Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpendae
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALIM HASSAN TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana wa Taallah kwa kutujalia sisi tulioko humu wazima wa afya. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Waziri wetu wa Mipango kwa kweli mpango aliouleta ni mzuri sana na madhubuti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea na safari hii pia nataka nimpongeze sana Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi ambaye ndiyo Rais wa nchi hii, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayotufanyia ya kutaka kuhakikisha kwamba Tanzania tunaingia katika uchumi wa kati. Sitaki kutafuna maneno, wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani na alipotoa matamko yake yale kwa kweli nilipigwa na butwaa nikasema hivi kweli mambo haya yanawezekana kwa kipindi hiki kifupi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ameweza kuthibitisha na mimi nachukua fursa hii kumpigia salute kabisa kwamba, kwa kweli anatupeleka kwenye maendeleo makubwa sana japo njia ni ngumu lakini dalili njema zimeshaanza kuonekana. Katika hilo wakati akiwa kama Waziri alikuwa akipiga kelele sana hapa kutaka madaraja yale ya ubungo pamoja na airport lakini nashukuru alipoingia madarakani tu alihakikisha daraja lile la pale njia ya airport TAZARA linasimama la Mfugale mara moja na limesimama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa sisi ambao tunatoka Zanzibar kuja Dar es Salaam na Dar es Salaam Zanzibar, kwa kweli njia sasa hivi imekuwa ni ya muda mfupi sana. Kwa hiyo, hizi nia ambazo amezipanga, Mwenyezi Mungu azibariki na amjalie afya njema. Kwa wale wanaomtakia mabaya Mwenyezi Mungu amwepushe nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare interest kwamba ni mfanyabiashara pamoja na viwanda, kwa hiyo, mada ambazo nitaongelea ni hizo na nitaanza na viwanda. Juzi moja tulirushiwa clip nzuri sana ya viwanda kutoka Ethiopia. Kwa kweli ukitaka kujifundisha jambo lolote, tushindane kwa mazuri. Katika Afrika yetu hii, Ethiopia ndiyo inaonekana kwamba ni nchi moja iliyojizatiti kweli kweli kutokana na umasikini na kuendelea mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walichokifanya wao kama Serikali, wametafuta wawekezaji wakaingia nao ubia, wakajenga eneo kubwa sana la viwanda. Wamejenga eneo hilo na kuwakaribisha wawekezaji. Kwa hiyo, mwekezaji anapokuja nchini, hahangaiki tena kwenda kutafuta maeneo ya kuwekeza, kuanza kutafuta umeme na maji. Hayo yote yamepitwa na wakati katika dunia hii tunayokwenda nayo. Kwa hiyo, inatakiwa katika eneo hilo sasa hivi Serikali na labda Mheshimiwa Waziri wa Fedha akija katika mipango yake atueleze kwamba amejipanga vipi? Kwa sababu eneo hilo linafanya kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hata katika kurejesha pesa kwake kwa mradi ule, wao watazame zaidi kwamba ile miradi inapokuja nchini, wananchi wetu wapate ajira. Kwa mfano tu leo, Tanzania tuko nyuma sana katika viwanda vya nguo. Tuna pamba ambapo leo Mheshimiwa Waziri ametoa tamko hapa nimemsikia kwamba pamba inayotakiwa kwa viwanda vyetu ni nyingi kuliko tunayozalisha. Kwa hiyo, tayari zile kelele za watu wa maziwa kule kupiga kelele hilo jambo naona limeshapata ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ili tutoke hapa, tunafanyaje? Nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mwijage alipokuwa hapa alisema kwamba anataka kila mtu awe anazalisha na kushona nguo. Vita vikubwa vya kushona nguo Tanzania ni kuruhusu mtumba. Mitumba inadumaza viwanda vya nguo. Kama hatutajipanga vizuri, naamini kwamba kuna nguo ambazo tunanunua China zinauzwa rahisi sana. Je, zikishonwa na pamba yetu wenyewe hapa Tanzania bila kusafirishwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna haja ya makusudi kujipanga kuhakikisha kwamba hilo eneo la viwanda linasimamiwa kwa nguvu zote na ile kodi ikawekwa ndogo sana ili wananchi waweze kunufaika na ajira na mapato ya Serikali yatakuwa makubwa sana kwa kupitia huduma mbalimbali katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, mwanzo wa kipindi hiki cha tano tulikuwa tunasimama hapa Bungeni na kupiga kelele, nami wakati ule nilikuwa niko katika Kamati ya Viwanda na Biashara, tulifanya ziara bandarini na tukasema kwamba sasa hivi watu wote wamekimbia bandari yetu kutokana na tozo zilizopangwa kwa wakati ule; mambo ya VAT na nini yaliyowekwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana ziara ile ilizaa matunda; Waziri na Serikali ambayo ni sikivu waliona upungufu wakajirekebisha. Sasa hivi naweza kusema kwamba Bandari ya Dar es Salaam imechangamka mia kwa mia. Nampongeza sana Mkurugenzi Mtendaji wa TPA kwa kazi kubwa anayofanya pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mwaka ule wa kwanza watu waliyachukua magari yale ya kusafirisha makontena wakapeleka nchi jirani. Hivi ninavyoongea na Bunge hili, kuna upungufu mkubwa sana wa magari ya kusafirisha container katika Bandari yetu ya Dar es Salaam, kwamba biashara imekubali Bandari ya Dar es Salaam. Naipongeza sana Serikali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili biashara hiyo iwe nzuri zaidi, Serikali imejipanga kwa kujenga bandari kavu mbalimbali. Serikali hiyo hiyo ilitoa tamko kwamba zile ICD za watu binafsi zote ambazo ziko katika mji wetu wa Dar es Salaam zihame ziende katika umbali wa kilometa 35 nje ya Dar es Salaam ili kuondoa msongamano wa magari. Hilo ni jambo jema sana ambalo limepangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi iko tayari kujenga ICD mbalimbali nje ya Dar es Salaam. Serikali inapanga bandari kavu sehemu mbalimbali, ni jambo jema sana, lakini naomba sana TPA, hao watu wanaotaka kujenga ICD nje ya Dar es Salaam, walipoenda kuwaomba kwamba waweke wakaambiwa kwamba tutawapa ruhusa ya miaka miwili, baada ya hapo, kama Serikali ikiwa imeshajipanga, basi itakuwa wamefeli wao. Hilo jambo limewatisha private sector.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo, naiomba sana Serikali yangu itazame uwezekano kwa sababu sasa hivi tunachoongelea hapa kwamba Bandari ya Dar es Salaam inazidi kujengwa na ninaamini muda siyo mrefu nchi jirani zote mizigo yao itakuwa ikipitishiwa hapa na hasa reli itakapoanza. Kwa hiyo, makontena yatakuwa ni mengi mno. Nafikiri Serikali haina haja ya kuwa na hofu na private sector, hawa ni partners wetu, twende nao sambamba watatusaidia kama wanavyotusaidia sasa hivi. Sasa hivi mizigo tena imejaa katika ICD za private kwa sababu mzigo umeshakuwa mwingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bora Serikali ikatoa tamko kuhakikisha kwamba tunapanga mipango mizuri ya kwenda pamoja. Tusitanguliane private na Government Sector ni partners, tutembee pamoja tutashinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Zanzibar na siku zote napendelea sana Zanzibar na Bara tuwe ndugu wa kupendana na kushirikiana na tusiwe washindni. Ila tunapoingia katika uchumi, tunaona kuna ushindani mkubwa sana. Ushindani gani?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Turky, muda wako umekwisha. Kengele ya pili imeshagonga. Ahsante sana. (Makofi)