Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami kwa niaba ya wanawake wenzangu walioko ndani ya ukumbi huu na wanawake wa Tanzania ambao sisi Wabunge wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunawawakilisha, napenda kuunga mkono azimio hili lililowasilishwa asubuhi ya leo kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya kwanza naunga mkono azimio hili la kumpongeza Rais kwa sababu Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikubali kwa niaba ya Watanzania kwamba Mkutano huo wa SADC ufanyike nchini Tanzania ambako ni heshima ya Watanzania wote na ikiwa ni ishara tosha ya kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Karume.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono azimio hili kwa sababu ni ukweli usiopingika Mkutano wa SADC uliandaliwa vizuri chini ya uongozi wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli mkutano huu ulitupa hadhi na heshima Watanzania kuendelea kuwa champion wa ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo nchi za SADC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono, azimio hili la kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu amepokea kijiti hiki cha kuwa Mwenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais wa Namibia ikiwa nchi ya Tanzania na nchi za SADC tukiwa na amani na usalama. Ninapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono azimio hili la kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si mwingine ni kipenzi chetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, aliongoza vema Mkutano wa SADC haijapata kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono kwa sababu kupitia Mkutano wa SADC Rais wetu kipenzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishawishi Marais wenzake na wakakubali lugha ya Kiswahili, lugha ambayo ni tunu ya Tanzania iwe sasa ni lugha ya nne katika nchi za SADC. Haijapata kutokea na katika hili hatutakaa tumsahau Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuleta azimio hili tumpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kweli tunampongeza na tunakushukuru sana. Naunga mkono azmio hili la kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameendelea kushawishi Marais wenzake na nchi za SADC ziendelee kujitegemea kiuchumi kwa kutumia rasilimali zake ili nchi za SADC ziondokane na utegemezi; na akanukuu akasema, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na pale alipopumzika alisema kujitawala ni kujitegemea na mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe; na uwezi kuwa uhuru kama nchi yako haijitegemei. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kusisitiza nchi za SADC kujitegemea na yeye mwenyewe akawa ndiyo mfano wa kuifanya Tanzania sasa ijitegemee na mfano hata wa bajeti hii, tulikuwa ni tegemezi kwa asilimia 40. Sasa Tanzania tunajitegemea kwa asilimia nane. Hiyo peke yake tuna kila sababu ya kutaka kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naunga mkono azimio hili, hongera sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Wanawake wa Tanzania tunakupongeza tuko pamoja na wewe. Ninachokuhakikishia, uchaguzi wa 2020 kura zote ni zako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono azimio hili. (Makofi)