Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na pumzi na kusimama hapa. Pili nikishukuru chama changu kwa kuniwezesha pia kuwa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda na mimi nichangie katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Elimu ni kila kitu katika Taifa hili la Tanzania na Taifa lolote duniani. Elimu ni suala nyeti na ni suala ambalo linaigusa Taifa. Hata katika dini zetu suala hili limetiliwa mkazo, nikirejea katika dini yangu ambayo mimi ni muumini, dini yangu ya kiislamu tumeamrishwa kutafuta elimu hata kama ni China na vilevile elimu ni faradhi kwa muislamu wa kike ama wa kiume, na hata katika dini zote nadhani suala hili limetiliwa mkazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala hili limetiliwa mkazo katika dini zote na katika tamaduni zote, ni muhimu pia na Walimu tuwape umuhimu huo huo. Imekuwa ni rahisi sana kwamba walimu hatuwatendei haki katika Taifa hili, Walimu wanapata matatizo mengi kusomesha watoto wetu, wanajitahidi kufundisha watoto wetu kihaki lillah! Leo hii ndiyo tunaodharau Walimu hao, leo hii hatuwasikilizi mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu ambaye anakupa kitu muhimu; hivi mtu ambaye anakuthamini, wewe huwezi kumthamini, ni kwa nini? Hiyo siyo haki na hatuwatendei haki kama inavyopaswa. Walimu hao hao leo wanapodai madai yao Serikali inawawekea kitimoto. Aidha, wanapoandamana wataweza kufukuzwa kazi, ama kitimoto cha aina yoyote cha kuweza kuwadhalilisha hao Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipowathamini Walimu wetu, hivi tutawathamini nani wengine?
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Kwa sababu Walimu hawa ni muhimu katika kila sekta. Wewe usingekuwa kiongozi kama hukupitia kwa Mwalimu, asingekuwa daktari kama hakupitia kwa Mwalimu, asingekuwa Rais kama hakupitia kwa Mwalimu. Sasa inakuwaje tunawakandamiza na kuwadhalilisha? Mwalimu huyu anasomesha miaka 50, lakini leo ukienda hana hata mahali pa kukaa. Hii ni haki? Ni kweli tunawatendea haki? Mwalimu huyu anasomesha miaka 50, hana uwezo hata wa kumiliki baiskeli. Lazima Taifa hili likae, litafakari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoamini ni kwamba Mwalimu ni mtu wa pili baada ya mzazi na anaweza kutoa radhi zikatufika. Naamini katika mwelekeo huo huo, ni kwamba mambo mengi hatuendelei kwa sababu tumewadharau Walimu. Tutapanga mikakati, mipango ya kila aina lakini hatutaendelea kwa namna hii na style hii tunavyowafanyia Walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee hapo hapo!
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tuliambiwa walimu wanatarajiwa kuajiriwa mnamo mwezi wa Tano, sasa tunaingia mwezi wa Sita, Walimu hawajaajiriwa. Naiuliza Serikali, itawaajiri lini Walimu ambao wamekwisha kwenda kuchukua mafunzo? Walimu ambao wamejitolea, ambao wamesoma pengine hata mikopo wamekosa; angalau wafute jasho lao kwa kupata hiyo ajira, kwa sababu elimu yetu haikuandaliwa kwamba unapomaliza shule ujiajiri mwenyewe, hiyo haipo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linguine, nizungumzie suala la elimu kwa upande wa Zanzibar. Suala la elimu kwa upande wa Zanzibar ni tete na ndiyo maana ikawa wanafunzi wa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita wanafeli sana. Hapo mwanzo nilidhani kwamba pengine elimu ya Form Four mpaka „A‟ level kwa kule Zanzibar labda ni elimu ya juu, kwa sababu suala ambalo linahusiana na Muungano ni suala la elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, wanafunzi wa Form Four wanafanya mitihani inayotungwa Tanzania Bara na siyo Tanzania Zanzibar. Mitaala hiyo inacheleweshwa, ndiyo maana watoto wengi wanafeli. Wakati mwingine mwingine anaulizwa pengine habari za pamba, kule Zanzibar hajaiona, wala hajaijua, naomba kuwasilisha.
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuwasilisha.