Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwanza kwa kupata nafasi ya kuweza angalau kujadili hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kwanza kabisa napenda kutoa kilio changu cha wana wa Ludewa, kwa sababu Ludewa sasa inaonekana ni eneo ambalo limesahaulika kwenye mambo mengi. Hivi ninavyoongea sasa, Jimbo la Ludewa lina uhaba wa Walimu 496, tuna shule 108; katika shule hizo 108 ni shule saba tu ndizo ambazo zina Walimu wanaoweza kukidhi. Shule nyingine zote 101 zina Walimu wanne kushuka chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ambayo ina Walimu wawili na shule zilizo nyingi zina Walimu watatu. Kwa hiyo, cha kwanza napenda tu kutoa masikito yangu kwamba tuna uhaba wa Walimu 496 na bahati mbaya kabisa katika kipindi hiki mmetupatia Walimu 30. Hata hivyo kuna Walimu 25 ambao wanastaafu Septemba na kupelekea uhaba wa Walimu 521.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuwasiliana na TAMISEMI, sasa napenda kutoa kilio hiki kwako Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe ndiye msimamizi wa elimu Tanzania. Kwa hiyo, naomba tu mwisho wa siku nikuletee majina kwa watu ambao wanataka kwenda kufundisha Ludewa na ikiwezekana basi mfanye utaratibu mtuletee Walimu. Kwa kweli hali ni ngumu na ndiyo maana nimeamua nije nizungumze katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hata vyuo vyetu vikuu havipeleki wanafunzi kwenda kufanya field kule, kwa sababu ya miundombinu mibovu ya barabara na miundombini mibovu ya mashule yetu, kiasi ambacho kimepelekea hata wanafunzi wenyewe wanaotoka kule kuomba msaada huo. Kwa hiyo, naomba nikuwasilishie hilo na hasa Chuo Kikuu cha Dodoma, kwamba hawawezi kupeleka Ludewa, lakini maeneo mengine yote ya Tanzania wanafunzi wanaweza kwenda kufanya field. Hii inapelekea shule zetu za Ludewa kuwa na pass ya chini kabisa na vijana wetu wengi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda ku-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule. Nianze na ada elekezi. Nadhani shule hizi za binafsi ndiyo zinazoleta fundisho kwa Serikali yetu kwamba ni namna gani shule zinapaswa ziwe na ninadhani zimeshaweka standard ya kuweza ku-move. Kwa hiyo, sababu ya kuweka ada elekezi, siyo za msingi na wala hazifai. Ninajiuliza swali, tusingekuwa na shule za private, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya na Uganda. Je, kule Uganda tungeweza kupeleka hizo ada elekezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suppose huku tungekuwa hatuna na kipindi kile kabla ya St. Marys kuanza, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya. Kwa hiyo, kosa letu ni kuboresha elimu, kutengeza miundombinu mizuri, mpaka inapelekea kuwa tunaongoza kwa hamsini bora. Hilo ndiyo kosa ambalo Serikali imeliona. Nadhani Serikali ingeshukuru, kwa sababu ninaamini kabisa wanafunzi wengi ambao wanang‟ara ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, ni wale ambao wanatoka private school, wanatuwakilisha. Kwa hiyo, tungewatengenezea miundombinu mizuri, ikiwezekana hata kuchukua mishahara mlipe nyie Serikali, kwa sababu watoto wanaofundishwa ni watoto wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sababu zile za msingi kupelekea kuweka hizo ada elekezi hamna. Kwa sababu usi-justify makosa unayoyafanya, usi-justify kutokuweka jitihada zozote ili uweze ku-capitalize kwenye shule za binafsi. Play your part, fanya shughuli zako, ninaamini ukitengeneza miundombinu mizuri, ukiwa na Walimu wa kutosha, hakuna mtu atakayeenda kwenye shule zenye gharama kubwa. Kwa hiyo, isifike kipindi Serikali inashindwa kufanya wajibu wake, kwa madai tu iende ika-suppress kwenye hizi shule za binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi ziachwe ziendelee, kwa sababu yale mazingira yaliyowekwa vizuri, wamiliki wa shule wengi wamekopa mikopo, wana madeni yenye riba kubwa. Kwa hiyo, maana yake utakaposema unatoa ada elekezi, tutashindwa kulipa yale madeni na mwisho wa siku sasa wakati huku tayari shule za private zimeshakaa vizuri, tunabomoa wakati huku kwetu kwenye government schools hatujaparekebisha bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya ujenzi wa Shule ya VETA Shaurimoyo, katika Jimbo la Ludewa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hajaiweka kabisa. Shule hii ya VETA kimsingi ilikuwa inaanzishwa pale kwa ajili ya kupokea miradi mikubwa miwili ya makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga, kuwaandaa vijana kwenye shughuli za kiufundi ili kuweza kushiriki katika hiyo miradi inayokuja. Nakumbuka mwaka 2012; kama siyo 2012, ni mwaka 2013, Serikali iliji-commit kwamba itajenga chuo hiki. Naamini sababu zile zile za kukitaka kukijenga hazijatoweka, sababu hizo zipo. Mlipeleka wataalam, ardhi imepimwa, hati mmepata, michoro mnayo, BOQs zote mnazo na mlisema mlishatenga hela kwa ajili ya kujenga hicho Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza tena swali hili, Chuo hicho kwanini kimeachwa? Matokeo yake, vile ambavyo wala havikuwepo katika kipindi hicho cha miaka miwili, mitatu iliyopita, leo ndiyo vimewekwa. Sasa watu wa Ludewa wanajiuliza maswali ya msingi, pana tatizo gani? Kwanini kisijengwe na kwanini hakuweka kwenye program yake? Kwenye hili Mheshimiwa Waziri hatutakubali kwa sababu kinachoonekana ni kuibagua Ludewa na Ludewa haitaweza kubaguliwa kwa sababu na yenyewe ipo katika nchi ya Tanzania.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja lakini tunaomba Chuo Ludewa.