Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. KANALI MASOUD ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuendelea kuliamini sana Jeshi letu katika kuwapa kazi mbalimbali licha ya ulinzi walionao, lakini bado wanaendelea kutekeleza majukumu mengi ya Taifa letu na kupunguzia gharama kubwa ya matumizi ya fedha za hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi tunaochangia tunazungumzia habari ya ulinzi, lakini nafikiri wengine hatuna taaluma ya ulinzi sana ndio maana tuazungumza mazungumzo ambayo hayalingani. Dhima ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi la Tanzania ni kuhakikisha usalama wa Taifa letu na wao wana jukumu la kuhakikisha adui kama yuko ndani, kama yuko nje ni jukumu lao kuhakikisha ulinzi wa Taifa hili. Sasa leo tunapokuja kuwaambia kwamba wao waende tu kule mpakani wakakae huku ndani si kazi yao, hii si sahihi. Lazima ifahamike kwamba ili wao wahakikishe wanalinda Taifa hili lazima wahakikishe adui wa ndani, adui wan je wote ni jukumu lao kwa Taifa. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. KANALI MASOUD ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilifikiri tukisimama hapa tutaendelea kulipongeza Jeshi la Wananchi kwa kazi kubwa wanayoifanya na hili ndio nalofikiria. Lakini leo tunapokuja hapa tukawaambia wamekwenda kuchukua korosho, wameoka shilingi ngapi we chukulia wameokoa shilingi ngapi nchi hii katika kazi hiyo waliyoifanya, lazima tuwaeleze ukweli wenzetu wanafanya kazi ya kujituma na ya kuhakikisha Taifa liko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uimara wa Jeshi lolote duniani likiwepo la Tanzania kwanza lazima liimarishwe katika baadhi ya nyenzo zake. Kwanza kuimarisha wapiganaji wenyewe kwa maana ya afya, nidhamu na mafunzo na kadhalika. Pia liimarishwe kwa zana za kisasa za kijeshi ambazo nazo ni gharama pia zinatakiwa zifanyiwe service, maintenance na vitu vingine kwa gharama kubwa. Kwa hivyo vyote hivyo viimarishwe lakini pia kuimarishwa kwa maslahi yao wenyewe askari, pia ni jambo muhimu, vitu vitatu hivi vikichanganywa Jeshi lolote duniani litakuwa imara na litafanya kazi kwa ueledi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza hapa katika muundo wa majeshi ya duniani katika nchi nyingi duniani ikiwepo Tanzania askari wastaafu wa jeshi pia linakuwa ni Jeshi la Akiba.

Kwa hiyo nilikuwa nataka niiombe Serikali iendelee kuangalia jinsi gani ya kuwawezesha wastaafu, kuwaongezea pensheni yao ili wawe imara ili wakati wowote tukitaka kuja kuwatumia wawe bado wana nguvu zinatosha za kuweza kuwatumia na mifano hai ipo katika vita vya Uganda, wanajeshi waliokuwa wamestaafu walichukuliwa wale ambao walionekana hali zao bado ni nzuri walitusaidia katika vita vile. Naomba Serikali sana iliangalie hili na kuwafikiria wanajeshi wastaafu kuwaongezea pensheni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumza ni mipaka ya kambi yetu ya majeshi bado kumekuwa na malalamiko makubwa sana, uingiliano kati ya raia na wanajeshi na mara nyingi tunapouliza ndani ya Bunge hili tunaelezwa hali halisi kwamba fedha za kulipa fidia na mambo mengine na upimaji wa maeneo bado hazitoshi. Naiomba sana Serikali iendelee kuhakikisha inawasaidia wenzetu Wizara ya Ulinzi kuwapatia fedha za kutosha kuhakikisha wanapima makambi yote na kulipa fidia katika yale maeneo ambayo tayari yamekwishapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumza ni kuhusu Shirika la Nyumbu na Shirika la Mzinga, tunaamini kama Jeshi ni watu wanaolinda Taifa tu, lakini mimi naamini Jeshi bado linaweza likatoa ajira, pia linaweza likachagia fedha kupitia mashirika haya. Tumeyashududia tumeona wenyewe kabisa mfano Shirika la Mzinga wana uwezo wa kuzalisha bidhaa ambazo zinahitajika nchi za nje, lakini bado mashine zao, vifaa vyao walivyonavyo ni vya teknolojia ya zamani na vingine ni vimechoka naomba pia Serikali iendelee kuangalia sehemu hizi mbili ili kuwasaidia sasa waweze kuzalisha lakini pia kukidhi mahitaji yao ya ndani ili waweze kufanikisha malengo yao waliyoyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)