Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi hili na pia sitomsahau Mkuu wa Jeshi la Nyuki Zanzibar ambaye kwa umahiri wa kazi zake anavyozifanya pamoja na viongozi wote wa Jeshi mliokuja hapa Bungeni leo, hongereni kwa Waziri wenu alivyotoa hotuba yake vizuri, hotuba yake ndogo lakini imeeleweka na imefahamika na tumeielewa vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nataka kuzungumzia nyumba za makazi za wanajeshi Zanzibar. Nyumba ziko chakavu za muda mrefu ukiangalia tuliokuweko Brigedi ya Nyuki pale Zanzibar, tayari ni chakavu za zamani toka Mapinduzi walivyozijenga, ukija Mtoni unakuta hivyo hivyo, ukienda Mwanyanya na kwingine kote, angalau mngezifanyia ukarabati zikaridhisha angalau na wanajeshi wakaweza kukaa pahala wakatulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiendelea utaangalia kwamba hizo Kambi zenyewe tayari ziko uraiani, ukija Brigedi ya Nyuki imezungukwa mpaka nyuma yake kuna soko, ukija Mwanyanya imezungukwa na raia, ukija Mtoni tena pale ndio imekuwa mashaka maana kuna mtu amejenga ameingia ndani ya Kambi ambaye ni mtu maarufu ambaye tuna wasiwasi mtu maarufu akikaa pahali kama penye Jeshi ni tatizo kwa kweli. Sasa ningeona lazima muweze kujipanga. Sikwambieni muhame kwa sababu nikisema muhame kwa Zanzibar ile mnakwenda wapi, lakini inabidi muweze kutoa elimu ya kutosha kwa wale wanaokaa pale na tuchukulie isije ikatokea kama yale yaliyotokea Mbagala inatakiwa mtoe elimu, muwaeleweshe, muwape mipaka yao wanatakiwa wanafika wapi na wapi ili kuimarisha ulinzi wa Kambi zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja lingine kuhusu malipo ya fidia ya maeneo yaliyotwaliwa au yaliyochukuliwa na Jeshi, ukurasa wa 30 umeelezea na nimeshukuru kwamba umesema Kigoma kule tayari mmelipa, na kule Lindi tayari mmelipa ambapo hili ni mwanzo mzuri na hayo mengine waliobakia wanadai fidia zao mjitayarishe nao muwalipe kwa sababu mtu akianza uzuri amalizie uzuri na kwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali walituarifu kwamba JKT na JKU wataweza kupata ajira ya Jeshi na ninajua hivi karibuni kama nilimsikia Mheshimiwa Rais akilizungumza hilo. Sasa nilikuwa nataka kujua hatua aliyofikia katika ajira hiyo wamefikia hatua gani, tunataka kujua pia na fedha hizo za kuajiri hao vijana wetu wanazo, kwa sababu ukiwaajiri vijana kutoka JKT na JKU unapata vijana wazalendo. Kwa sababu kule Jeshini wanafundishwa somo la uzalendo, ukakamavu na heshima, sasa ukipitia kwenye misingi ya kuwachukua wao unapata watu waliobora na watoweza kuliheshimu Jeshi na kuwaheshimu raia wao na kuheshimu utendaji wao wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija suala la haki za wastaafu wanaomaliza muda wao wa kazi wanajeshi. Unajua kwa wale waliokuweko Zanzibar wakati wanapomaliza wakistaafu wanapata shida kwenda Bara kufuatilia mafao yao na nilishazungumzia mara nyingi. Kwanza inapendeza unapostaafu unapewa chako kabisa, ki-cheque chako mkononi, unaondoka. Maana hii kumpeleka mara kaenda Bara kufuatilia mara karudi unamtia umaskini, kwa sababu pesa yenyewe hana na kwenda na kurudi unamuongezea umaskini.

Sasa Mheshimiwa Waziri nataka akija aniambie ile Ofisi ya Zanzibar itashughulikia pensheni kwa waliokuweko Zanzibar vipi ipo au itaanzishwa au mnachukua hatua gani au bado waendelee kupata usumbufu na kuhangaika kwenda huku na huku? Ningeomba na hilo nilijue Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja la mwisho mambo ya michezo, michezo ajira, michezo ni afya, michezo maingiliano baina ya upande huu na upande huu na tuna michezo yetu ya aina mbalimbali na ninyi mnao vijana wenu mahiri wa JKT na JKU, kwa nini hao hamuwafanyi ndio vijana wa Taifa? Kwa sababu tayari wana umahiri, mnawafundisha michezo, wana uwezo ili watakapokuwa mkiwapeleka kwenye Kambi zetu za michezo mpira kitaifa, riadha kwenda mbio, hebu liangalieni na hili badala ya kuokota vijana hatukatai vijana mitaani kuwa mnakuwa nao lakini ingekuwa jicho lenu kubwa mnalenga hawa vijana ambao mmewasomesha JKT na JKU. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naunga mkono hoja. (Makofi)