Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuunga mkono azimio lililoletwa leo asubuhi. Kwanza nami nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwanza kwa kukubali mkutano kufanyika Tanzania. Ni kweli mikutano ya SADC ni rotational lakini angeweza kukataa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kama hali yetu ya pili isingekuwa nzuri, bado hata wenyewe watu wa SADC wasingeleta mkutano Tanzania. Kwa hiyo, ni vizuri tuelewe mkutano umekuja Tanzania kwa sababu ya utayari wa Rais wetu, ulikuja kwa sababu Tanzania tupo tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza kwa sababu kwanza kama walivyosema wenzangu, Tanzania ndiyo kitovu cha ukombozi wa Bara la Afrika hasa upande wa Kusini mwa Afrika; na kwa wale mnaokumbuka, wakati wa liberation struggle, ile committee ya liberation struggle, Katibu Mtendaji wa kwanza alikuwa Marehemu Balozi George Magomba baadaye akafuatiwa na Ndugu Brigadier Hashim Mbita. Kwa hiyo, Tanzania tumefanya kazi kubwa sana kwa ukombozi wa Kusini mwa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono na nikiomba Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti wetu mpya wa SADC, kazi ya ukombozi Kusini mwa Afrika imekwisha, nadhani umefika wakati na Rais amesema huu ni wakati wa ukombozi wa uchumi wa Kusini wa Bara la Afrika. Nina uhakika Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli atalisimamia hili kama Mwenyekiti mpya wa SADC kuhakikisha tunaondoa vikwazo vya kufanya biashara kati ya nchi wanachama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alipokuwa anafungua Bunge la South Africa mwaka 1994 aliwaambia wa South Africa msijigeuze kuwa kaka wakubwa, South Africa hamna jirani, jirani yenu ni sisi Waafrika wenzenu. Akasema ili block hii iweze kuendelea, lazima tufanye biashara ndani ya wanachama wenyewe. Kwa hiyo, ni matarajio yangu na ninayo hakika Mwenyekiti mpya wa SADC atafanya yafuatayo: moja, akisaidiwa na Waziri wa Mambo ya Nje kuhakikisha tunaondoa vikwazo vya kufanya biashara ndani ya nchi wanachama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, ili tuweze kufanya biashara na wananchi wanachama, umefika wakati lazima tutafakari, hivi kwenda Kongo ni lazima niwe na visa? Hivi Mkongoman lazima awe na visa kuja Tanzania? Hivi Wamalawi lazima wawe na visa kuja Tanzania? Tukifanya hivyo, nina hakika biashara kwenye nchi hizi itashamiri na ninayo hakika hii ndiyo itakuwa legacy atakayoiacha Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli.

Mheshimiwa Spika, ninapongeza kwa sababu mkutano wenyewe umefanyika kwanza kwa utulivu mkubwa sana, lakini pia umefanyika kwa ushirikishwaji wa watu wengi sana. Kwa mara ya kwanza mkutano wa Kitanzania; na ninawapongeza walioandaa mkutano huu, tumeona private sector ikishiriki kuhakikisha mkutano huu unafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nami nashukuru sana na ninamtakia mema Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa hiyo aliyoianza. Moja legacy ya kwanza kama mnavyofahamu Bunge hili, kazi ya kwanza Rais amefanya kwenye SADC ni kufanya Kiswahili ni kuwa lugha ya SADC. Kwa hiyo, mtu yeyote mwenye wasiwasi wa legacy ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwenye SADC, legacy ya kwanza ni Kiswahili. Ninaamini legacy ya pili itakuwa ni biashara ndani ya nchi ya wanachama na legacy ya tatu nina hakika itakuwa kuhakikisha katika nchi za SADC kunakuwepo na utulivu na amani kama ilivyo Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba niunge mkono azimio hili. Namtakia maisha mema Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti mpya wa SADC.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)