Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango huu wa Maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018, nilisimama hapa na nikaongea na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango kumwambia kwamba mipango tunayoipanga kama Taifa na Bunge likaridhia na tukapitisha, ni vyema Serikali ikasikia yale ambayo tumeyashauri na kuyatendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina zaidi ya asilimia 70 ya wananchi ambao ni wakulima. Cha kushangaza, bajeti iliyopita tulipata shilingi bilioni 100 iende kwenye kilimo ili iweze kusaidia shughuli mbalimbali ikiwemo utafiti, shughuli za kilimo na mambo mbalimbali ya Wizara husika. Napenda kusikitika kwamba imetoka shilingi bilioni mbili peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kilimo ni uti wa mgongo, kwa sababu najua kauli hii haijatenguliwa toka tumepata uhuru wa Taifa hili; leo hii ambapo wakulima ni wengi huko vijijini na hususan wanawake tunaowawakilisha, kama hujapeleka pesa unakuwa hujawatendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ufanikiwe katika viwanda, tunasema kwamba sasa hivi tunaenda kwenye viwanda vya kati kama Taifa. Usipowekeza kwenye kilimo, ambapo kilimo ndiyo kinatoa malighafi kwa viwanda hivi, unakuwa bado unafanya siasa kwenye mambo ya makini ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika asilimia 100 ya bajeti ambayo Bunge lako Tukufu lilipitisha, asilimia 98 ya gawio la fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango haikupelekwa. Ninaomba tunapopanga vitu na Bunge lako likaridhia, Serikali na Wizara iweze kuachia fedha kwa ajili ya watu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani ni wachache. Kwa mfano, nikichukua tu kwenye Wilaya ya Rungwe, wasimamizi wa kilimo wako wachache, hawawezi kufikia wakulima wote. Tuna Chuo cha Uyole Mbeya; Chuo kile kinasaidia utafiti. Huwezi kuwa na kilimo kisichokuwa na Utafiti. Tunataka kujua ni ng’ombe gani bora wenye mbegu bora kwa ajili ya kilimo? Utawezaje kujua pasipo utafiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, chuo kile takribani miaka mitatu sasa hakijapelekewa fedha za maendeleo, unawezaje kuwasaidia wasomi hawa ambao wanasimamia raslimali za Taifa na ni washauri wa kundi kubwa la wakulima? Hawana fedha. Naomba Wizara yako Mheshimiwa Dkt. Mpango iliangalie suala hili kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia pembejeo. Tumekuwa na kilio kikubwa sana juu ya pembejeo. Leo hii kuna mbegu za aina mbalimbali na nyingine hazioti, wakulima wanalalamika. Tumesema Maafisa Ugani ambao wangetusaidia, leo hii ajira ya kuwaleta na kutuongozea kule vijijini hawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tujipange na bahati mbaya sana tumebaki na mwaka mmoja kama siyo miezi sita ili tuweze kumaliza mipango tuliyokuwa tumejiwekea. Naomba tafadhali tusimame kwa yale tunayoyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumzia mbolea, kuna sehemu nyingi sana; sehemu za Mbarali na sehemu nyingine mbalimbali ambazo mimi nawakilisha, mbolea inaenda kwa kuchelewa. Wakati mwingine Mawakala mnaowapa wamekuwa hawawatendei haki wakulima jinsi ambavyo ilipaswa wafanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niache hapo, niende kwenye suala la elimu. Taifa lolote likitaka kukandamiza watu wake linaweka elimu kuwa ni ya hali ya chini. Usipowekeza kwenye elimu, umeandaa jeshi la watu wajinga ambao watakuwa rahisi sana kupotea. Elimu kwa bajeti ya maendeleo iliyopita tuliweka shilingi bilioni 249. Sasa mnasema elimu bure, elimu isiyokuwa na malipo. Ni kweli ukitamka shilingi bilioni 200 kwa mwananchi wa kawaida anaona ni fedha nyingi, lakini ukienda kwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari kwa mfano, anakwambia amepewa shilingi 200,000/= Capitation. Shilingi 200,000/= anunue chaki, alipe mlinzi na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tunahitaji kuwekeza zaidi. Tunaposema bure, nafikiri bora turudishe kama tulivyokuwa mwanzo, kwa sababu wananchi walijitolea wakatusaidia, watoto wote walikula chakula cha mchana. Ukisema bure, kuna wazazi wengine wamegomba kutoa michango kwa sababu Serikali imesema elimu ni bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni nyumba za walimu. Hiki ni kilio kikubwa sana. Walimu wengi wamepanga, wanakaa mbali na maeneo ya shule. Mishahara haijaongezeka. Mheshimiwa Waziri, hebu tuwatazame walimu, maabara na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matundu ya vyoo ni tatizo hususani kwa watoto wa kike. Nazungumzia suala la bajeti. Tunapopitisha pesa, mashirika mengi, Wizara nyingi zinapata robo ya mapato inayostahili kupata. Sasa inakuwa kama vile; aidha mtuambie Serikali haina hela, lakini Serikali ya Awamu ya Tano inasema ina hela nyingi. Sasa bajeti ya shilingi bilioni 100, unapata shilingi bilioni mbili. Tunaomba maelekezo ya kina, kwa nini Bunge linapitisha halafu fedha inayotoka inakuwa kidogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni deni la Taifa. Mwaka 2018 nilizungumza juu ya deni la Taifa. Tumevuka sasa zaidi ya shilingi trilioni 50. Naomba, na nilisema mwaka 2018 pia, tusikope pesa. Tulete sheria humu Bungeni Serikali isikope mpaka Bunge liwe limeridhia. Hii tabia ya kukopa pesa hatujui tunalipaje, deni la Taifa limekuwa kubwa na mnasema ni deni himilivu na mna lugha zetu za kisomi, lakini mwisho wa siku wanaolipa madeni haya ni watoto ambao leo hawajazaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Dkt. Mpango ni msomi, naomba asimamie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mifugo na uvuvi ambayo ndiyo imeajiri sekta ya watu wengi. Kwenye uvuvi tulitoa shilingi bilioni nne ya maendeleo, tunarudi pale pale kwamba ni asilimia tatu ya fedha ndiyo iliyotoka. Tuna maziwa makubwa; Ziwa Nyasa, Ziwa Victori na Ziwa Tanganyika, kama Taifa tusipojipanga juu ya kutumia maziwa haya kuleta maendeleo kwa vijana wetu, nafikiri tutakuwa tunajidanganya. Unafanyaje maendeleo pasipo kuwawezesha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna maendeleo bila demokrasia. Ndugu zangu wameongea habari ya demokrasia. Leo hii tunapanga mipango lakini kwa njia ya figisu mmewaengua watendaji ambao ndio waleta maendeleo. Mnaendeleaje? Tukae chini kama Taifa, tuache uwoga, tufaanye kazi kama team. Leo hii mmeumiza watu wengi nafsi zao na kujiandikisha wameona ni kitu cha kupoteza muda. Tunaomba demokrasia ichukue nafasi yake. Wengine wameumizwa na wengine wako ndani. Hivi ni watu gani wajinga wasioona? Kwa sababu mwisho wa siku, watu wanaishi na watu kule chini. Mmetupa watu ambao sisi hatujawachagua, tunapangaje maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, demokrasia ni tunda la haki. Pasipo haki, amani haiwepo. Naomba tusimame na hilo, tuwasimamie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono Kambi Rasmi ya Upinzani. Ahsante. (Makofi)