Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami sasa niweze kuchangia Wizara hii muhimu ambayo kwa kweli na mimi naomba ku-declare interest kwamba mimi pia ni Mwalimu kama ambavyo wengine wame-declare interest. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili bajeti ya Wizara ya Elimu, wanafunzi ambao wako Vyuo vya Elimu ya Juu, tangu wamefungua chuo hawajapata mkopo; na hili ni jambo la kusikitisha sana. Imefika mahali wanafunzi wetu wanacheleweshewa mikopo na mikopo ambayo mwisho wa siku watakuja kuirejesha, lakini wanapokuwa sasa wanadai hizo fedha, tunaenda kuwapiga mabomu, tunawapelekea Polisi jambo ambalo linasikitisha sana. Kiukweli kabisa kama mikopo inakuwa inacheleweshwa, nadhani mtu wa kwanza kupigwa bomu inatakiwa awe Waziri wa Elimu na Watendaji wake lakini siyo wanafunzi wetu. Tunawaonea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba japokuwa pia wenzangu amegusia sana kwenye suala hili la Bodi ya Mikopo, naomba nami niguse baadhi ya vitu pia. Kuna kitu fulani kinaitwa Quality Assurance Fee kwenye elimu ya juu. Mwanafunzi anaambiwa alipie shilingi 20,000/= kwa ajili ya kudhibiti ubora wa elimu. Kimsingi jukumu hili la kudhibiti ubora wa elimu ambalo linafanywa na TCU ni jukumu la Serikali. Hivyo, kumbebesha mwanachuo mzigo, ni suala ambalo kwa kweli haliruhusiwi hata kidogo! Kwasababu TCU ni sehemu ya majukumu, inakuwaje tunakwenda kumbebesha mzigo mwanafunzi masikini? Kwa kweli hali hii inasikitisha sana na sidhani kama inatakiwa tuendelee kuivumilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na sifa ambazo amepewa mimi sitaki kumsifia, kwasababu siwezi kumsifia mtu wakati ni majukumu yake. Naomba suala hili ukaliangalie sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala linguine, kwenye elimu ya juu. Leo wanafunzi hakuna mawasiliano kati ya Wizara ya Ulinzi pamoja na Wizara ya Elimu. Wametangaza kwamba wanafunzi waliomaliza Form Six waende JKT kuanzia tarehe 1 mwezi wa Sita hadi tarehe 6 walipoti JKT. Wakati wowote kuanzia sasa wanafunzi watahitajika kuomba mkopo waliomaliza Form Six. Tafsili yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba wanafunzi wanaoenda JKT wengi wanakosa fursa ya kuomba mkopo. Mwaka 2015 wanafunzi 80 waliokwenda JKT walikosa mkopo Chuo Kikuu cha Dar es salaam peke yake sehemu ya Mlimani. Kwenda JKT imekuwa dhambi leo hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili Mheshimiwa Waziri aliangalie sana, kuwe na utaratibu maalum; kabla hawajaenda JKT, waombe mkopo mapema ili wanapomaliza pale waende chuo tayari wakiwa wameshaomba mkopo. Kama tatizo ndiyo hilo, mwisho wa siku watu watasema kwamba JKT hatuendi kwasababu tukitoka JKT tutakosa mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana. Hakuna mawasiliano kati ya TCU na Bodi ya Mikopo. Kwanini nasema hakuna mawasiliano? Leo ukisoma kitabu cha TCU kinakuonesha kozi ambazo ukienda kusoma utapata mkopo (priority course), lakini wakati huo huo anapoomba mwanafunzi kozi hizo kwenda kusoma Bodi ya Mikopo inasema kwamba hizi kozi siyo za mkopo. Hakuna mawasiliano kati ya Bodi ya Mikopo pamoja na TCU. Alishaongea Mheshimiwa Godbless Lema kwamba hii nchi imekuwa kama ghetto, hamna utaratibu, nami nadiriki kusema kwamba nchi hii ni kweli hakuna utaratibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme maneno makali, tunaendesha nchi utafikiri ile nchi ya kijuha, kwasababu kama Bodi ya Mikopo ni chombo cha Serikali, TCU ni chombo cha Serikali hawa wanakwambia hii kozi inakopesheka, ukienda kule wanakwambia hii kozi haina mkopo. Maana yake ni nini? Mheshimiwa Waziri, naomba ukaliangalie hili. Kama Taifa tunaaibika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nizungumze suala linguine. Leo kuna changamoto nyingi sana katika elimu ya juu. Ukienda katika hostel za wanafunzi wetu; kwa mfano pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tu sehemu ya Mlimani, wanafunzi ambao hostel inaweza ku-accommodate ni wanafunzi 6,500, lakini idadi ya wanafunzi ni 18,000. Wanafunzi wengi wanabebana, wanalala wawili kwenye kitanda kimoja. Hali ambayo ni mbaya sana! Leo hii kama kuna fedha inatakiwa zipelekwe basi zinatakiwa zipelekwe kwenye elimu ya juu za kutosha. Kama Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alipeleka pesa kwa Mahakimu akasema hakuna pesa, kesho kutwa kapeleka; baada ya siku mbili akapeleka, leo mnaonaje kupeleka pesa elimu ya juu? Pesa zipo. Tatizo la nchi hii siyo pesa, tatizo la nchi hii ni uongozi mbovu ambao nadhani kwa muda mrefu sana tumekuwa tukilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumze suala lingine kuhusu mfumo wa uandaaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia. Leo kutokana na elimu yetu jinsi ilivyo, kila mtu anapanga la kwake. Akilala Mheshimiwa Waziri anaamka asubuhi anasema, leo tunachanganya Physics na Chemistry, wanafunzi wanaanza kusoma. Kesho mwingine anarudi anasema hapana ulikosea. Hii hali ni kwasababu ya kukosa uongozi bora. Tatizo ni Uongozi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee, leo tunataka elimu yetu iwe bora, kuna tatizo la kutowalipa Walimu wetu wanaoidai Serikali. Nataka nitoe mfano mdogo tu. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Walimu wanainaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 800 na kitu, hawajalipwa. Watoto wetu watafaulu vipi kwa namna kama hii ambapo Walimu waliokata tamaa wanaidai Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Momba wanaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 600. Walimu hawajalipwa hizo fedha! Ileje Walimu wanaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 400, hawajalipwa. Unataka watoto wafaulu vipi? Suala hili halihitaji kufunga kwa maombi wala kupiga ramli, tatizo ni Serikali! Walimu wengi wameshakata tamaa. Suala hili lisiposhughulikiwa kwa kweli tutaendelea kulia na vilio vyetu havitaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee, kuna Walimu wamesimamia mtihani a Kidato cha Nne mwaka 2015 hawajalipwa fedha zao, karibu shilingi milioni 118 Halmashauri ya Mbozi; leo ni nani Mbunge hapa, ni nani Waziri hapa ambaye posho yake ya mwaka 2015 hajaichukua? Posho yake ya mwaka 2014 hajaichukua! Mshahara wake wa mwezi uliopita hajachukua? Ni nani Waziri hapa au Mbunge? Tuwaonee huruma Walimu! Walimu hawa waliokata tamaa mwisho wa siku wakianza kuandamana, msije mkaanza kutafuta mchawi ni nani. Mchawi ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu hawa walipwe fedha hizo na wasipolipwa fedha hizo kwasababu sisi ni Wawakilishi wao, nimechangia hata mara ya kwanza nilizungumzia suala hili; tuataenda kukaa nao, ikiwezekana tuingie barabarani. Muwe tayari kutupiga na mabomu! Sawasawa! Kwasababu hatuwezi kuvumilia Walimu wetu wanateseka! Hata mimi pia ni Mwalimu, nina uchungu sana! Naomba kama kweli tunawapenda Walimu wetu, tukalipe fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, bado kuna suala la makazi bora ya Walimu, ni tatizo! Ameongea mwenzangu pale kwamba ametokea mahali, kwa mfano wanasema hii ni TAMISEMI, hii ni wapi; lakini makazi bora kwa Walimu ni tatizo. Kuna shule moja ambayo nilikuwa nafundisha kabla sijawa Mbunge, shule hiyo ina nyumba moja tu ya mwalimu. Walimu wanalala nane kwenye nyumba moja. Unaweka kitanda, unaweka godoro chini, this is shameful! Kwa kweli suala hili ni aibu sana, Serikali hii lazima ifike mahali iangalie sana kwenye suala la elimu, ahsante.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Yohana. Tunaendelea na..
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba nisiunge mkono hoja na nimshukuru sana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuichapa; tunamuunga mkono, Mungu ibariki UKAWA. Ahsante sana.