Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia mimi na Watanzania wote afya njema. Na pia nawatakia waislam wa Tanzania na duniani kwa ujumla mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JWTZ na JKT ni majeshi yetu ya ulinzi wa nchi yetu ya Tanzania na kwa muda mrefu yamekuwa yakifanya kazi katika mazingira magumu katika kutekeleza majukumu yao. Kwa kuwa Tanzania bado ni nchi maskini na bajeti yetu haijitoshelezi na tunategemea sehemu ya bajeti yetu toka kwa nchi wafadhili ambapo fedha haziletwi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi letu pia linatumika vizuri wakati wa majanga mbalimbali kama mafuriko, tetemeko la ardhi, ujenzi wa madaraja na barabara wakati wa athari za mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya JWTZ na wananchi; jina la Jeshi letu linajieleza kuwa ni la wananchi wa Tanzania lakini katika siku za karibuni kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na wananchi, na katika kitabu cha hotuba ya Waziri imezungumzia ukurasa wa 29 hadi 30 imeeleza kuwa limedhibiti maeneo ya Jeshi kwa kuboresha mazingira kwa kupanda miti na kusimika nguzo na pia kulipa fidia maeneo ya Ras Mshindo (Lindi) shilingi 3,005,697,801.00 na Kakonko (Kigoma) shilingi 550,000,000.00, napongeza hatua hii. Lakini katika Jiji letu la Tanga upo mgogoro wa Jeshi na wananchi katika Kata za Masiwani Shamba na Tangasisi, naiomba Wizara imalize mgogoro huu kwa kulipa fidia wananchi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi Na. 4 (1999) inasema; “whether you have title deed or not so long you have been there for long time, customary law recognizes you as the owner of the land.” Naomba kupitia sheria hii na Wizara wawalipe wananchi fidia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano na majeshi mengine duniani; napongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Jeshi letu na majeshi mengine katika nchi za Bara la Afrika, Ulaya, Marekani na Jumuiya za Kimataifa kama NATO na United Nations. Vyema tukatoa kila aina ya ushirikiano katika mafunzo na mazoezi mbalimbali kwani Jeshi letu pia huvuna uzoefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao kwa wanajeshi wastaafu; kumekuwa na tabia wanajeshi wetu wanapostaafu au wanapopandishwa vyeo kucheleweshewa malipo yao ya kustaafu na malipo ya kupandishwa vyeo. Naiomba Serikali ihakikishe wanajeshi wanalipwa stahiki zao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora; katika Jeshi linazungumzwa suala la utawala bora lakini mara kadhaa Jeshi linahusishwa na mambo ya kisiasa kwa kuegemea upande wa Chama Tawala (CCM). Nashauri Jeshi letu lisijihusishe na masuala ya kisiasa kabisa.