Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii muhimu kwa ulinzi wa mipaka ya nchi yetu dhidi ya adui wa nje, Jeshi la Wananchi la Tanzania lipo kuhakikisha linamlinda Mtanzania dhidi ya mataifa mengine na pale kunakuwa na utawala dhalimu basi Jeshi hushika hatamu. Ni kwa masikitiko makubwa Awamu hii ya Tano tumeshuhudia wanajeshi wakishushwa hadhi hadi kufikia kusafisha Jiji la Dar es Salaam, kupiga picha zilizo na mantiki wala taswira nzuri na Wakuu wa Mikoa hasa wa Dar es Salaam. Enzi nakuwa niliamini wanajeshi ni watu wenye mosi, kujitokeza kwa nadra sana mbele ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sote tunakumbuka hata wakati wa operation UKUTA ya CHADEMA tulishuhudia wanajeshi nao wakijiandaa kukabiliana na raia ilhali Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ipo kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, na kama kuna uhalifu wowote ichukue hatua. Hii ni sawa kuona Jeshi la Wananchi likifanya mambo kwa matakwa ya mtawala na hili limedhihirishwa dhahiri kwa kauli aliyoitoa Mkuu wa Majeshi Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Ofisi za Serikali kuwa wanafuatilia kauli za uchochezi na viashiria vyake na kuwa wapo tayari kuvidhibiti. Hii si sawa na wala si kazi ya JWTZ. Na hili linabidi likemewe kwa nguvu zote na kila mzalendo anayelitakia mema Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia kwenye hilo napenda sana Mheshimiwa Waziri atuambie wananchi wa Bugosi na Kenyambi ni lini watalipwa fidia zao stahiki kwa sababu wanajeshi walivamia lile eneo inasemekana ni baada ya kuvutiwa na mnara ambao Ndugu Thobias Ghati alikuwa ameingia mkataba na Kampuni ya Vodacom huku wakiacha kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto ambayo mosi ipo nje ya mji na mahali stahiki kwa wao kukaa maana miundombinu ya barabara na madaraja sasa imeimalika si kama awali. Lakini kama wameshindwa kulipa fidia kwa wakati wananchi wangu wanaomba wanajeshi wawapishe na warudi kwenye kambi yao, maana hili nimekuwa naliongelea tangu Bunge la Kumi na kila siku Waziri anaeleza watalipa mwaka wa fedha uliopo lakini hawalipi mwaka wa tisa huu sasa nikilisemea hili bila utekelezaji wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hivi wananchi hawa wamewakosea nini Serikali ya Chama cha Mapinduzi tangu mwaka 2008 wanashindwa kuyaendeleza maeneo wala kufanya shughuli za maendeleo maana wamezuiwa, hii si haki kabisa. Jana Tarehe 15 Mei, 2019 Waziri akijibu swali la Mheshimiwa Masoud alisema zile shilingi bilioni 20 zilizotengwa na Bunge tayari wananchi waliofanyiwa tathmini wamelipwa shilingi bilioni tatu, nauliza Tarime tulishafanyiwa tathmini kwa zaidi ya mara tatu bila malipo na hata juzi walikuwa huko, ni lini sasa tutalipwa? Naomba kupewa majibu yanayokidhi haja na yenye matumaini kwa wananchi wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niombe wanajeshi hao waliovamia maeneo ya Bugosi na Kenyambi ambayo yapo katikati ya mji basi iwapo mtalipa fidia wasizidi kujiongezea maeneo maana Tarime Mji hatuna maeneo ya kutosha na inakuwa na muingiliano mkubwa kati ya Jeshi na raia. Mwisho wa siku kwa principle za Jeshi unakuta wananchi wangu wanapitia dhoruba nyingi na mateso ya kijeshi pale wanapotumia public services zilizopo kwenye maeneo waliochukua na kibaya zaidi mnachelewesha fidia huku wanajeshi wamewazuia wananchi kuendeleza maeneo yao ila wao wanakodisha hayo maeneo waliopoka kwa raia na fedha wanazichukua, hii si sawa na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Kama kiongozi nimekuwa nikiwasihi wananchi wavumilie lakini uvumilivu una mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa Waziri utuhakikishie, kumbuka hata wale wananchi waliokuja mwaka juzi kukuona toka Tarime wengine ni wazee wanafariki kabla ya kupata haki yao si sawa kabisa. Mwisho naomba kujua kama Wizara inapata mapato ya ule mnara uliopo Bugosi ambao ulikuwa na mkataba kati ya Ndugu Thobias Ghati na Vodacom na baada ya wanajeshi kujichukulia maeneo yale waliamuru Vodacom walipe Mkuu wa Kikosi cha Makoko kinyume na sheria maana bado yule mwananchi hajafidiwa, hivyo ule mkataba ulitakiwa kuendelea mpaka pale watakapolipa fidia. Maana hapa si sawa na kuamuru mojawapo ya nyumba yenye wapangaji kuwa wale wapangaji walilipe Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Ndugu Thobias Ghati tunapenda kujua hizo fedha za mnara zimekuwa zikija Wizarani na kama ndivyo ni kiasi gani cha fedha kwa miaka yote hiyo? Na kama haziji ni hatua gani itachukuliwa sambamba na ukaguzi wa kina kwenye hilo suala la mnara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndio maombi na mchango wangu kwa leo ambayo ni Jeshi la kulinda mipaka ya nchi na sio kuingilia mambo ya ndani ya nchi. Pili fidia kwa wananchi wangu wa Mtaa wa Kenyambi, Kata ya Nkende na Bugosi Kata ya Nyamisangura pamoja na mapato ya mnara uliopo kwenye eneo la Ndugu Thobias Ghati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.