Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nashukuru kwa kupata fursa hii kuchangia kwenye hii Wizara ambayo ina uhusiano mkubwa sana na mkoa ambao nauwakilisha kwa maana ya Mkoa wa Singida. Mkoa wa Singida ni miongoni mikoa ambayo inafanya vibaya sana katika suala la taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea, naomba mama yangu, Mheshimiwa Waziri Ndalichako, wakati unakuja kuhitimisha nakuomba uje na majibu ya kwanini Walimu takriban 366 wanaotokea Mkoa wa Singida Wilaya ya Iramba hawajapandishwa madaraja toka mwaka 2013 na wakati katika mkoa huu Wilaya nyingine zote Walimu wao wamepandishwa madaraja, lakini kasoro Wilaya ya Iramba peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote humu ndani tunatambua kwamba dunia ya sasa ni dunia ya ushindani, silaha pekee kwenye dunia ya ushindani ni elimu; lakini cha kusikitisha ni kwamba elimu inayotolewa katika Taifa letu ni elimu duni kabisa. Ni elimu ambayo haijakidhi vigezo. Nasema hata kwa sababu hapa nina taarifa ya USAID ya mwaka huu ambayo inaonyesha kwamba asilimia 70 ya wanafunzi hawajui kusoma Kiswahili, Shule ya Msingi na wakati huo huo asilimia 90 ya wanafunzi hawajui kusoma Kiingereza. Kwa tafsiri nyingine ya watu, hata kuandika barua ya kuomba kazi hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Vyuo Vikuu vilivyopo katika Taifa letu, kuna baadhi ya Vyuo Vikuu kwa sasa vimeamua kupanua magori kuhakikisha kwamba wanaanza kusajili wanafunzi kutoka Form Four kwa sababu kuna wanafunzi wa Form Six hawajakidhi vigezo kuingia Vyuo Vikuu. Takwimu ya TCU ya mwaka 2015 inaonyesha kwamba kuna nafasi 25,000 zimeshindwa kuwa fulfilled kwa sababu wanafunzi hawajakidhi vigezo vya kwenda University. Hii inasikitisha sana na ni aibu! (Makofi)
Sasa katika kutafakari, nikaangalia, msingi wa haya ni nini? Sababu kubwa, kwanza ni kwa sababu hakuna mkazo kwenye suala la elimu. Hakuna mkazo ambao Serikali imepelekea kwenye suala zima la elimu. Niseme tu, nafikiri hii ni kwa sababu anguko la elimu katika Taifa hili haliwahusu Mawaziri, wala haliwahusu vigogo katika Taifa hili. Ila kwa sababu hiyo hapa we are not talking the same language! Hatuongei lugha moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema hivi: “kilio na mwenyewe.” Katika hali ya kawaida katika cabinet hii, msiba wa elimu, hamna member hapa kwenye cabinet ambayo inamhusu kwa namna yoyote ile. Kwa sababu asilimia kubwa watoto wao wanasoma nje na wengine wanasoma shule za private. (Makofi)
Kwa hiyo, ifike mahali tulitazame hili kwa sura nyingine. Mfano mzuri ni UK. Uingereza, Waziri kumpeleka mtoto wake kusoma shule ya private ni kashfa kubwa sana. Naomba kupitia Bunge hili Tukufu nimwombe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli atangaze rasmi Mawaziri wote wa Taifa hili, watoto wao wasome shule za government. Wasome shule za Serikali! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye suala la madawati, ni aibu! Eti wanafunzi milioni tatu na nusu, wingi wote huo wa wanafunzi, wanakaa chini. Upungufu wa madawati ni karibia 1,174,000. Ukiangalia gharama zinazoweza madawati haya, siyo chini ya shilingi ya bilioni 90 mpaka 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ni vema wakaona kwamba kuna umuhimu hata suala hilo wakalipeleka kwenye jeshi, jeshi likatutengenezea madawati wakawa wanalipa taratibu; au wakatumia mifuko ya hifadhi kuhakikisha kwamba mifuko ya hifadhi inakopesha wanajeshi halafu Serikali inakuwa inailipa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la ukaguzi. Unapozungumzia ukaguzi, ukaguzi una uhusiano mkubwa sana na performance ya mwanafunzi, kwasababu ukaguzi unapelekea kumtambua Mwalimu bora na ubora wa elimu wanayoitoa. Kwa Taifa letu ni aibu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Best Education Statistics za mwaka 2015, zinaonesha karibia asilimia 81 ya shule zote za Msingi hazijafanyiwa ukaguzi, lakini wakati huo huo asilimia 76 ya Shule za Sekondari hazijafanyiwa ukaguzi. Halafu mwaka 2015 mkatenga fedha shilingi bilioni 22.4 kwa ajili ya kupeleka kwenye ukaguzi, mkachukua shilingi bilioni 20 mkawalipa wakaguzi kama mshahara, halafu shilingi bilioni 2.4 ikatumika kwa ajili ya ukaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawasawa na Mbunge hapa amlipe dereva wake mshahara kila mwezi, halafu asiwe anamwendesha, awe anaendesha mwenyewe. Naona huu ni ubadhirifu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja anaitwa Aristotle aliwahi kusema hivi: “mizizi ya elimu ni michungu, lakini matunda ya elimu ni matamu.” Mimi nabadilisha kwa Taifa letu, “mizizi ya elimu ni michungu na hata matunda ya elimu ni machungu vile vile.” Tafsiri halisi ya elimu ni ili mtu atoe ujinga awe na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazomzunguka. Kwa Taifa letu, watoto wetu wanakwenda shuleni ili mradi wavae uniform wafanane na wengine. Ni masuala ya aibu, ambayo ni lazima tuyafanyie kazi haraka iwezekananyo, maana tunachekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba Waziri, mama yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako kama itakupendeza, muda wowote nikupatie majina haya ya Walimu wote ambao wana madai yao kwa ajili ya kuweza kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja, ahsante.