Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, Wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ina majukumu yanayogusa sekta kama tatu zenye kuwezesha maendeleo ya nchi na wananchi. Katika aya ya 26 ukurasa wa 15, Waziri ameeleza ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze, kilomita 144 haujaanza kutokana na maamuzi ya Serikali kusogeza mbele utelekezaji wa mradi huu ili kukamilisha kwanza miradi hii inayoendelea, ni vyema katika majumuisho Serikali ikaeleza imesogeza mbele mradi huu mpaka lini.
Mheshimiwa Spika, aidha, ni kwa nini Serikali imeamua kusogeza mbele wakati ambapo imesema mara kadhaa kwamba mwaka 2011 kwamba mradi huu ungetekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) na ungekuwa na barabara za kulipia ili kurejesha gharama za ujenzi ambazo zingeingiwa na sekta binafsi katika ujenzi.
Mheshimiwa Spika, katika aya ya 44, ukurasa wa 24, Serikali ieleze sababu ya barabaa za Kimara - Korogwe Maji Chumvi (kilomita tatu) na sehemu ya Goba - Madale (kilomita tano), ujenzi wake kwenda taratibu. Aidha, ni kwa nini Serikali imechukua kipande kidogo tu cha Mloganzila – Kisopwa (kilomita moja) kati ya kilomita 14.66 za barabara ya Kibamba – Kisopwa – Kwembe - Makondeko. Kwa kasi hii ndogo itachukua miaka takribani 14 kwa barabara hiyo kukamilika.
Mheshimiwa Spika, katika aya ya 54, ukurasa wa 30, imeelezwa kuwa ujenzi wa barabara ya juu (interchange) katika barabara ya Ubungo umefika asilimia 28. Hii inaonesha kwamba kasi ya ujenzi ni ndogo sana. Wizara ikumbuke kwamba mwezi Machi, 2017 wakati na uzinduzi wa ujenzi Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba ujenzi wa barabara ya juu ya Ubungo ukamilike ndani ya miezi 30. Kwa agizo hilo ujenzi unapaswa kukamilika mwezi Agosti, 2019, hivyo kwa asilimia 28 mwezi Mei ni kiwango cha chini sana cha utekelezaji. Hivyo Wizara itoe maelezo ni mikakati gani imewekwa kuharakisha ujenzi ili ukamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwenye aya ya 60, ukurasa wa 33, Waziri ameeleza kuwa upanuzi wa barabara kwa njia nane kwa sehemu ya Kimara - Kiluvya (kilomita 19.2) unaendelea ambao utarahisisha pia upanuzi wa Madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji. Hata hivyo, Waziri hajaeleza ujenzi wa barabara umefikia hatua gani, eneo ambalo ni vyema akalieleza katika majumuisho. Katika kipindi cha uzinduzi uliofanywa na Rais ambapo walishiriki, kasi ya ujenzi kabla na baada ilikuwa kubwa. Hata hivyo, kwa sasa kasi imepungua, hivyo ni vyema Wizara ikafuatilia kwa karibu kuwezesha ujenzi kufanywa kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, aidha, naomba mkandarasi kama alivyofanya kwa eneo la Kibamba CCM kusawazisha eneo kwa ajili ya kituo cha muda cha daladala afanye hivyo katika eneo la Kiluvya. Eneo la kusimama daladala lilishawekwa, Wizara ihakikishe SUMATRA inasimamia daladala zifike Kiluvya badala ya kuishia Kibamba CCM na kufanya wananchi wa Kiluvya waingie gharama kubwa za kupanda mabasi yanayokwenda Kibaha, Mkoani Pwani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Rais kuhusu fidia ya wananchi kupisha ujenzi wa barabara hii, naomba Wizara irejee hukumu ya kesi ya wananchi wa Mbezi ambao walifungua kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ambapo mahakama ilitamka wananchi wanastahili fidia.
Mheshimiwa Spika, katika aya ya 73, ukurasa wa 40, kwenye hotuba ya Waziri amezungumzia kuhusu miundombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya pili hadi ya tano. Naomba majibu ya Serikali katika majumuisho ni awamu ipi hasa ya ujenzi itahusisha ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kwa kipande cha kutoka Kimara mpaka Kiluvya?
Mheshimiwa Spika, ili kutoiingiza nchi kwenye gharama kama iliyotokea katika maeneo mengine ambapo lami na miundombinu mingine imelazimika kuvunjwa kuwezesha kujengwa kwa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka, ni vyema upanuzi wa sasa wa barabara ya Morogoro kutoka Kimara mpaka Kiluvya ukahusisha pia ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umekuwa ukikabidhiwa ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali. Kati ya kazi ambazo TBA imefanya hivi sasa ni pamoja na ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya Mpya ya Ubungo. Naomba TBA iharakishe kukamilisha ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya. Aidha, naomba TBA izishauri mamlaka zinazohusika ili ujenzi huo unaofanyika katika Kata ya Kwembe, Mtaa wa Luguruni uhusishe pia ujenzi wa Ofisi ya Mbunge ambayo katika michoro ya sasa haijawekwa.
Mheshimiwa Spika, TBA pia ikutanishwe na Shirikia la Nyumba (NHC) kujadiliana kuhusu uendelezaji wa Mji wa Viungani (Satellite Town) wa Luguruni ili majengo ya Serikali na nyumba za viongozi katika eneo hilo TBA ifuatilie kwa karibu ujenzi uanze. Serikali ililipa muda mrefu fidia katika eneo hilo lakini shughuli za uendelezaji zimesimama.
Mheshimiwa Spika, juu ya kasma 4138 ya kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam (De-congestion of Dar es Salaam Roads) kipande cha Goba - Makongo kilomita nne kimetengewa milioni 310 tu ilihali kuna kipande cha barabara ambacho kwa muda mrefu hakijawekewa lami. Naomba kiwango cha fedha kiongezwe kuwezesha eneo lote lililobaki kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwenye kasma 4161 kuhusu Madaraja ya Juu (Dar es Salaam Road Flyovers) kwa upande wa Ubungo Interchange zimetengwa milioni 145 tu kwa upande wa fedha za ndani. Napendekeza kiwango kiongezwe kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye mkataba.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kasma 4132 juu ya fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali katika kutekeleza miradi ya mkoa barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi yenye kilomita mbili umetengewa katika bajeti milioni 60 peke yake wakati barabara hii ina hali mbaya. Naomba TANROADS watembelee barabara hii na kufanya matengenezo yanayostahili. Hali iko hivyo pia kwa barabara ya Goba – Matosa - Temboni.
Mheshimiwa Spika, katika kasma 2326 kumetengwa milioni 150 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina (feasibility study and design) kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya juu (interchange) Mbezi mwisho kuelekea eneo kutakapojengwa kituo cha mabasi ya mikoani. Naomba mchakato huu uharakishwe ili uende sanjari na ujenzi wa kituo unaoendelea pamoja na upanuzi wa barabara kuwa njia nane.
Mheshimiwa Spika, fedha za Mfuko wa Barabara zitatumika pia kuboresha kwenda DSD barabara ya Kunguru - TATEDO (kilomita tano) ambapo kumetengwa milioni 120. Naomba hatua hiyo iende mbele zaidi kwa kujenga daraja katika eneo la Muungano, Kata ya Goba katika sehemu inayounganisha na Salasala.
Mheshimiwa Spika, katika kiambatisho namba 5(B-2), ukurasa 381, Waziri ameeleza barabara ambazo zitafanyiwa marekebisho ya muda maalum (period maintenance) kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara. Hata hivyo, katika orodha hiyo hakuna hata barabara moja ya Jimbo la Kibamba kwenye Kata sita za Kwembe, Msigani, Mbezi Luis, Goba, Saranga na Kibamba. Hivyo ni vyema Wizara ikaongeza katika orodha hiyo barabara muhimu za Jimbo la Kibamba zenye kuunganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na zenye kuunganisha Wilaya ya Ubungo na Wilaya za Kinondoni na Ilala katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kati ya barabara ambazo ni muhimu TANROADS ikazichukua na kuzifanyia matengenezo ya haraka ni Temboni kwa Msuguri – Msingwa ambayo inaunganisha mpaka Wilaya ya Ilala. Kihistoria, barabara hii TANROADS iliwahi kuitengeneza lakini baadhi ya wananchi wakaenda mahakamani miaka mingi nyuma hali iliyofanya TANROADS kuacha kuihudumia kwa muda mrefu. Mgogoro huo umemalizika lakini TANROADS na TARURA bado wanarushiana mpira mpaka sasa kuhusu kuihudumia. Pamoja na kuwa TARURA wameanza matengenezo madogo, naomba barabara hii ichukuliwe na TARURA ili ifanyiwe matengenezo makubwa na hatimaye ijengwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwenye sehemu (b) juu ya barabara za mikoa za changarawe/udongo. Matengenezo ya barabara zilizopo kwenye Jimbo la Kibamba yamekuwa yakifanyika lakini sio kwenye kiwango cha kuridhisha. Barabara hizo baadhi zimetajwa kwenye ukurasa wa 39o za Kibamba Shule – Magoe Mpiji na Makabe Junction – Mbezi Msakuzi. Naomba katika majumuisho, Serikali ieleze ni lini itafanya matengenezo yenye kiwango. Pia kwa barabara kutoka Mbezi kupitia Mpiji Magoe – Mabwepande mpaka Bunju. Barabara ina vipande kadhaa ambavyo viko kwenye hali mbaya ikiwemo kipande cha barabara kilichomo ndani ya Pori la Akiba la Pande.
Mheshimiwa Spika, Wakaguzi watembelee barabara hii na matengenezo yafanywe. Kwa upande mwingine, Serikali ieleze ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Serikali iliahidi miaka ya nyuma.
Mheshimiwa Spika, kwenye kiambatisho namba 5(D- 2) juu ya matengenezo makubwa ya madaraja na makalavati (bridge major repair) kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara. Nashukuru kwa kalavati (box culvert) la Msakuzi katika barabara ya Kibamba Shule – Mpiji Magohe limejumuishwa na kutengewa milioni 340. Naomba ujenzi wa box culvert hilo ufanyike kwa haraka. Aidha, naomba maelezo ya Serikali ya sababu za Kibwegere box culvert kutengewa shilingi milioni 10 tu.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya uchukuzi, Serikali ihakikishe ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (SGR) unatumia kwa kiasi kikubwa malighafi kutoka ndani ikiwemo matumizi ya chuma kutoka Mchuchuma na Liganga ili kuhakikisha sehemu kubwa ya fedha zinabaki katika mzunguko wa ndani. Kamati za Kisekta zinazohusika zipewe nafasi ya kuangalia Mikataba mikubwa ya Ujenzi na Uchukuzi ili kuhakikisha maslahi ya kiuchumi ya nchi yanalindwa kikamilifu.