kazi hizo za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imegoma kusaini mkataba wa Mkandarasi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi na usanifu wa mradi huu pamoja na kuwa mfadhili wa mradi, Serikali ya Ubelgiji iko tayari na fedha ziko tayari. Mradi huu ambao ungehusu kata nane za Manispaa ya Kigoma Ujiji ungekuwa ni ‘Game Changer’ kwa uchumi wa Kigoma. Nao unakwamishwa. Kwa nini?
Mheshimiwa Spika, watu wa Kigoma ni wavumilivu sana. Wamevumilia kwa zaidi ya miaka hii 58 ya Uhuru wa Tanganyika na 55 ya uwepo wa Tanzania bila kuunganishwa na mkoa wowote, wakatengwa kiuchumi. Uvumilivu huo una kikomo, hasa ikiwa ni kwa miradi yao ya miundombinu na uchumi inahujumiwa namna hii. Serikali isiwafikishe huko.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Wizara hii ilipaswa ichochee ukuaji wa uchumi, kwa nini uchumi unadumaa?
Mheshimiwa Spika, mgawo wa bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano ni ufuatao: 2016/2017 shilingi trilioni 4.8 ambayo ilikuwa 40.3 % ya bajeti yote ya maendeleo ya shilingi trilioni 11.8. Mwaka 2017/2018 shilingi tirilioni 4.9 ambayo ilikuwa 40.8 % ya bajeti yote ya maendeleo ya shilingi trilioni 11.9. Mwaka 2018/2019 shilingi trilioni 4.1 ambayo ilikuwa 34.5 % ya bajeti yote ya maendeleo ya shilingi trilioni 12.0.
Mheshimiwa Spika, mpaka mwaka huu wa fedha unaoisha 2018/2019 Bunge litakuwa limeidhinisha kwa Wizara hii jumla ya shilingi trilioni 13.8 katika miaka mitatu ya bajeti. Ni wastani wa 38.5% ya bajeti yote ya maendeleo kwa miaka hii mitatu. Tukipitisha bajeti ya 2019/2020 tutakuwa tumewekeza jumla ya shilingi trilioni 40.6 na kati ya hizo shilingi 18.7 zitakuwa zimekwenda Wizara hii ya Miundombinu. Hii ni sawa na 46% ya Bajeti yote ya maendeleo kwa miaka minne kati ya mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Spika, ni halali kabisa kwa Wabunge kuhoji: ajira ngapi za kudumu zimetengenezwa kutokana na uwekezaji huu? Sekta zipi nyingine za uchumi zimechochewa (multiplier effect) kutokana na uwekezaji huu? Kwa Mfano, viwanda vingapi vya chuma vimeanzishwa? Pato la Taifa limeongezeka kwa kiasi gani kutokana na uwekezaji huu? Watanzania wangapi wameondokana na umasikini? Mapato ya Serikali yameongezeka kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, kikawaida ni Bajeti ya Wizara hii ndiyo ambayo matumizi/manunuzi yake hutumika kuchochea shughuli za kiuchumi na kupeleka fedha kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi. Hali iko hivyo duniani kote, lakini hapa nchini kwetu hali ni tofauti, manunuzi mengi ya ujenzi yanayofanywa kupitia Wizara hii hayajachochea ukuaji wa uchumi, bali namna yalivyofanyika yamekuwa ni sababu ya kudumaza uchumi.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ilirithi Bajeti ya Serikali ya Awamu ya Nne ya Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ilipoingia madarakani Novemba 5, 2015. Katika wakati husika kasi ya mzunguko wa fedha nchini (M3) ilikuwa ni 15%. Hivyo kila shilingi nchini ilibadilisha na wastani wa mikono 15 kwenye matumizi ya kiuchumi. Ripoti ya BOT ya Mwezi Machi, 2019 (inayoelezea hali ya Februari, 2019) inaonyesha kuwa M3 kwa sasa ni 3% tu. Mzunguko wa fedha umepungua mno.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mitatu tumepitisha Tanzania Shillings 1.5 trillion kununua ndege. Fedha zote hizo zimekwenda nje ya nchi, hakuna hata shilingi moja kati ya hizo ambayo imerudi nchini. Hiyo ni moja ya sababu ya kupungua kwa mzunguko wa fedha nchini.
Mheshimiwa Spika, tuna ujenzi wa SGR. Mkataba wa Ubia Kati ya Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki na kampuni ya Construção Africa SA ya Ureno, naambiwa Kampuni hii imejitoa kwenye mkataba huu na kwamba kuna Kampuni nyingine iko kwenye huu mradi. Ikumbukwe ni hiyo kampuni ya Ureno ndiyo yenye uzoefu wa ujenzi wa reli. Je, mbia mpya wa Yapi Merkezi ni Nani? Uwezo wake ukoje? Tumefanya Due Diligence ili mambo ya Indo Power ya kwenye korosho yasijirudie? Taifa linapata nini?
Mheshimiwa Spika, tumerudia makosa tuliyoyafanya wakati wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam. Mwezi Septemba, 2012, Wizara ya Fedha kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Exim ya China walitiana saini makubaliano ya mkopo wa miaka 33 yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.225 kwa riba ya 2% kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi linalounganisha eneo la Msimbati na Mnazibay mpaka Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Kampuni zilizoshinda zabuni ya ujenzi huu ni China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC) na China Petroleum Pipeline Engineering Corporation (CPPEC), ambapo kila kitu kilichotumika kwenye ujenzi wa bomba hili kilitoka China na hakuna ushahidi wa kitaalam wa ujenzi huo ulioachwa nchini. Ndicho tunachofanya kwenye SGR. Mbaya zaidi kwa sasa tunatoa hela ndani kupeleka Uturuki na za nje tunazozikopa ni kutoka mabenki ya kibiashara yenye riba kubwa.
Mheshimiwa Spika, reli inahitaji chuma na chuma cha pua (Iron and Steel), mbao ngumu, wahandisi na mafundi mchundo wengi, vifaa vidogo kama screws na kadhalika. Je, Serikali imefungamanisha ajenda ya viwanda na ujenzi wa reli? Serikali inaweza kutuambia viwanda vingapi vya ugavi kwenye bidhaa za ujenzi wa reli vimejengwa?
Mheshimiwa Spika, viwanda vingapi vya mataruma vimejengwa nchini? Tunaagiza mataruma na hata screws za kufungia mataruma kutoka nje ya nchi. Ndiyo maana trilioni zote hizi tunazoipa Wizara kwa miaka hii mitatu hazisaidii ukuaji wa uchumi.