Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: AhsanteMheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali, napenda kuipongeza pia Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa wanayoifanya kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakua, kinakua endelevu na chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa kuitoa Tume ya Umwagiliaji kwenye Wizara ya Maji na kuipeleka kwenye Wizara ya Kilimo. Tume hii kupeleka kwenye Wizara ya Kilimo imefika hasa pahali pake; kwa maana kwamba Wizara ya Kilimo sasa itaitumia Tume hii ya Umwagiliaji kwa kukuza kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Tume hii ya Umwagiliaji lazima sasa Wizara ijipange vizuri ili kuhakikisha Tume hii watendaji wake wanafanyakazi kwa uadilifu na weledi. Ili kuifanya Tume hii ya Umwagiliaji iweze kufanya kazi zake vizuri ni vyema sasa miundombinu yote ya umwagiliaji inayohusu kilimo iangaliwe upya kuhusu kodi; ikiwemo mitambo ya kuchimbia mabwawa, vifaa vyote vya umwagiliaji pamoja na mitambo ya kuchimbia visima vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiliangalia hili la kodi miradi ya umwagiliaji itakuwa na wananchi watahamasika sana kulima kilimo cha umwagiliaji. Kutokana na hali na mabadiliko ya tabia nchi kilimo cha umwagiliaji ndiyo mkombozi wetu wananchi wa Tanzania. Kwasababu kilimo hiki kitakuwa endelevu na cha muda wote kwa maana hiyo viwanda vyetu sasa vitapata malighafi ya kutosha na kwa muda wote. Pia kilimo cha umwagiliaji kitatuweka vizuri katika usalama wa chakula na kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, katika kuimarisha kilimo chetu nchini ni vyema sasa tukawekeza zaidi kwenye utafiti. Tuingize nguvu zetu nyingi katika utafiti katika kupata mbegu bora ambazo zitatoa mazao mazuri yenye tija. Kwa faida ya kilimo hiki ni vyema sasa tukaziimarisha hizi taasisi zetu za utafiti kama TARI, Taasisi zetu za kutayarisha mbenu kama ASA, tukazipa mitaji ya kutosha ili ziweze kufanyakazi zake vizuri kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na hasa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali na Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha kitengo cha kutafuta masoko ya kilimo. Kitengo hiki kitakuwa mkombozi na mtatuzi wa changamoto za mazao yetu ya kilimo katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha mradi wa kudhibiti sumu kuvu. Sumu kuvu ilikuwa ni tatizo kwa mazao yetu; na kwa vile mwananchi alikuwa hajui sumu kuvu ni nini kwahiyo baadhi ya wananchi walipoteza maisha kutokana na kula vyakula vilivyokuwa na sumu kuvu. Kwahiyo naipongeza hii Wizara kwa kuliona hili na kuhakikisha kwamba mazao yetu yanakuwa hayana sumu kuvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti ya kilimo. Bajeti ya kilimo imeongezeka. Pia napenda kuishauri Serikali iendelee kuongeza bajeti ya kilimo ili kukidhi matakwa na mahitaji yote ya Wizara ya Kilimo na taasisi zake zote. Bajeti ikiongezeka taasisi zote zitapata fedha na miradi ya kilimo itaongezeka kwa kupata mbegu bora viuatilifu bora na mengineyo. Naipongeza Serikali kwa kuona nakupunguza tozo mbalimbali za kilimo, lakini pia naishauri Serikali iendelee kuangalia tena uwezekano wa tozo na vikwazo au changamoto mbalimbali inazokabili sekta hii ya kilimo ili wananchi wahamasike kulima kilimo chenye tija na kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imechambua kwa kina sana kuhusu zao la korosho, naipongeza sana kamati kwa ushauri wake kwa Serikali, na ninaamini kwamba Serikali haina nia mbaya na wananchi au wakulima wa korosho. Wakulima wa korosho watalipwa na watapata haki zao kwasababu najua Serikali iko mbioni sasa kuhakikisha madeni yote yanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyongeza tu, na mimi napenda kuongeza kwenye korosho kwamba waangalie pia na wadai wa korosho wa mwaka 2017/2018, kwa sababu nako huku kwenye vyama vya ushirika vimewatapeli wananchi wetu wakulima wa korosho kwa madai yao ya mwaka huu. Kwa hiyo Serikali itakapoandaa mchakato wa kuwalipa wananchi na wakulima wa korosho iangalie pia na wale wa mwaka wa jana; kwa sababu tunataka kilimo cha korosho kiwe endelevu na chenye tija mazao yaongezeke tupate mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naipongeza sana Wizara ya Kilimo kwa jitihada mbalimbali za kuendeleza kilimo nchi Tanzania na Serikali yetu kwa ujumla ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais wetu kuhakikisha kwamba kilimo kinakua, kilimo chenye tija kwa ajili ya biashara na mtaji au rasilimali muhimu na mali ghafi kwa viwanda vyetu tunavyovijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti,, naunga mkono hoja, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipa nafasi.